Habari za Punde

BODI AMBAZO HAZITAWASILISHA GAWIO IFIKAPO JANUARI 23 ZITAKUWA ZIMEVUNJWA





Serikali imesema  Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma ambazo hazitawasilisha gawio na michango yao kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali  ifikapo Januari 23 mwaka 2020, kabla ya saa 6 usiku, Bodi zitakuwa zimevunjwa na watendaji wake kupoteza ajira zao.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, wakati akipokea gawio na michango kutoka Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 11, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alilolitoa Novemba 24 mwaka huu lililozitaka taasisi hizo kutoa gawio ndani ya siku 60.
Alisema itakapofika saa sita usiku ya tarehe 23 Januari, 2020 kama hawajaleta gawio wala michango ya kuingia kwenye mfuko Mkuu, Bodi hizo zimevunjwa, Watendaji Wakuu wa hizo taasisi husika nao watahusika na akabainisha kuwa hiyo ndiyo amri ya Serikali.
 “Tukio la Novemba 24, 2019 la kupokea gawio, mashirika yalikuwa 79 na Mhe. Rais, alipokea hundi ya jumla ya Sh. trillion 1.05 na aliniagiza ndani ya siku 60, Taasisi, maashirika na kampuni 187 ambazo hazikutoa gawio siku hiyo zitekeleze maagizo yake”, alieleza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa baada ya agizo la Rais, katika kipindi cha siku 18, Taasisi, Kampuni na Mashirika 58 yametekeleza agizo ambapo jumla ya fedha zilizopokelewa katika mfuko Mkuu wa Hazina ni Sh. bilioni 12.12.
Dkt. Mpango aliyapongeza mashirika, kampuni na taasisi hizo kwa kuitikia wito huo kwa kutoa fedha hizo ambazo amesema zitasaidia katika shughuli za maendeleo  ya nchi kwa njia ya ujenzi wa miradi na kuiwezesha nchi kujitegemea.
Alisema kuwa amefurahishwa na gawio na michango lakini amesema wanatakiwa kuongeza kiwango hicho mwakani kwa kuwa Watanzania wanatakiwa kuona kuwa waliopewa  dhamana  ya kusimamia mashirika yao wanatimiza wajibu wao.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbutuka, amesema idadi ndogo ya kampuni, mashirika na taasisi ya umma 71 kati ya 266 yaliyo katika orodha ya Msajili wa Hazina yaliyochangia gawio na michango mingine wakati Mhe. Rais Magufuli akipokea magawio hayo kwa niaba ya  wananchi, haikumfurahisha Kiongozi huyo wa Nchi.
Miongoni mwa Taasisi zilizotoa mchango ni pamoja na Chuo cha kilimo- SUA, Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini- IRDB, Taasisi ya Taifa ya  Usafirishaji – NIT, Mfuko wa Misitu Tanzania- TFF, Chuo cha Ufundi Stadi- VETA, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Kudhibiti ubora wa Mbegu Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.