Mkaazi wa Mtaa wa Mombasa Wilaya ya Magharibi “B” Bw. Hassan Hamad akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif maafa yaliyoikumba Familia yake baada ya Nyumba yao kuwaka Moto Jumatato iliyopita.
Balozi Seif akiitahadharisha Jamii kufuatilia nyendo za Watoto wao hasa wanapokuwa ndani ili kuwepuka maafa pale alipofika Mtaa wa Mombasa kuifariji na kuipa pole Familia ya Bwana Hassana Hamad baada ya Nyumba yao Kuwaka Moto.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametahadharisha Wazazi Nchini kufuatilia nyendo za Watoto wao kila wakati ili kuepusha mapema cheche za maafa zinazoweza kutokea hasa Watoto hao wanapokuwa ndani ya Nyumba pekee yao.
Alisema matukio mengi ya kusikitisha na hatimae kuleta maafa makubwa huzikumba baadhi ya Familia baada ya Watoto wao kuwa na Uhuru wa kutosha wa kufanya mambo ambayo wakati mwengine huleta hatari.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo alipofanya ziara ya kuipa Pole Familia ya Bwana Hassan Hamad wa Mtaa wa Mombasa Wilaya ya Magharibi “B” baada ya Nyumba waliokuwa wakiishi kuungua Moto Jumatano iliyopita na kuteketeza kila kilichomo ndani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiifariji Familia hiyo iliyopoteza pia Uhai wa Mtoto wao anayekadiriwa kuwa na Umri wa Miaka Minne katika ajali hiyo aliwashukuru Viongozi na Wananchi na Majirani walisaidia kupunguza maafa zaidi katika eneo hilo.
Alisema Serikali imepokea taarifa za awali za tukio hilo na kusubiri Ripoti rasmi ya tukio lenyewe kutoka kwa Maafisa na Watendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana Maafa Zanzibar ambayo iko chini ya Ofisi yake ili kuangalia hatua madhubuti za kutafuta mbinu za kujaribu kunusuru matukio kama hayo.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Kepteni Silima Haji Haji alimueleza Balozi Seif kwamba Wapo Viongozi wa Taasisi za Umma na hata binafsi walioguswa na tukio hilo na kuamua kusaidia nguvu katika mdhana ya kuipa faraja Familia hiyo ya Bwana Hassan Hamad.
Kepteni Silima alizitaja Taasisi hizo kuwa ni pamoja na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi “B”, Jumiya ya Misikiti Mitatu pamoja na baadhi ya Watu Binafsi.
Chanzo cha Moto huo kilichoteketeza kila kitu kilichomo ndani ya Nyumba hiyo bado hakijaenelewa rasmi ingawa kuna dhana kwamba huenda ikawa chembe ya Kibiriti kilichokuwa kikichezewa na Watoto waliokuwemo ndani.
No comments:
Post a Comment