Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein(katikati) akimzawadia Mwanafunzi Nasma Talib Saleh wa Skuli ya Sekondari ya SOS katika hafla ya kuwapongeza Wanafunzi waliofaulu Mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne na Sita pamoja kuwaandalia chakula cha mchana katika hafla iliyofanyika leo viwanja vya Ikulu Mjini Zanzibar,(kulia) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe.Riziki Pambe Juma
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ametangaza kuongeza nafasi
60 badala ya 30 alizozitoa mwaka jana za udhamini wa masomo kwa wanafunzi bora
wa Kidato cha Sita wenye viwango vya juu kabisa vya ufaulu.
Hayo aliyasema leo
katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi bora wa Kidato cha Nne na cha Sita
waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa, hafla ya kuwapa zawadi maalum
pamoja na chakula cha mchana alichowaandalia wanafunzi hao huko katika viwanja
vya Ikulu mjini Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema
kwamba idadi hiyo aliyoiongoza mwaka huu ni mara mbili ya nafasi za ufadhili wa
masomo ambazo zlizitoa mwaka jana kwa wanafunzi bora wa Kidato cha Sita.
Dk. Shein alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na utaratibu wa kuwapa
udhamini wanafunzi bora wa Kidato cha Sita wenye viwango vya juu kabisa vya
kufaulu kwa masomo ya sayansi na masomo ya sanaa.
Alifahamisha kuwa mwaka huu ameongeza nafasi hadi kufikia
60 badala ya 30 za mwaka jana kwani aliahidi kuendeleza utaratibu huo ili
kupata wataalamu wa fani mbali mbali watakaoendelea na masomo yao ndani na nje
ya nchi.
Rais Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa wanafunzi wote watakaopata fursa hio ya udhamini
wa masomo na kuwasihi kuzitumia ipasavyo.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa wanafaunzi 187 waliofaulu kwa daraja la kwanza
katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka jana pamoja na skuli bora kumi ambapo
ufaulu wa mwaka jana ulikuwa ni wanafunzi 135.
Pongezi maalum
alizitoa Rais Dk. Shein kwa kijana Hassan Ali Hamad wa Skuli ya Sekondari ya
Lumumba kwa kupata pointi saba na kuwatangulia wenzake wanne kati ya vijana
watano waliofanya vyema zaidi katika mitihani hiyo ya Kidato cha Nne mwaka
2018.
Kadhalika,
aliwapongeza wanafunzi wote 188 wa Kidato cha Sita hasa vijana wanne waliofaulu
kupata pointi nne kila mmoja na kuonesha uwezo mkubwa walionao zaidi ya
wenzano.
Aliongeza kwua mwaka
jana kwa Kidato cha Sita kwenye daraja la Kwanza walikuwa wanafunzi 126 ikiwa
ni ongezeko la wanafunzi 62 sawa na ongezeko la asilimia 49.2 na kutoa pongezi maalum
kwa Wahda Mbaraka Uzia kutoka Skuli ya Sekondari ya FEZA kwa kufanikiwa kuwa
miongoni mwa wanafunzi bora wanawake kwa Tanzania kwa masomo ya Sayansi.
Alieleza kuwa kwa mara
nyengine tena wanafunzi wa kike wameonesha uwezo wao mkubwa wa kufanya vyema
katika mitihani ya Taifa na hasa kwa masomo ya Sayansi na kuwapongeza wanafunzi
wa kike kwa kuonesha uwezo huo.
Rais Dk. Shein
alisisitiza kuwa hatua hiyo mbali na kuiletea sifa Zanzibar pia, ni mafanikio
katika malengo ya Serikali ya kuimarisha elimu ya juu kwa watoto wa kike jambo
ambalo hapo zamani halikuwa rahisi.
“Wazee walisema
‘Mcheza kwao, hutunzwa’ na ‘Chanda chema, huvikwa pete’. Kauli zote hizo za
wazee wetu zinasibu kwenu. Kwa hivyo, tumeamua kuwaandalia hafla hii kwa ajili
ya kukutunzeni, kwa sababu mmecheza vyema kwa ajili yenu na kwa ajili ya nchi
yenu”,alisema Dk. Shein.
Aidha, alitoa pongezi
kwa skuli za binafsi zilizopo Zanzibar ambazo zimeweza kuwakilisha vizuri kwa
kutoa wanafunzi bora na kuzipongeza skuli zote zilizotoa wanafunzi wengi wa
daraja la kwanza na hasa wale waliopata alama za juu kabisa.
