Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizindua kitabu cha Historia ya Maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa akishuhudiwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na Balozi wa Finland nchini Tanzania Mhe. Antila Sinikka katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumanne Novemba 12, 2019
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein leo ameungana na viongozi mbali mbali wa Kitaifa katika
uzinduzi wa Kitabu cha Maisha Binafsi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Benjamin William Mkapa chenye jina la “My Life, My Purpose”.
Sherehe za Uzinduzi
huo zilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa
wa Julius Nyerere ( JNICC) Jijini Dar-es-Salaam, ambapo
mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe
Joseph Magufuli.
Katika hotuba yake ya
uzinduzi wa kitabu hicho Rais Magufuli alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea
kumpa afya njema na umri mrefu na baraka nyingi Rais Mkapa ambae ni aliweza
kumuunga mkono sana katika uongozi wake tokea akigombea nafasi ya Ubunge ya
Jimbo Biharamulo Mashariki ambalo hivi sasa ni Jimbo la Chato wakati Mzee Mkapa
akigombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Magufuli alieleza
historia fupi ya nafasi aliyomteua mara tu baada ya uchaguzi huo wa mwaka 1995 ambapo
Rais Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa
Wizara ya Ujenzi chini ya Mama Anna Abdalla.
Aidha, Rais Magufuli
alieleza jinsi alivyojifunza mambo mbali mbali kutoka kwa Rais Mkapa kwa
kueleza kuwa viongozi wote mbele ya Rais Mkapa wakati wa uonmgozi wake walikuwa
na haki sawa sambamba na kuwaunga mkono katika kazi zao, zikiwemo kazi
alizozifanya pamoja na uwamuzi wa Rais Mkapa katika shughuli zake za kazi hasa
katika ujenzi wa barabara pamoja na madaraja hapa nchini.alifanya jitihada
kubwa za kuondoa Umasikini,
Alieleza mafanikio ya
Rais mstaafu Mkapa ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mkakati wa Kuondoa Umasikini na
Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Mali na Biashara
Tanzania (MKURABITA), Mradi wa (TASAF), Kuimarisha huduma za jamii zikiwemo
elimu na kuongoza idadi ya wanafunzi wa skuli za msingi sambamba na kuendelea
kutunza amani na umoja wa Watanzania.
Alieleza kuwa Watanzania
wengi na watu mbali mbali duniani kupitia kitabu hicho watamfahamu Mzee Mkapa
pamoja na kuifahamu vyema Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Rais Magufuli alieleza
jinsi Mzee Mkapa alivyogusia suala zima la imani katika kitabu chake hicho
jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Mzee Mkapa ni kiongozi MchaMungu.
Alieleza kuwa kutokana
na nidhamu na uwajibikaji wake Rais mstaafu Mkapa aliweza kupata nafasi mbali
mbali za uongozi ndani na nje ya Tanzania na hatimae kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Pamoja na hayo, alieleza
kuwa hata baada ya kustaafu nafasi yake ya Urais, Rais mstaafu Mkapa ameendelea
kuisaidia Tanzania na nchi nyengine nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kujenga
utawala bora katika bara la Afrika pamoja
na kusimamia amani na kuwa msuluhishi.
Aidha, Rais Magufuli alisisitiza
haja ya kumshukuru mzee Mkapa kwa kuweza Tanzania kujenga barabara zake kwa
fedha zake za ndani pamoja na na kumuunga mkono sambamba na kumsaidia kwa kiasi
kikubwa katika uongozi wake.
Alisisitiza kuwa Mzee
Mkapa ndio shujaa wake katika maisha yake yote na kutoa wito kwa Watanzania
kuwaenzi na kuwatunza wazee wote wakiwemo viongozi wastaafu ambao wana mambo
mengi ya kujifunza kutoka kwao .
Alieleza jinsi
alivyovutiwa na Sura nyingi za Kitabu hicho ambazo zimeeleza namna ya kuendelea
kujitegemea kazi ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali anayoiongoza na kuyapa
kipaumbe katika azma ya kuondokana na utegemezi.
Kitabu hicho kinaeleza
historia ya Rais mstaafu Mkapa kuanzia alipozaliwa, safari yake ya masomo,
safari ya kisiasa ikiwemo uongozi wa nchi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005 na pia, mchango wake mkubwa
alioutoa kwa Taifa na Kimataifa katika masuala ya uongozi.
Aliitumia fursa hiyo
kuipongeza Taasisi ya Uongozi na kutoa wito wa kukifanyia tafsiri ya lugha ya
Kiswahili kitabu hicho.
