Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano 50 wa Chama Cha Mabunge cha Jumuiya ya Madola (CPA) uliofanyika leo katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahr Mbweni Wilaya ya Magharibi B Unguja.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kwamba teknolojia ya habari na mawasiliano ina nafasi
kubwa ya kuleta mabadiliko ya maendeleo katika Mabunge ya nchi za Jumuiya ya
Madola.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Mkutano wa 50 wa Chama Cha Mabunge cha
Jumuiya ya Madola (CPA) Kanda ya Afrika unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli
ya Madinatul Bahr, iliyopo Mbweni nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema
kwamba iwapo teknolojia ya habari na mawasiliano itatumika ipasavyo hasa katika
kuimarisha kanzi data mbali mbali hatua hiyo itarahisisha suala zima la kufanya
maamuzi kwa wakati na kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.
Aliongeza kuwa
uendeshaji wa Bunge kwa kutumia njia za kisasa kunawaweka karibu zaidi Wabunge
na wananchi, jambo ambalo linatoa fursa
pana zaidi kwa wananchi ya ya kutoa maoni yao na hoja mbali mbali za maendeleo
zinazogusa maisha yao ya kila siku.
Alieleza kuwa Bunge
Mtandao ni nyenzo nzima ya kupunguza harama za mambo mbali mbali kama vile
usafiri sambamba na kuokoa muda.
Hata hivyo, Rais Dk.
Shein alisema kwamba juhudi zinazochukuliwa na nchi wananchama wa Jumuiya hiyo
za kuimarisha Bunge Mtandao lazima ziende sambamba na juhudi za uhamasishaji wa
teknolojia ya habari katika skuli zilizo katika Majimbo yao na nchi nzima kwa
jumla.
Akieleza Kaulimbiu ya
Mkutano huo mwaka huu, inayosema “Bunge Mtandao
ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ustawi wa demokrasia “ Rais Dk. Shein
alisifu kauli mbiu hiyo inayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na
masuala mbali mbali ya utandawazi.
“Nafahamu kwamba
matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ikiwemo mitandano ni muhimu sana katika
utekelezaji wa majumuku ya Wabunge duniani likiwemo suala la utungaji wa
sheria, kuwasilisha hoja za wananchi pamoja na kusimamia utekelezaji wa
shughuli za Serikali”alisema Dk. Shein.
Rais Dk. Shin alitumia
fursa hiyo kupongeza juhudi zinazochukuliwa na Wabunge pamoja na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi za kushirikiana na uongozi wa skuli mbali mbali
zilizozomo katika Majimbo yao katika suala zima la kuhamasisha utoaji wa elimu
ya habari na mawasiliano.
Akielezea kwa upande
wa Zanzibar, alisema kuwa hivi sasa tayari skuli mbali mbali zimefaidika na
matumizi ya kompyuta za aina zote ambazo hutolewa na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kwa ajili ya skuli zilizopo katika Majimbo yao.
Alieleza imani yake
kwamba juhudi kama hizo tayari zinafanywa wa Wabunge wa nchi nyengine wa
Jumuiya ya Madola hivyo, alisisitiza haja ya kupewa kipaumbele ili zipate
kuendelezwa na Wabunge wote wa nchi za Jumuiya hiyo.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kueleza juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha Demokrasia na Utawala Bora
pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kaunzisha Serikali Mtandao.
Alisema kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza mradi mkubwa wa Serikali Mtandao ambao
aliuzindua rasmi Januari mwaka 2013.
Aliongeza kuwa kuwepo
kwa Serikali Mtandao kumesaidia sana katika kuimarisha Demokrasia na Utawala
Bora kwa kuimarisha uwazi, ufanisi na uwajibikaji kama ilivyoelekezwa katika
Sheria na Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011.
Alisema kuwa juhudi
zinazoendelezwa na Serikali za kuimarisha teknolojia ya habari na
mawasiliano hapa nchini zimekuwa na
mchango mkubwa katika kuimarisha utekelezaji mipango ya maendeleo ya nchi hasa
MKUZA III na Dira ya Maendeleo ya
Zanzibar 2020.
Aidha, Rais Dk. Shein
alifahamisha kwamba Serikali imekuwa ikitekeleza awamu ya II ya Serikali
Mtandao ambapo jumla ya waya zenye urefu wa kilomita 419 zimelazwa katika
maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ambapo jumla ya Taasisi 112
zimeshaunganishwa na Mtandao huo likiwemo Baraza La Wawakilishi.
Alifahamisha kwamba
kwa ujumla Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti katika kuhamasisha
matumizi ya teknolojia ya Habari ambapo Baraza la Wawakilishi ni miongoni mwa
Ofisi zilizo mstari wa mbele katika kuhamasisha suala hilo.
Vile vile, Rais Dk.
Shein alibainisha kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepata
mafanikio makubwa sana katika utoaji wa huduma na ukusanyaji mapato kwa
kuanzisha mifumo mbali mbali yenye kurahisisha utoaji wa huduma na ulipaji wa
kodi.
Kutokana na faida
zinazopatikana kutokana na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano Rais
Dk. Shein aliwasisitiza Wabunge wa Jumuiya ya Madola kutilia mkazo kwa vijana
juu ya matumizi ya teknolojia ya habari kwa kutumia njia sahihi.
Alisema hivi sasa
teknolojia ya habari ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanaadamu kwa kuwa imegusa
na kuathiri kila nyanja ya maisha ya mwanaadamu kama vile elimu, afya, biashara
pamoja na suala zima la usalama.
Rais Dk. Shein
aliupongeza uongozi wa Jumuiya hiyo kwa ubunifu walio nao katika suala zima la
kuhamasisha uwekezaji sambamba na kuzichangamkia fursa mbali mbali za kiuchumi
zilizo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Rais Dk. Shein
aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa uwamuzi wao wa kuja kufanya mkutano huo
mkuu wa 50 hapa Zanzibar na kuwapongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Job Yusnino Ndugai na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali
Maulid kwa matayarisho mazuri na kufanikisha
mkutano huo.
Dk. Shein alipongeza
mfumo wa Jumuiya ya Madola na Taasisi zake kwa kufanya shughuli zake kwa
mzunguko jambo ambalo linaimarisha umoja na mshikamano katika nchi za Jumuiya
hiyo pamoja na wananchi wake.
Alieleza kuwa hatua
hiyo inatoa fursa kwa wananchi wa nchi za Jumuiya ya Madola kuifanahamu vyema
Jumuiya hiyo sambamba na Taasisi zake.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa tayari Tanzania
imeshawahi kufanyika mkutano wa Majaji mnamo Septemba 2017 ambapo wajumbe wake
walipata fursa maalum ya kuitembelea Zanzibar na kuweza kuangalia fursa kadhaa
zilizopo.
Alieleza kuwa Zanzibar
imekuwa mshiriki mkubwa wa mikutano ya Jumuiya ya Madola ambapo katika mkutano
kama huo wa 49 ambao ulifanyika mjini Gaborone nchini Botswana ilituma ujumbe mkubwa
kutoka Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambao ulioshiriki kikamilifu katika
mkutano huo.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kuwaalika washiriki wa mkutano huo kama ni wanachama wa Jumuiya hiyo
na wawakilishi wa nchi zao waje kuekeza Zanzibar katika sekta zote za kiuchumi na kijamii kwani
Zanzibar ni nchi yenye amani na utulivu mkubwa na imekuwa kivutio muhimu kwa
wawekezaji wanaotoka nchi mbali mbali duniani.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa ikiwa huo ni mkutano
wa 50 ni matarajio yake kwamba huu ni wakati muwafaka wa kutathmini mafanio
yaliopatikana pamoja na changamoto zilizopo.
Alisema kwamba
anaamini maazimio yatakayopitishwa yatakuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha
demokrasia na Utawala Bora pamoja na
kuyafikia malengo ya Jumuiya hiyo.
Nae Nae Mwenyekiti wa
Jumuiya hiyo ambae pia ni Spika wa Bunge la Kenya Justin Muturi alisifu juhudi
zilizochukuliwa na spika wa Bunge kwa kushirkiana na Spika wa Baraza la
Wawakilishi kwa kufanikisha mkutano huo hapa Zanzibar na kutumiafursa hiyo
kueleza dhamira ya Jumuiyahiyo ya kujenga hoteli ya kisasa ya nyota tano huko
Dodoma, na kupongeza mashirikiano mazuri wanayoyapata kutoka Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nae Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai pamoja na Spika wa Baraza la
Wawakilishi Zubeir Ali Maulid waliwakaribisha wajumbe hao wa mkutano huo na
kuwaeleza fursa mbali mbali zilizopo Zanzibar zikiwemo za uwekezaji na hata za
utalii kwani Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio vingi.
Nao baadhi ya Maspika wa Mabunge ya nchi za Jumuiya hiyo walitoa salamu zao na
kusifu juhudi za mashirikiano zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo huku mwakilishi maalum
kutoka Bunge la Pakistan alitoa salamu za Spika wa nchi hiyo Asad Qaiser na
kueleza umuhimu wa Bunge Mtandao na nafasi ya mwanamke katika maendeleo.
Mkutano huo ni wa wiki
moja ambao ulianza Agosti 30 kwa kamati mbalimbali unatarajiwa kumaliza
Septemba 5 mwaka huu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment