Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Wazee wa CCM wa Wilaya ya Wete Pemba Ukumbi wa Jamuhuri leo.12-10-2019.


Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wazee wa CCM Wilaya ya Wete Pemba katika ukumbi wa Jamuhuri Wete akiwa katika ziara yake Kisiwani Pemba.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndio waasisi wakubwa wa kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi ya Januari 12, 1964 hivyo ni vyema wakaenziwa.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika Ukumbi wa Jamhuri Wete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wa Wilaya ya Wete.
Alisema kuwa juhudi hizo zote za kuendelea kuwatunza na kuwaenzi wazee  zinatokana na mikakati sambamba na kauli ya Marehemu Mzee Abeid Karume chini ya Manifesto ya ASP ya kuhakikishwa wazee wanatunzwa na wanaenziwa vizuri.
Alieleza haja kwa vijana kuwahudumikia na kuwatunza wazee kwani wana historia kubwa katika kuipigania nchi yao na jasho lao katika kupigania uhuru wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein aliwataka vijana kuwatumia wazee kwani wanamchango huku akisisitiza kuitumia nguvu kubwa iliyiopo ya umoja na mshikamano wao kwa kushirikiana na wazee ili kuendelea kupata mafanikio zaidi.
Aliwapogeza wazee wa Wilaya ya Wete kwa risala yao ambayo ina mambo ya msingi mengi yakiwemo pongezi kwa Serikali kwa kutekeleza vyema Ilani ya CCM kwa vitendo sambamba na kueleza changamoto zilizopo ambazo zinamatumaini ya kufanyiwa kazi.
Ameeleza jambo kubwa lililofanywa na Srikali anayoiongoza ikiwa ambalo ni kuhakikisha wananchi wakiwemo wazee wanapata huduma za afya bure vikiwemo vipimo vyote kama vile”X ray” “CT Scan” kipimo kikubwa cha MRI ambacho ni ghali sana kupata huduma zake duniani kote na vyenginevyo.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa Serikali ya Mapindzi ya Zanzibar imekuwa ikiongeza Bajeti ya kunua dawa kwa kila mwaka ambapo mwaka jana ilikuwa TZS Bilinoni 12.7 na mwaka huu zimefikia TSZ Bilioni 15.
Alisisitiza kuwa iwapo wazee wataenda hospitali na kudaiwa pesa kwa ajili ya huduma za afya basi wapeleke taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wao huku akieleza azma ya Serikali ya kuweka elimu bure.
Akielezea kuhusu suala zima la unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto Rais Dk. Shein alisema kuwa hatua za makusudi zinaendelea kuchukuliwa ikiwemo kutolewa hukumu, adhabu sambamba na kuhakikisha tatizo la ucheleweshwaji wa kesi linafanyiwa kazi.
Alieleza kuwa wapo wanafamilia wanamaliza kesi za unyanyasaji wa kijinsia wenyewe kwa wenyewe jambo ambalo ni kosa la jinai.
Pamoja na hayo, Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewapa wananchi wake heka tatu tatu lakini wapo baadhi yao wanazitumia vibaya kwa kuziuza na kuzikata viwanja jambo ambalo ni uvunjifu wa sheria.
Aidha alisema kuwa zaidi ya mashamba 800 yamevamiwa.
Alisisitiza haja kuongeza kasi na mori na ari katika kufanya ziara Matawini kwa azma ya kukiimarisha chama hicho kizidi kuimarika huku akieleza kuwa kuwa nguvu ya CCM iko kwenye Matawi, Wilaya, Mkoa sambamba na Jumuiya za chama hicho na  Mabaraza ya wazee.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alisema kuwa Rais Dk. Shein anafanya hayo kwa kutekeleza mafanikio ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 na kuwa Mabaraza ya Wazee kwa kila ngazi, kuanzia Tawi hadi Ofisi Kuu ambaye Mwenyekiti wake ni Bi Khadija Jabir.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa wanaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutekeleza mambo mengi    huku akisema kuwa wazee wamekuwa na msaada mkubwa katika kuendeleza mema yote yaliyofanywa.
Aliongoza kuwa hikma za kuwaenzi wazee zimeanza kabda ya Mapinduzi chini ya Jemedari Hayati Mzee Abeid Amani Karume na hadi hivi leo hikma na busara hizo zinaendelea kutumika ikiwa ni pamoja na kuwatuza wazee wote wa Unguja na Pemba.
Nao wazee wa Wilaya ya Wete walimpongeza Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuleta maendeleo Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwahudumikia wazee na kuwawekea mazingira bora tena bila ya ubaguzi wa rangi, dini ama chama cha siasa anachotoka.
Sambamba na hayo, wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendeleza huduma zote za kijamii zikiwemo afya, elimu, maji safi na salama, miundombinu ya barabara, pencheni jamii kwa wazee waliotimia umri wa miaka 70, ambao hupewa kiasi cha TZS 20,000 kwa kila mwezi pamoja na huduma nyengine muhimu.
Huduma za kuwatuza wazee hasa katwa huduma za pencheji zimekuwa zikiwanufaisha wazee wa Wilaya hiyo wapatao 3,134 wanapatiwa pencheni jamii sawa na TZS milioni 62.6 kwa mwezi na kwa mwaka ni TZS Milioni 752,160,000.
Waalieleza kuwa na jumla ya wazee 778 wasiojiweza wanapatiwa msaada wa jumla ya TZS Milioni 3.9 kwa mwezi na TZS Milioni 47.2 kwa mwaka.
“Tunakupongeza sana na tunakushukuru wkani katika kuwahudumia wananchi na sisi wazee hukutusahau”, walieleza wazee hao kwenye taarifa yao.
Aidha, jumla ya wazee wanane wanaendelea kutunzwa katika nyumba maalum ya wazee iliyopo Limbani, Wete Pemba kwa pamoja kila mwezi wazee hao kwa kila mmoja hupewa TZS 40,000 ambazo sawa na TZS Milioni 3.8 ambapo fedha zote hizo zinatolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wazee hao pia, waliahidi kuwa wataendelea kumuunga mkono na kuahidi kushirikiana na wenzao kwa kuhakikisha CCM inapata ushindi, huku wakiwesema kuwa Baraza la Wazee limekuwa likifanya kazia kubwa katika kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushika hatamu.
Wazee katika taarifa yao walimpongeza Rais Dk. Shein na kueleza kuwa kitendo cha kwenda kukutana nao ni kielelezo kuwa anawajali na kuthamini juhudi zao ama mchango wao ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Nae Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Mberwa Hamad Mberwa alieleza kuwa wazee wa CCM wa Wilaya hiyo ni wakereketwa na wanakithamini sana chama chao na wamekuwa wakitoa ushauri kwa Chama na Serikali.
Katika neno lao la shukurani wazee hao walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuwaendeleza wazee wa Limbani, pongezi kwa bandari yao ya Wete kwa kuanza shughuli za usafiri na usafirishaji, kuwapelekea boti kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri kwa wagonjwa katika visiwa kikiwemo Fundo, Kojani na vyenginevyo.
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.