RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein amesisitiza dhamira ya Serikali katika kulipa kipaumbele suala la
kufanya utafiti, kuwa inalenga kuzitafutia majibu na ufumbuzi changamoto mbali
mbali zinazojitokeza katika Wizara za Serikali.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini Zanzibar, wakati akipokea
taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamo wa
Pili wa Rais kwa mwaka 2018/2019.
Alisema ni muhimu kwa Idara na taasisi zote za serikali
kufanya utafiti, badala ya jukumu hilo kuiachia Idara ya Mipango, Sera na
Utafiti pekee.
Alisema katika kufanikisha jambo hilo, Idara zinaweza kuwatumia
wataalamu wake na pale wanapokosekana, ni vyema ikatowa mafunzo kwa wafanyakazi
wenye elimu ya kutosha, ili hatimae waweze kutumika kwa kazi hiyo, na kubainisha
kuwa baadhi ya tafiti hazihitaji fedha nyingi.
Aliwataka viongozi wa Idara za Serikali kujenga mapenzi ya
kufanya tafiti, sambamba na kujenga uwezo wa kitaaluma ili waweze kutekeleza shughuli
hizo kwa ufanisi.
Aidha, aliitaka Wizara kupitia Idara ya Sherehe na Maadhimisho
ya kitaifa kuwasilisha waraka Serikalini, ili kupata muafaka baada ya kubainika
kuwepo kwa baadhi ya Wizara zilizonunua
vifaa mbali mbali vya sherehe, ikiwemo mashamiana kwa lengo la kuvikodisha , jambo ambalo
kimsingi linapaswa kufanywa na Idara hiyo.
Akigusia mchakato wa serikali kuihamishia mjini Dodoma Idara
ya Uratibu wa shughuli za Serikali iliopo Dar es Salaam, Dk. Shein alisema eneo
la ardhi la ekari 30 ililopatiwa serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania ni kubwa, hivyo akasisitiza azma ya Serikali ya kuihamishia
Ofisi hiyo Dodoma, mara baada ya hatua ya ujenzi kukamilika.
Alisema eneo hilo linapaswa kutumika vizuri kwa kuwepo mipango mizuri ya ujenzi , kuambatana
na maelekezo ya Mainjinia, pamoja na kutoa indhari ya kuhakikisha ardhi hiyo
inabaki salama.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali kupitia vyombo vyake
vya Ulinzi na Usalama imejipanga vyema na vimekuwa vikifanya juhudi kubwa kukabiliana na uingizaji wa dawa za
kulevya,hivyo akabainisha umuhimu wa kuzifanyia kazi taarifa za uhalifu katika maeneo
yote, ikiwemo baharini.
Katika hatua nyengine, Dk Shein aliwakumbusha watendaji wa
Ofisi hiyo, kuwa Ofisi ya Makamo wa Pili
wa Rais kama ilivyo Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
zinahitaji wafanyakazi wanaoheshimika na
kufanya kazi zao kwa misingi nidhamu, weledi na uwajibikaji.
Alisisistiza haja ya watendaji hao kuondokana na hali ya
kufanyakazi kwa mazoweya, ili kuweza kupata ufanisi katika malengo
wanayojiwekea.
Aidha, alisema utaratibu wa Bango kitita ni wa kilimwengu,
akibainisha uzuri wake, kwa misingi kuwa unawawezesha wafanyakazi kujitathmin
kutokana na utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema miongoni mwa mambo yanayoleta ufanisi katika kazi ni
pamoaj na kuwepo kwa maeneo na ofisi
nzuri za kufanyia kazi, jambo ambalo Serikali imekuwa ikiendelea na juhudi za
kuimarisha.
Dk. Shein aliwapongeza watendaji wa Ofisi hiyo kwa juhudi
kubwa wanayofanya katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja kazi nzuri waliyofanya katika uwasilishaji wa
mpango kazi kwa mwaka 2018/2019.
Nae, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd,
aliwataka watendaji wa Ofisi hiyo kujifunza na kutekeleza kwa ufanisi yale yote
walioelekezwa, kuambatana na shabaha na malengo waliyojipangia.