Aliwahimiza viongozi
wastaafu wengine kuiga hatua za Mzee Mkapa kwa kuandika vitabu vya maisha yao
na kupiongeza hatua zinazoendelea za kuandika kitabu cha Rais Mstaafu Mzee Ali
Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu Mzee Jakaya Mrisho Kikwete.
Alihamasisha Taasisi
hiyo ya uongozi kwa kuendeleza historia za viongozi na kuwasisitiza Watanzania
kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu huku akitoa wito kwa Watanzania kuendeleza
umoja na mshikamamo wao na wasikubali kuyumbishwa na badala yake washirikiane
katika kuijenga Tanzania ili izidi kuleta maendeleo .
Rais mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa ambaye leo
ndio siku yake ya Kuzaliwa na kufikisha umri wa miaka 81 alitoa shukurani kwa
wale wote waliomuunga mkono katika kutayarisha kitabu hicho huku akimuelezea
Rais Julius Kambarage Nyerere kwa jinsi alivyojifunza mambo mengi kutoka kwake.
Alieleza kuwa suala la
kujitegemea ni moja ya mada aliyoiandika katika kitabu chake hicho na
kumpongeza Rais Magufuli kwa kulipa kipaumbele suala hilo huku akieleza kuwa
kitabu hicho kitampa fursa ya kutoa shukurani kwa wale wote aliofanya kazi nao
sambamba na kueleza ukombozi wa bara la Afrika.
Alieleza kuwa katika
kitabu chake hicho amemuelezea Mwalimu Nyerere kwa mtazamo wake kama anavyomjua
jambo ambalo limempa faraja kubwa sana. Na kueleza kuwa kitabu hicho
kitawasaidia wanafunzi na viongozi pamoja na vizazi vijavyo.
Mapema Profesa Joseph
Semboja Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi alitoa maelezo mafupi ya
Mradi wa Tawasifu na kueleza kuwa taasisi
yake iliyoanzishwa mwaka 2010 ndio iliyokuwa na jukumu la kutayarisha kitabu
hicho na kumuunga mkono.
Alieleza kuwa hivi
karibuni Taasisi hiyo itatoa kitabu cha Maisha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya
Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na kuongeza kuwa viongozi wengi wakiwemo wa nchi
za Magharibi wamekuwa na utamaduni wa kuandika vitabu vya historia ya maisha
yao na kutoa shukurani kwa viongozi hao ambao hufanya hivyo na watu kupata
kuvisoma na kuwasaidia
Kwa bahati mbaya Profesa
Semboja alieleza kuwa viongozi wengi wa Bara la Afrika hawapati nafasi ya
kuandika vitabu vyao kutokana na mazingira yao na badala yake hujifunza
maandishi kutoka kwa nchi nyengine wanazoandika vitabu kama hivyo.
Alieleza kuwa historia
ya kiongozi katika bara la Afrika si historia yake binafsi bali ni historia ya
nchi nzima na kueleza kuwa Mzee Mkapa ameandika historia ya nchi na sio
historia yake binafsi na ndio maana uzinduzi wake umejumuisha makundi mbali
mbali na tukio hilo si la kifamilia bali ni la Kitaifa.
Aliongeza kuwa mwaka 2016
mchakato wa kuandika kitabu hicho ulianza na kutoa shukurani kwa watu
walioshiriki kwa namna moja ama nyengine kufanikisha kitabu hicho..
Kampuni ya Uchapishaji
ya Mkuki na Nyota kimechapisha kitabu hicho ambapo jumla ya TZS Milioni 230
sawa na Dola za Kimarekani laki Moja zimetumika ambapo gharama hizo sio kubwa
ikilinganishwa na gharama za vitabu vinavyochapishwa na viongozi wengine katika
nchi nyingi duniani wakiwemo viongozi wastaafu wa Marekani.
Alieleza kuwa kitabu
hicho kinauzwa kwa bei nafuu na kinapatikana sehemu mbali mbali Hapa Tanzania
ikiwemo Jijini Dar-es-Salaam, Zanzibar, Mwanza, Dodoma na sehemu nyenginezo
ikiwa ni pamoja na kwenye mitandao.
Nae Profesa Rwekaza
Mukandala Mgoda wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitoa uchambuzi wa Kitabu
hicho cha Rais Mkapa ambacho kina Sura 16
na kurasa 320 pamoja na utangulizi uliotayarishwa na Rais mstaafu wa Msumbiji
Rais Chisano.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment