Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikabidhiwa Tuzo ya Sinema Zetu na Waziri wa Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Zanzibar Mhe. Balozi Ali Karume hafla hiyo imefanyika Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wasanii kuitumia
kikamilifu studio ya Muziki na Filamu iliopo Rahaleo, ili waweze kupata
mafanikio ya kiuchumi pamoja na kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Dk. Shein ametowa wito huo Ikulu Mjini hapa, katika hafla ya
kupokea tuzo, Cheti na CD kutoka kwa wasanii wa filamu nchini, zilizotokana na
ushindi walioupata katika mashindano yalioandaliwa na Kituo cha Azam TV.
Katika mashindano hayo yaliofanyika mwezi April, 2018 , filamu
200 kutoka nchi sita zilishindaniwa na wasanii wa Zanzibar waliibuka washindi
kupitia filamu za ‘Bint Zanzibar’, ‘Sisi na wao’ pamoja na ‘Dema’.
Dk. Shein alisema Studio
ya Muziki na filamu iliipo Rahaleo, ni miongoni mwa studio bora na yenye vifaa
vya kisasa, hivyo amewataka wasanii kuitumia kikamilifu, ili waweze kunufaika
kutokana na Hati miliki ya kazi zao pale watakapoziuza.
Alisema safari ya wasanii hao bado ni ndefu, hivyo akawataka
kuongeza bidii ili kupata mafanikio, sambamba na kuitangaza Zanzibar kimataifa,
akibainisha baadhi ya Mataifa ikiwemo Marekani, India na Nigeria ambapo wasanii
wake wamepata mafanikio makubwa kutokana na sanaa ya uigizaji.
Aidha, aliwataka kuongeza kasi katika kuendeleza sanaa, kwa kigezo
kuwa jamii inahitaji kuliwazwa baada ya shughuli mbambali za kazi.
Dk. Shein, aliwapongeza wasanii hao kwa kazi kubwa waliyofanya
na kuiletea sifa Zanzibar.
“Mmefanya kazi kubwa , ni kazi ya thamani………mimi nimeonyesha
njia……………..”, alisema.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kuwapongeza wasanii waliojitokeza kuomba matengenezo ya Studio hiyo.
Alisema Serikali imetumia fedha nyingi kwa ajili ya
matengenezo ya studio hiyo na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono wasanii pale
mahitaji zaidi yatakapojitokeza katika studio hiyo.
Akigusia historia ya filamu Zanzibar, Dk. Shein alisema
Zanzibar inajivunia kwa kuwa na magwiji wa sanaa mbali mbali, ikiwemo wa filamu
pamoja na kupata bahati ya wasanii mahiri duniani kuja nchini kwa ajili ya
kurekodi michezo yao.
Alisema baada ya Mapinduzi ya 1964, filamu ya mwanzo
iliyojuilikana Zanzibar yasonga mbele” ilirikodiwa na baadae kusambazwa katika
Mikoa yote mjini na mashamba.
Nae, Waziri wa
Vijana,Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume, alimshukuru Rais
Dk. Shein kwa juhudi zake za kuendeleza sanaa nchini na kuunga mkono
mahitaji ya wasanii, ambapo alifanikisha ujenzi wa Studio ya kisasa ya
Muziki na Filamu.
Aidha, aliwapongeza wasanii kwa kazi nzuri ya uigizaji
akibainisha heshima kubwa wanayopata wasanii mbali mbali duniani kutokana na kazi
za sanaa, hivyo akawataka kuiga mfano wao.
Mapema, Katibu wa Chama
cha wasanii waigizaji, Salum Maulid ‘stika’ alisema wasanii wanahitaji kupatiwa
mafunzo zaidi ya uigizaji ili kuongeza uwezo wao kiutendaji.
Alisema katika utendaji wao wakazi wamekuwa wakipata
mashirikiano mazuri na viongoi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa an Michezo
pamoja na COSOZA.
Aliiomba Serikali kuendelea kuwaunga mkono wasanii na kusema
hatua hiyo itafanikisha azma ya kuutangaza Utalii kupitia sanaa.
Aidha, alisema Chama cha wasanii Zanzibar, kimejidhatiti
kuwaelekeza wasanii juu ya umuhimu wa kufanya kazi zao kwa msingi wakulinda
mila, silka na utamaduni wa Wazanzibari.
Abdi
Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment