Habari za Punde

Cuba Mshirika Mkubwa Katika Sekta ya Afya na Kilimo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Jamuhuri ya Cuba ukiongozwa na Naibu Waziri wa Kwnza Wizara ya Mambo ya Nje wa Cuba. Mhe,Marcelino Medina Gonzalez, kulia na kushoto Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ujio wa Viongozi Wakuu,Watendaji Waandamizi pamoja  na Wataaalamu kutoka Jamuhuri ya Cuba kuja Nchini Tanzania unathibitisha wazi Ushirikiano wa Kihistoria wa muda mrefu uliopo baina ya Mataifa hayo Mawili Rafiki.
Alisema yapo Maendeleo makubwa yaliyopatikana katika Sekta Tofauti za Maendeleo ikiwemo Afya, Kilimo na Elimu kufuatia ziara za mara kwa mara za Viongozi hao zilizoanza tokea kupatikana kwa Uhuru na Ukombozi wa Mataifa hayo.
Balozi Seif Ali Iddi akiiongoza Timu ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa sekta zenye mafungamano ya moja kwa moja na Taasisi za Serikali ya Cuba alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo Bwana Marcelino Medina Gonzalez Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Jamuhuri ya Cuba imekuwa Mshirika muhimu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa Zanzibar  katika Sekta za Kilimo na Afya zilizopata mafanikio makubwa yanayopaswa  kujivunia kutokana na mafungamano mazuri ya ushirikano wa Watendaji katika Sekta husika.
Balozi Seif alisema ongezeko la Madaktari Wazalendo 38 Visiwani Zanzibar kupitia Mpango Maalum ulioanzishwa kwa Ushirikiano kati ya Serikali ya Cuba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeiwezesha Zanzibar kuwa na Wataalamu wa uhakika wa kuimarisha huduma katika Sekta ya Afya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Naibu Waziri Mkuu huyo wa Mambo ya Nje wa Cuba ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Nchi hiyo kwa moyo wake thabiti wa kusaidia ufinyanzi wa Wataalamu wa Sekta tofauti hususan  ile ya Afya.
Balozi Seif  alimueleza Bwana Marcelino Medina Gonzalez kwamba huwezi kuizungumzia Tanzania na uhusiano wake wa kirafiki na Mataifa mengine ya kigeni bila ya kuitaja Jamuhuri ya Cuba.
Akigusia Sekta ya Kilimo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alieleza kwamba Zanzibar mepata mafanikio makubwa katika uzalishaji wa mazao mbali mbali ya Kilimo kutokana na mchango mkubwa wa Kitaalamu uliopatikana kutokana na Wataalamu wa Nchi hiyo Rafiki.
Alisema ukulima wa mazao ya Nafaka , Matunda na mboga mboga umekuwa ukiimarika na kuongezeka siku hadi siku kutokana na Teknolojia inayotumiwa na Wazalishaji  baada ya kupata elimu na maarifa yanayotokana na mchango wa Wataalamu wa Cuba.
Mapema  akitoa salamu katika Mkutano huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Marcelino Medina Gonzalez  alisema  uhusiano wa Cuba na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla utaendelea kuwa wa kudumu kwa faida ya maisha ya Vizazi vya sasa na vile vijavyo.
Bwana Marcelino Medina alisema uamuzi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kufikiria wazo la kufungua Ubalozi wake Mjini Havana Nchini Cuba ni uthibitisho sahihi ulio wazi wa uhusiano wa pande hizo mbili zilizoshibana Kidiplomasia.
Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Cuba alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  kwamba Utaalamu uliyofikiwa  na Taifa lake katika Sekta tofauti utaendelea kusambazwa katiba Mabara yote Duniani katika  azma  ya kuimarisha Uhusiano wa karibu.
Bwana Marcelino Medina alifahamisha kwamba  Serikali ya Cuba wakati wowote iko wazi na tayari kutiliana sanini Mikataba ya Ushirikiano baina yake na Taasisi inayomafungamano katika  Sekta inayoweza kupatiwa msukumo wa Kitaalamu kutoka Nchi hiyo.
Nao Mawaziri walioshiriki Mkutano huo, Waziri wa Afya Mh. Hamad Rashid Mohamed, Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Kilimo, Maliasili Mifugo na Uvuvi Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Riziki Pembe Juma walisema Cuba imeonyesha moyo thabiti wa kusaidia Harakati za Maendeleo ya Watu wa Zanzibar.
Mawaziri hao walisema wapo Wataalamu Wazalendo waliopata mafunzo ya muda mrefu na mfupi kutoka  Nchini Cuba  ambayo kwa sasa yanaendelea kufaidisha Wananchi walio wengi hasa katika Sekta za Afya na Kilimo.
Hata hivyo Mawaziri hao wameishauri Serikali ya Cuba kupitia ujumbe huo ulioongozwa na na Naibu Waziri wake wa Mambo ya Nje kufikiria uimarishaji wa Nyanja nyengine ya kiuchumi katika eneo la Utalii na Viwanda.
Walisema wakati Zanzibar imebarikiwa kuwa na rasilmali za kutosha  katika Sekta za Uwekezaji  Utalii Taasisi na Makampuni ya Taifa hilo la Amerika ya Kusini yanaweza kuitumia fursa hiyo muhimu itakayokuwa chachu ya kuendeleza mbele uhusiano uliopo.
 Balozi Seif Kulia akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Mamboi ya Nje wa Jamuhuri ya Cuba Bwana Marcelino Medina Gonzalez.
Naibu Waziri wa Mamboi ya Nje wa Jamuhuri ya Cubwa Bwana Marcelino Medina Gonzalez Kushoto akipokea zawadi ya Mlango wa Zanzibar kutoka kwa Balozi Seif Ali Iddi kama ishara ya kukaribishwa wakati wowote kuitembelea Zanzibar.
Balozi Seif  Kulia na Bwana Marcelino Medina Gonzalez wakifanya mzaha mara  baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.