Kadhalika Rais Dk.
Shein alizipongeza skuli ambazo zimetoa wanafunzi japo si kwa idadi kubwa
lakini na wao wameweza kupata wanafunzi waliofaulu kwa daraja la kwanza na hata
la pili. “Nafahamu matokeo haya hayaji kwa
sadfa lakini yametokana na jitihada na mikakati mahsusi ya kufanya
vizuri”,alisisiatiza Dk. Shein.
Kwa mnasaba huo Rais
Dk. Shein aliwapongeza walimu, Kamati za Skuli na Wazazi kwa kuandaa mikakati
bora ambayo imewezesha vijana kupata matokeo mazuri katika mitihani yao ya
Taifa.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na
walimu wa skuli zote zilizowaandaa wanafunzi wao kwa ajili ya mitihani yao.
Pia, Rais Dk. Shein
alitoa wito kwa walimu kuendelea kuutekeleza kwa moyo thabit, uzalendo na
huruma, wajibu wao huo na kutambua kuwa Serikali na wananchi wote kwa jumla
wanathamini jitihada zao hizo.
Kadhalika aliwataka
walimu wasiozingatia vyema majukumu yao na kuyakiuka maadili ya
ualimu wajirekebishe kwani kazi hiyo ni ya watu wenye heshima kubwa katika jamii.
Alieleza kuwa
nidhahiri kwamba matokeo hayo yametokana na jitihada za pamoja na ushirikiano
ambao siku zote huwa na matokeo mazuri na kutoa wito wa kuendeleza mikakati na
kushirikiana ili mafanikio hayo yawe endelevu na isije ikaonekana ni matokeo ya
bahati mbaya ama ‘nguvu za soda’.
Kwa kuzingatia umuhimu
wa elimu kwa Taifa lolote, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar tangu Awamu ya Kwanza ya Uongozi imekuwa ikichukua jitihada mbali
mbali katika kuimarisha sekta hiyo muhimu kwa maendeleo.
Alisema kuwa jitihada
hizo zinahusisha uimarishaji wa elimu ya ngazi mbali mbali ikiwemo elimu ya
Sekondari kama Mwasisi wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume
alivyosisitiza na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya elimu hiyo ya Sekondari kwa wingi zaidi jambo ambalo
halikuwepo wakati wa ukoloni.
Alieleza kuwa azma
hiyo imeendelezwa katika Awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi
hivi sasa, katika Awamu hii ya Saba ya Uongozi wake.
Alisema kuwa Ilani ya
Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010-2015 ilipoanza Awamu ya Saba ya Uongozi
ilielekeza Serikali baada ya kuundwa, kuimarisha elimu ngazi zote ikiwemo elimu
ya Sekondari kwa kufanya mambo kadhaa yakiwemo kuongeza idadi ya skuli za Sekondari Unguja na Pemba jambo ambalo limefanywa kwa
mafanikio makubwa.
Rais Dk. Shein mbali
ya kuwaandalia chakula hicho cha mchana wanafunzi hao pia, aliwapa zawadi
maalum wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kutoka Skuli zote za Zanzibar zikiwemo
za Serikali na Binafsi.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki
Pembe Juma alieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta ya elimu na kutumia
fursa hiyo kutoa pongezi za pekee kwa rais Dk. Shein kwa juhudi zake za
makusudi za kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.
Waziri Pembe alieleza kuwa Rais Dk. Shein
anaendeleza nyayo za waasisi wa Taifa hili Marehemu Mzee Abeid Karume pamoja na
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kuimarisha sekta ya
elimu na kukuza sekta zote za maendeleo kwa watu wote.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Idrisa
Muslim Hijja alieleza kuwa mafanikio yote yaliopatikana katika sekta ya elimu
ni juhudi za Rais Dk. Shein katika kuhakikisha anaweka mazingira bora katika
sekta hiyo huku akitumia fursa hiyo kuwataja wanafunzi wote waliofanya vizuri.
Akitoa neno la shukurani Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Issa Haji Ussi Gavu alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kuendelza
utamaduni wake huo na kueleza kuwa fursa ya kupata elimu hivi sasa ni ya watu
wote wa mjini na vijijini.
Huo ni utamaduni alioweka Rais Dk. Shein wa kila
mwaka wa kuwaalika Ikulu wanafunzi wanaopata matokeo ya daraja la Kwanza katika
mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nnne na cha Sita kwa malengo maalum ambapo pia,
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na viongozi wengineo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment