Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein akikabidhiwa Qasweeda ya Mwaka huu Al Hijra 1441 na Mshauri wa Jumuiya ya Malide Nabii Zanzibar Sheikh Sherali Champsi (kushoto) wakati wa hafla ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammed (S.A.W) yaliofanyika katika viwanja vya Maisara Suleiman Wilaya ya Mjini Unguja jana usiku 9-11-2019.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliwaongoza
Waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi mbali mbali katika Maulidi ya
kuadhimisha Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kitaifa yaliofanyika katika viwanja
vya Maisara mjini Zanzibar.
Sherehe hizo za
kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka Kitaifa hapa
Zanzibar ni miongoni mwa kawaida na mila ya Waislamu wa Zanzibar ambao huungana
na Waislamu wenzao wote duniani ambapo kwa hapa nchini zilianzishwa mapema
mnamo mwaka 1926.
Alhaj Dk. Shein
aliungana na Waislamu pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na viongozi wa
Dini na wananchi ambapo pia, Mama Mwanamwema Shein nae alihudhuria Maulid hayo
akiwa pamoja na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa.
Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar
Sheikh Hassan Othman Ngwali alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote
pamoja na viongozi mbali mbali waliohudhuria katika Maulid hayo akiwemo Alhaj
Dk. Ali Mohamed Shein ambae pia, ni mlezi wa Jumuiya ya Milade e Nabii
ambayo inasimamia shughuli za Maulid ya
kitaifa hapa nchini.
Katika Sherehe hizo, Waislamu walisisitizwa suala zima la
amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na kutakiwa kufuata nyayo za Mtume
Muhammad (S.A.W) ili wapate kuongoka hapa duniani na kesho akhera.
Akisoma khutba ya
Maulid hayo, Sheikh Hassan Ali Kombo kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana
alisema kuwa kila Muislamu inampasa kumpenda Mtume Muhammad (S.A.W) yeye na
kizazi chake huku akisisitiza haja ya uendeleza utamaduni huo ambao umekuwa
ukitumika kwa muda mrefu hapa Zanzibar.
Aidha, Sheikh Hassan aliwataka Waislamu kuwa kitu kimoja na kusisitiza umuhimu
wa kuimarisha umoja na mshikamano kwa
lengo la kupata rehema za Allah.
Sheikh Hassan pia, alitumia fursa hiyo kukemea mambo maovu
katika jamii hasa suala la unyanyasaji wa wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na
suala zima la ubakaji jambo ambalo limeshamiri hivi sasa katika jamii na
kueleza athari zake na kutaka mashirikiano ya pamoja katika kulipiga vita.
Aidha, alieleza kuwa
ni jukumu la Waislamu kusherehekea siku hii adhimu pamoja na kumcha Mwenyezi
Mungu, kufuata kitabu chake cha Qur-an pamoja na kufuata mafunzo ya Mtume
Muhammad (S.A.W) aliyokuja nayo.
Mapema Mshauri Mkuu wa
Kamati ya Maandalizi wa Jumuiya ya Milade e Nabii ambayo inasimamia shughuli za Maulid ya kitaifa hapa
nchini Sheikh Sherali Champsi alieleza
historia ya Maulid hapa Zanzibar ambayoinatimiza miaka 94 tokea kuanzishwa kwa
shughuli hizo hapa nchini.
Sherehe hizo za Maulid
ambazo husherehekewa duniani kote, zilianza kufunguliwa na Qur-an tukufu
iliyosomwa na Ustadhi Miraji Nyange
Khamis kutoka Kigunda Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo tafsiri yake
ilitolewa na Sheikh Ilyasa Hassan Hamad kutoka Chuo cha Kislamu Mazizini mjini
Unguja.
Milango ya Maulid Barzanji iliyoenda sambamba na
Qasweeda ilisomwa na Maustadhi kutoka vyuo mbali mbali vya Qur-an kutoka Unguja
na Pemba yakiwemo Maulid ya Hom kutoka Jumuiya ya Maulid ya Hom Mtendeni, Mkoa
wa Mjini Magharibi ambayo nayo yalikuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo adhimu.
Katika sherehe hizo za
Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Madrassa Noor El Islamiya ya Mji
Mkongwe, Mjini Unguja ilisoma Qiyaam Talaa, kilichotanguliwa na Mlango wa nne
uliosomwa na Ustadhi Juma Faki Omar kutoka Amani, Mjini Unguja.
Qasweeda ya mwaka 1441
Al Hijra, ilisomwa na wanafunzi kutoka Madrassa Munawara ya Shaurimoyo, Mkoa wa
Mjini Magharibi ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maulid
hayo Sheikh Sherali Chapsi alitumia fursa hiyo kama ilivyokaida kwa kila mwaka
kumkabidhi Rais, Qasweeda hiyo maalum.
Maulid hayo
yalimalizika kwa Mlango wa dua uliosomwa na Abubaker Said Abubaker, kutoka Mji
Mkongwe Unguja na hatimae kufungwa kwa fatha iliyosomwa na Naibu Mufti Mkuu wa
Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi chini ya mshereheshaji Mohammed Suleiman
(Tall).
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment