Na. Ismail Ngayonga.Maelezo Dar es Salaam. 22.10.2019
MWAKA 1979 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria Na. 4 ya mwaka 1979 kuhusu uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa unaowawezesha mwananchi kushiriki katika kuchagua Kiongozi kupitia uratibu wa Halmashauri za Wilaya.
Moja ya malengo ya uchaguzi huo ni kuwapatia wananchi na viongozi fursa ya kutafakari kujadili kuhusu changamoto za maisha ya watu na namna bora ya kukabiliana nazo pamoja na kuwakumbusha wagombea kuwa kura ni mkataba baina ya mwananchi na mgombea.
Ibara ya nane ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatamka wazi kuwa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, ambapo moja ya misingi hiyo ni uhuru wa maoni, ushiriki na kupiga au kupigiwa kura.
Aidha moja ya haki za kijamii afya, maji, kilimo, hifadhi ya jamii na elimu, hivyo kutokana na misngi huo yapo mahusiano makubwa baina ya ushiriki katika uchaguzi huru na upatikanaji wa huduma za jamii.
Pia kipengele cha pili cha Ibara ya 21 ya Katiba kinatamka kuwa kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa, hivyo ni wazi kuwa uchaguzi ni moja ya haki za kijamii inayomhusu kila Mtanzania.
Kwa mujibu wa ibara ya 145 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Serikali za Mitaa ndiyo mamlaka za wananchi ambazo huundwa, huendeshwa na huwajibika kwa wananchi ambao ndiyo chimbuko la mamlaka yote katika nchi.
Aidha ibara ya 146 Katiba inazitambua Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama vyombo vya haki vyenye mamlaka ya kuwashirikisha wananchi kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma muhimu na kuhakikisha zinasimamia utoaji huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji, afya, kilimo, ufugaji na uvuvi, barabara, maliasili na utalii n.k.
Aidha, mamlaka hizo zipo kwa lengo la kukuza demokrasia kwa kuwashirikisha wananchi kuchagua viongozi wao na kwa mantiki hiyo ushiriki wa wananchi katika chaguzi za vyama vingi zilizo huru na haki (kidemorkasia) ni nguzo muhimu ya kukuza utawala bora na dhana ya maendeleo kwa ujumla.
Tarehe 24 Novemba mwaka huu Watanzania wanatarajia kushirki katika Uchaguzi wa uchaguzi wa sita chini ya mfumo wa vyama vingi kuwachagua viongozi wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa wanaotakiwa kuwepo madarakani kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2024.
Uchaguzi huo unatarajia kutoa taswira na mwongozo juu ya namna wananchi watakavyoshiriki katika maamuzi na pia katika shughuli za maendeleo, uchumi wa nchi, huduma za jamii na maisha yao kwa ujumla ikiwemo usimamizi wa miradi ya maendeleo ambayo itakuwa na manufaa kwa umma.
Uwepo wa viongozi imara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa utawezesha Serikali kuepuka hasara katika mikataba mbalimbali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo afya, elimu, maji na ujenzi kutokana na ukweli kuwa Serikali za Mitaa ndizo zinazofanya kazi moja kwa moja katika jamii katika kutoa maamuzi.
Upo uhusiano mkubwa wa kura yako na suala la maendeleo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuwa uchaguzi huo huweza kuleta viongozi wanaopaswa kusimamia rasilimali muhimu ikiwemo makusanyo ya mapato ikiwemo kodi, mikopo na michango ya kijamii, fedha zitokanazo na huduma, ada ya leseni, ushuru, vibali n.k.
Moja ya changamoto kubwa zilizokuwepo hapo awali katika Mamlaka za Mitaa ni pamoja na usimamizi na matumizi ya rasilimali fedha jinsi inavyokusanywa na kutumika, hivyo kupitia uchaguzi huo wananchi wanapata fursa ya kutafakari kuhusu mtu wanayemtaka kumchagua kama anatosha kusimamia rasilimali hiyo.
Ni wazi kuwa moja ya jukumu la anayechaguliwa ni pamoja na kutatua kero au changamoto nyingine kuhusu afya, elimu, maji, migogoro ya ardhi na mipaka, hivyo mpigakura anapaswa kutambua kuwa anayepaswa kuchaguliwa anaweza kuzikabili changamoto hizi katika kijiji, kitongoji au mtaa.
Pia Uchaguzi wa Mitaa utawawezesha wananchi kuchagua viongozi wawajibakaji wanaopaswa kutoa na kusoma taarifa ya mapato na matumizi katika mikutano maalum ya mitaa, vijiji a vitongoji jambo limekuwa likikwepwa na Viongozi na watendaji katika Mamlaka hizo na hivyo kuzua malalamiko kuhusu wajibu wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji kwa wananchi.
Ni wajibu wa wadau na wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye upigaji kura ili kuitumia vyema haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa kwa kuwa serikali itahakikisha uwapo wa utulivu na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment