Habari za Punde

Ndege Ya Tanzania Yashikiliwa Canada, Serikali Yaelezea Masikitiko Yake

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa,  ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania ( ATCL), Bombardier Q400 iliyokuwa iwasili nchini hivi karibuni,  inashikiliwa nchini Canada na kesi ipo mahakamani.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Mabalozi mbalimbali, Waziri Kabudi amesema kuwa, ndege hiyo inashikiliwa baada ya kufunguliwa kwa kesi mpya, kesi ambayo imefunguliwa na  Mkulima aliyeshindwa Kesi aliyoifungua nchini Afrika Kusini.

Profesa Kabudi ameongeza kuwa,  Serikali imekasirishwa na vitendo vya  ndege zake  kushikiliwa nchini Canada, na kwamba tayari amekutana na kufanya mazungumzo na  Balozi wa Canada hapa nchini kumueleza kuhusu jambo hilo.

Waziri Kabudi pia ametumia hafla hiyo kuwataka Mabalozi hao wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye Mataifa mbalimbali, kwenda kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali, kwa kuwa kumekua na matumizi mabaya ya fedha  kwenye Ofisi za Ubalozi.

Ametolea mfano Ubalozi wa Tanzania huko Addis Ababa - Ethiopia  ambapo kumekua na ubadhirifu mkubwa na fedha na kuongeza kuwa kwa sasa Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) inaendelea na uchunguzi.

Katika hafla hiyo, Rais John Magufuli amewaapisha Mabalozi Watano ambao wanakwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.