Rais Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, mjini Zanzibar wakati
alipofungua mkutano wa 10 wa Jumuiya ya Wapatholojia wa Tanzania (APT), ambalo
mwaka huu linafanyika hapa Zanzibar.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kwamba
tayari Serikali imewapeleka masomoni madaktari saba kujifunza maeneo mbali
mbali ya fani hiyo ambapo wanne wapo nchini Misri, mmoja yupo nchini India,
mmoja nchini Cuba na wengine wawili wapo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili nchini Tanzania.
Aliongeza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa na
Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha angalau Wapatholojia 15 wanarudi ama
wanaendelea na masomo pale atakapomaliza muda wake wa uongozi.
Rais Dk. Shein ambaye pia, ni mlezi wa
Wanapatholojia Tanzania alisema kuwa huduma za uchunguzi wa maradhi mbali mbali
zimeimarika katika hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo wananchi hivi sasa wanaweza
kupatiwa huduma zote muhimu za uchunguzi wa maradhi katika maabara ya
Patholojia bila malipo.
Katika jitihada za kupiga vita maradhi ya
kuambukiza na yale yasio ya kuambukiza, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa
ikiongeza bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa dawa na nyenzo za
utibabu.
Alisema kuwa kima cha fedha kilichotengewa sekta
ya afya kimepanda kutoka TZS bilioni 7 mwaka 2017/2018 hadi kufikia bilioni
12.7 mwaka 2018/2019 na kwa mwaka huu wa 2019/2020 kiwango hicho kimefikia TZS
15.7 ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 124.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ilizindua mradi wa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi katika mwezi wa
Disemba 2018 ambapo mradi huo ni wa miaka mine ambapo unaendeshwa kwa mashirikiano
baina ya Jamhuri ya Watu wa China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema kuwa huduma za kisasa za
kutumia mionzi katika kuchunguza maradhi mwilini zinapatikana wakati wote
kwenye hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo tangu zilizofungwa mashine za CT Scan
mwaka 2009 pamoja na mashine ya MRI na
mashine 3 za X-ray zinazotumia mfumo wa dijitali zilizofungwa mwaka
2019.
Alieleza kuwa huduma hizo zinazopatikana katika
hospitali ya Mnazi Mmoja na hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani Pemba zinatolewa
bure.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza haja ya kufanya
kazi kwa pamoja kati ya Wizara ya Afya ya Zanzibar na Hospitali ya Muhimbili
hasa katika maradhi ya uchunguzi na kueleza umhimu wa kushughulikia masuala ya
uchunguzi wa maradhi ili kuwatibu wananchi hapa hapa nchini.
Kwa upande wa ugonjwa wa Ebola Rais Dk. Shein
alisema kuwa Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ziafanya jitihada kubwa kuzuia ugonjwa huo usiingie
nchini.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa
madaktari bingwa wastaafu wakiwemo wa patholoji wasiharakishwe kustaafu na
badala yake waandaliwe mazingira mazuri ili waendelee kutoa huduma kwa jamii.
Aidha, alieleza umuhimu wa kuwaandaa vijana kusoma
masomo ya patholojia ili waje kuziba pengo la wataalamu ambao watastaafu kabisa
kutoa huduma hizo.
Sambamba na hayo, alieleza kuwa kwa upande wa
Zanzibar, jitihada za kukuza maendeleo ya janmii katika sekta ya afya
zinakwenda sambamba na matakwa ya Kanuni za afya za Kimataifa pamoja na Ajenda
ya Usalama wa Afya Ulimwenguni.
Rais Dk. Shein aliwapongeza Wapatholojia hao kwa
uwamuzi wao wa kuja kufanya mkutano wao hapa Zanzibar na kuahidi kushirikiana
nao huku akitumia fursa hiyo kuwakaribisha kuitembelea Zanzibar wakati wowote.
Nae Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed
alimpongeza Dk. Shein ambaye ni mmoja miongoni mwa waanzilishi wa Jumuiya hiyo
katika mwaka 1991 na muwasisi wa Wapatholojia
na kumuelezea kuwa ana ubinaadamu wa hali ya juu.
Alisema kuwa tokea Dk. Shein aingie madarakani
hali ya Amani na utulivu imeendelea kuwepo hapa nchini hali ambayo imeweza
kwuavutia watu mbali mbali wakiwemo Wanapatholojia hao ambao wameamua kuja
kufanya mkutano wao hapa Zanzibar.
Alimpongeza Dk. Shein kwa kusimamia Sera ya mwaka
1964 chini ya chama cha Afro Shirazi Party (ASP), ya kuhakikisha huduma za afya
zinatolewa bure huku akitumia fursa hiyo kueleza jinsi uchumi wa Zanzibar
unavyoimarika.
Mapema, Mwenyekiti wa Wapatholojia Tanzania Dk.
Charles Massambura akitoa usalamu zake alitoa pongezi wka Rais Dk. Shein kwa
kuimarisha sekta ya afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maabara ya
Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja inapandishwa hadhi katika masuala mazima ya
uchunguzi.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dk. Elisha
Osati alitoa pongezi kwa Serikali zote mbili kwa kuendeleza sekta ya afya na
kusisitiza haja ya kuwaendeleza madaktari na kuwaenzi huku akiwataka madaktari
kukumbushana katika kutelekeza majukumu yao ya kazi.
Profesa Eligius Lyamuya akiwasilisha mada kuu katika
hafla hiyo alieleza umuhimu wa wapathojia katika kutambua maradhi kadhaa kwa
binaadamu, wanyama na mimea pamoja na uchunguzi wa visababishi vya magonjwa
mbali mbali.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment