Habari za Punde

SMZ Yatiliana Saini na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi Ukarabati na Ujenzi wa Hospitali ya Wete Pemba.


Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa akisaini hati ya makubaliano ya Ujenzji na Ukarabati wa Hospitali ya Wete Pemba na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi. Sheikh Mohammed Saif Ali Suwaid, hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Mfuko huo Abu Dhabi leo. 
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano (MOU) juu ya ujenzi na matengenezo ya Hospitali ya Wete Pemba.

Makubaliano hayo yataipelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata Dola za Kimarekani Milioni 10 sawa na Shilingi za Kitanzani Bilioni 23 kupitia Mfuko huo ambazo zitasaidia katika ujenzi na matengenezo ya Hospitali hiyo ikiwewa ni pamoja na upanuzi wake.

Hafla hiyo ya utiliaji saini imefanyika katika ofisi ya Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi mjini Abudhabi ambapo kwa upande wa Zanzibar Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisaini kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkurugenzi  Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi Mohammed Saif Al Suwaid alisaini kwa niaba ya Serikali ya (UAE).

Mara baada ya utiliaji saini wa Mkataba huo Waziri Abdiwawa alieleza kuwa, fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta ya afya Zanzibar.

Alieleza kuwa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake wote wanatoa pongezi na shukurani za dhati kwa Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) kwa juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.

Balozi Ramia aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana juhudi hizo ambazo zimekuwa chachu katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Aidha, Balozi Ramia alitumia fursa hiyo kutoa shukurani za pekee kwa Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan Rais wa Nchi za Umoja huo kwa msaada wake huo na kueleza kuwa hatua hiyo inatoa taswira nzuri ya mashirikiano yaliopo kati ya viongozi wa umoja huo na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wao.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi, Mohammed Saif Al Suwaid alieleza kuwa Mfuko huo unajivunia kupata fursa hiyo na kusisitiza kuwa Serikali ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu utaendelea kuinga mkono Zanzibar.

Alieleza kuwa mradi wa ujenzi na matengenezo ya Hospitali ya Wete ni mradi mkubwa kwani unawagusa moja kwa moja wananchi hivyo, aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein kwa kuweka kipaumbele hicho hasa ikizingatiwa kuwa mradi huo ni muhimu katika maisha ya wananchi.

Sambamba na hayo, Al Suwaid alieleza kuwa  Mfuko wa Maendeleo wa  Abudhabi utachukua juhudi na ari za makusudi katika kahakikisha mradi huo unafanikiwa na unatekelezwa kwa muda uliopangwa.

Fedha hizo zilizotolewa na Serikali ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi zinatokana na agizo maalum la Rais wa Umoja wa nchi hizo Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan katika kuhakikisha Serikali anayoiongoza inaiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.

Katika hafla hiyo baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  walishuhudia tukio hilo akiwemo Waziri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said Hassan Said pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mbarouk Omar Mbarouk.

Hatua hiyo ni matunda ya ziara ya Rais Dk. Shein aliyoifanya katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mnamo mwezi Januari mwaka 2018 kufuatia mwaliko wa Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Katika kuhakikisha mazungumzo ya viongozi hao na makubaliano yao yanafanyiwa kazi mnamo mwezi wa Agosti mwaka 2018, Ujumbe wa timu ya Wataalamu kutoka Serikali ya Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulikuja Zanzibar na kufanya ziara ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Zanzibar ukiongozwa na Mshauri wa Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Nchi za Falme za Kiarabu Bi Najla Al Kaabi.

Ujumbe huo ulifanya ziara ya siku moja katika Kisiwa cha Pemba na kutembelea barabara ya Chake Chake hadi Mkoani, Hospitali ya Abdalla Mzee, Bandari ya Mkoani, Hospitali ya Wete, Bandari ya Wete, pamoja na kutembelea kikundi cha Wajasiriamali cha Upendo cha mjini Wete.
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.