Aliwataka watendaji hao kuendelea na mshikamano wao na kufanya
kazi kwa pamoja, akibainisha kuwa ndio siri ya mafanikio waliyoyapata, mbali na
baadhi nyakati kukabiliana na matatizo mbali mbali.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Waziri wa
Wizara hiyo Mohamed Aboud, alisema Ofisi
hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipijndi hicho, ikiwemo kuratibu ujenzi
wa nyumba ya makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais unaoendelea kufanyika katika eneo
la Pagali, kisiwani Pemba,
Alisema ujenzi huo unafanyika chini ya kikosi cha KMKM ambapo
hadi kufikia sasa tayari umefikia asilimia 75 ya kazi.
Alisema Ofisi imefanikiwa kuratibu na kuendesha Uchaguzi mdogo
wa Jimbo la Jang’ombe, sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa wapiga kura kwa
makundi mbali mbali ya kijamii, ikiwemo walimu na wanafunzi wa sekondari na vyuo
vya elimu ya juu vilivyopo Zanzibar.
Aidha, alisema Tume ya Uchaguzi imefanikiwa kubadilisha mfumo
wa Uandikishaji na kutengenza mfumo mpya kwa kutumia wataalamu wa ndani.
Alieleza kuwa ndani ya kipindi hicho, Wizara ilibeba dhima ya
kuwaelimisha wafanyakazi, wanafunzi wa skuli za msingi na sekondari pamoja
na wananchi katika shehiya mbali mbali
Unguja na Pemba juu ya athari ya matumizi ya dawa za kulevya.
Sambamba hilo, alisema Ofisi ilifanikiwa kuteketeza dawa za
kulevya zilizokuwa maeneo ya uhifadhi wa kisheria, jambo ambalo kwa mara ya
mwisho lilifanyika mnamo mwaka 2009.
Waziri Aboud, alieleza kuwa Ofisi ya Baraza la
Wawakilishi imeendelea na shughuli zake
za kuratibu mikutano ya Baraza pamoja na kazi za Kamati za kudumu kwa ufanisi
mkubwa.
“Jumla ya mikutano minne ilifanyika, ambapo kutokana na mikutano hiyo jumla ya miswada mitano ya
sheria ilijadiliwa na kupitishwa na Baraza”, alisema.
Alisema kazi za kamati za kudumu zilifanyika kupitia Wizara
zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na mashirika yake.
Aidha, alisema Ofisi ilifanikiwa kuendeleza ujenzi wa Kituo
cha Tiba na marekebisho ya tabia katika hatua ya tatu pamoja na kutoa mafunzo katika masuala ya UKIMWI, afya ya
uzazi na uzingatiaji wa masuala ya UKIMWI kwa watendaji wa vyuo vya Mafunzo na
Asasi za kiraia.
Katika hatua nyengine, Waziri Aboud alisema Ofisi ilichukuwa
hatua ya kulihami eneo la fukwe huko Msuka ili lisiendelee kumong’onyoka
kutokana na maji ya bahari, kwa kuandaa utaratibu wa kujenga ukuta maalum
utakaogharamiwa na Serikali ikiwa ni hatua ya muda.
Aidha, Ofisi iliwapatia mafunzo ya kazi na utaratibu wa maisha
wafanyakazi wa Ofisi, ikiwemo mafunzo ya sheria na kanuni za Utumishi wa Umma,
masuala ya Ukimwi na Homa ya Ini, rushwa na uhujumu uchumi, udhibiti na
utunzaji wa kumbu kumbu na siri za
serikali, pamoja na mkataba wa Huduma za umma.
Waziri Aboud, alibainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo pia
kulijitokeza changamoto mbali mbali, ikiwemo upungufu wa gari katika baadhi ya
Idara, ufinyu wa nafasi katika mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Idara ya
Mazingira pamoja na Tume ya Uchaguzi za Wilaya.
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa
Rais, Shaaban Seif Mohamed, alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuanzisha utaratibu
wa kuwasilisha Mpango kazi na kusema una
faida kubwa katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Wizara za serikali.
Abdi
Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment