RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,
akizungumza na Ujumbe wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland cha Nchini
Norway, ukiongozwa na (CEO) Mr. Eivind Hansen (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu
Zanzibar kwa mazungumzo na Rais leo 22-11-2019
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland ya nchini Norway kusaidia ujenzi wa Hospitali ya wagonjwa wa akili, Kidongo Chekundu ambayo itakuwa ya kisasa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland ya nchini Norway
ukiongozwa na Trond Mohn aliyefuatana na rafiki zake pamoja na familia yake
wakiwa pamoja na uongozi wa Wizara ya Afya.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa hiyo ni habari njema na ya kujivunia inayotokana na uhusiano, ushirikiano
na urafiki wa muda mrefu unaoendelezwa kati ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha
Haukeland ya nchini Norway na Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.
Aliongeza kuwa
Hospitali ya wagonjwa wa akili iliyopo Kidongo Chekundu ni hospitali kongwe
katika hospitali kadhaa hapa nchini ambayo ina historia kubwa inayotokana na
utoaji huduma zake kwa wakati huo ilipojengwa na wakoloni wa Kiengereza mnamo
miaka ya 50 ambapo ilipewa jina na jamii kwa kuitwa “Jela ya Wendawazimu”.
Hivyo, hatua za
kuijenga upya Hospitali hiyo na kuwa ya kisasa na ya pekee katika ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati itakuwa ni faraja kubwa kwa Wazanzibar kwa kuiimarisha
sambamba na kutoa huduma za kisasa za wagonjwa wa akili na kuwa msaada mkubwa
kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.
Alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake mkubwa kwa uongozi
wa Hospitali hiyo chini ya kiongozi wake mkuu Trond Mohn ambayo imekusudia
kujenga Hospitali ya wagonjwa wa akili ya Kidongo Chekundu na kuwa ya pekee
katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Rais Dk. Shein
aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana mashirikiano
inayotoa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hakeland katika kusaidia kuimarisha sekta
ya afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusaidia ujenzi wa majengo kwa ajili ya
huduma za afya na tiba, vifaa, wataalamu pamoja na mafunzo kwa madaktari wa
Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliupongeza uongozi huo kwa kufanya kazi na Wizara ya Afya kupitia Hospitali
Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kwa muda wa miaka kumi hivi sasa hatua ambayo
imeweza kukuza na kuimarisha sekta ya afya nchini sambamba na kuendeleza huduma
za kijamii na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na Sera yake
ya kutoa huduma za afya bure, Sera ambayo iliasisiwa na Jemedari wa Mapinduzi
matukufu ya Januari 12, 1964 Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na hadi hivi
leo inaendelezwa.
Aliongeza kuwa juhudi
za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuhakikisha sekta ya afya inaimarika ambapo pia, nchi marafiki pamoja na
mashirika ya Kimataifa yamekuwa yakiendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuhakikikisha sekta ya afya inaimarika na wananchi wanapata huduma za afya.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein aliukaribisha Zanzibar uongozi wa Hospitali hiyo ulioongozwa na
Kiongozi Mkuu na Mfadhili wa Hospitali wake Trond Mohn na kuueleza jinsi sekta
ya utalii ilivyoimarika hapa nchini na vipi inachangia uchumi wa Zanzibar.
Nae Afisa Mtendaji
Mkuu wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland Eivind Hansen alimueleza Rais Dk.
Shein kuwa Hospitali hiyo inajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati
yake na Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambapo tayari imeshatimia miaka
10 tokea kuanzisha mashirikiano hayo.
Afisa Mkuu huyo alieleza
kuwa Hospitali ya Haukeland imeweza kushirikiana na Hospitali ya Mnazi Mmoja
kwa kuanzisha na kuendeleza miradi mbali mbali ikiwemo ya ujenzi wa majengo kwa
ajili ya kutoa huduma za afya, mafunzo wka madaktari, vifaa na wataalamu.
Alieleza kuwa mbali ya
mashirikiano hayo pia, kumekuwa na mashirikiano mazuri ya kubadilishana
wataalamu na utaalamu kati ya madaktari wa Hospitali ya Haukeland na Hospitali
Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja jambo ambalo kuna haja ya kuendelezwa.
Pamoja na hayo
alieleza kuwa, Hospitali hiyo ya Haukeland imekuwa ikitoa ufadhili wa mafunzo
kwa madaktari wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kila mwaka utamaduni ambao uongozi
huo umeahidi kuuendeleza.
Uongozi huo wa
Hospitali ya Haukeland ulieleza kuwa tayari mradi wa ujenzi wa Hospitali ya
wagonjwa wa akili ya Kidongo Chekundu umeshafikia asilimia 50 ambapo majengo
mapya zaidi yatajengwa, pamoja na ukarabati wa majengo ya zamani katika eneo
hilo huku akieleza kuwa mradi huo pia, utahusisha mafunzo kwa wafanyakazi.
Aidha, uongozi huo
ulisisitiza kwamba azma na lengo lao ni kuifanya Hospitali hiyo ya Kidongo
Chekundu kuwa ya pekee itakayotoa huduma za kisasa kwa wagonjwa wa akili katika
nchi za Bara la Afrika.
Waliongeza kuwa katika
ziara yao ya hapa Zanzibar pia, wamepanga kukutana na kukaa pamoja na uongozi
wa Wizara ya Afya pamoja na Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kujadiliana masuala
mbali mbali ya uendelezaji na uimarishaji wa miradi ya sekta ya afya hapa
nchini.
Katika maelezo yao
uongozi huo pia, ulieleza azma yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa kuendeleza na
kuanzisha miradi mipya ya sekta ya afya sambamba na kuimarisha mashirikiano na
Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment