Habari za Punde

Hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Wakati wa Kuahirisha Mkutano wa Kumi na Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi 06 Disemba 2019

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisoma Hotuba ya Kuahirisha Mkutano wa Kumi na Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Tumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwenye wingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi na sita wa Baraza la Tisa ambao ulioanza tarehe 27 Novemba, 2019 na leo hii tunauahirisha.
Mheshimiwa Spika,
Kama kawaida yangu napenda kuchukuwa fursa hii kukupongeza wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Spika wa Baraza letu Tukufu pamoja na Naibu Spika wako, na Wenyeviti wote wa Baraza kwa kuviendesha vyema vikao vyetu kwa hekima, busara na weledi mkubwa zilizopelekea mkutano huu kuwa na  mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika kikao hiki jumla ya maswali ya msingi 96 yaliulizwa na yalijibiwa kwa ufasaha na ufafanuzi wa kina kutolewa na Waheshimiwa Mawaziri.
Nawashukuru wote waheshimiwa na Wajumbe wote  waliouliza na pia nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliotoa majibu kwa umakini, kwani maswali na majibu ni njia muwafaka inayowasaidia wananchi wetu kuelewa kwa urahisi utendaji wa Serikali yao, yakiwemo mafanikio na changamoto zake.
Mheshimiwa Spika,
Baraza lako tukufu limepokea na limejadili Miswada mitano na hatimae kuipitisha; Miswaada yenyewe ni :-
·       Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria kuanzisha Ofisi ya Mufti, Nam. 9 ya 2001;
·       Mswada wa Sheria ya kuanzisha Wakala Serikali Mtandao, Kazi zake na Mambo mengine yanayohusiana na hayo;
·       Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbali mbali na kuweka masharti bora ndani yake;
·       Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usafiri barabarani Nam. 7 ya mwaka 2003 na
·       Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Wakala wa Barabara Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo;
Mheshimiwa Spika,  
Waheshimiwa Wajumbe walipata wasaa wa kutosha kujadili kwa kina miswada yote hii mitano.
Mheshimiwa Spika,
Naomba niwakumbushie kwamba katika hotuba yangu ya kuakhirisha Mkutano wa kumi na tano wa Baraza la tisa tarehe 04 Novemba, 2019 nilieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukabiliana na maradhi ya mripuko imezindua Mpango Shirikishi wa miaka kumi (10) wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar ‘’Zanzibar Comprehensive Cholera Elimination Plan 2018-2027’’ wenye lengo la kuondosha kabisa usambaaji wa vimelea vinavyoeneza maradhi ya kipindupindu hapa Zanzibar.  Nina faraja kubwa kulieleza Baraza lako tukufu kwamba katika kufanikisha azma hiyo Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza kufanya Utafiti wa kitaalamu unaojulikana kwa jina la ‘Cholera situation analysis and epidiological study of cholera hotspots in Zanzibar to inform preparedness and response planning’ Utafiti huo wenye lengo la kuelewa maeneo hatarishi ya kipindupindu nchini ili kupanga mipango ya kukabiliana na ugonjwa huo unafanyika  katika Wilaya ya Mjini, Wilaya ya Magharibi A, Wilaya ya Magharibi B kwa Unguja, kadhalika Wilaya ya Wete na Wilaya ya Micheweni  kwa upande wa Pemba. Nachukuwa nafasi hii kuwataka Waheshimiwa
Wawakilishi pamoja na wananchi wote kutoa mashirikiano kwa watendeaji wa zoezi hili ili kufikia azma ya Serikali yetu ya kutokomeza maradhi ya kipindupindu Zanzibar. “KWANI ZANZIBAR BILA YA KIPINDUPINDU INAWEZEKANA “
Mheshimiwa Spika,
Vitendo vya Udhalilishaji bado vinaendelea kuwa tishio katika nchi yetu vikitoa sura mbali mbali ikiwa ni pamoja kupigwa na kubakwa kwa wanawake na watoto wadogo, kutelekezwa kwa watoto wachanga, talaka zisizofata utaratibu, ushirikishwaji wa watoto wenye umri mdogo katika biashara zikiwemo biashara haramu za dawa za kulevya.  Vitendo hivyo vinakwenda kinyume na sheria, mila, silka, desturi na utamaduni wetu. Kwa mara nyengine tena nawakumbushia wazee, jamii na viongozi wa ngazi na nyanja mbali mbali pamoja na wananchi, kuwa kila mmoja wetu kuendelea kutekeleza wajibu wake katika kupinga suala hili. Naomba tuelewe kuwa “Kila mmoja ni mchunga na kila mchunga ataulizwa juu ya uchungaji wakeKwa upande wa Serikali inavisisitiza vyombo vyote vinavyohusika pamoja na wadau wote kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kukomesha kabisa vitendo vya udhalilishaji katika jamii yetu bila ya kumuonea haya mtu yoyote. 
Mheshimiwa Spika,
Wakati Serikali  ikiendelea na hatua mbali mbali za uimarishaji wa ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja, vibomba, kuweka alama za barabarani, jambo la kusikitisha ni kuonekana kwa kuendelea kutokea ajali za barabarani ambazo zinaendelea kutishia maisha yetu, kutuachia simanzi na majonzi. Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Mtakwimu Mkuu na kuripotiwa katika Gazeti la Kingereza Zanzibar Mail zinatisha. Kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu tumepoteza watu 145 kwa ajali za barabarani. Kwa uchanganuzi zaidi watu 12 walifariki kila mwezi kutokana na ajali katika kipindi hicho. Hii ni hali ya kutisha na lazima tuchukuwe hatua madhubuti kupambana na ajali nchini ikiwemo kuhakikisha asiyekuwa na leseni ya udereva haendeshi chombo, walevi wanadhibitiwa kuendesha vyombo vya moto, alama za barabarani zinaheshimiwa na mwenye kuzivunja anaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika,
Kama inavyoeleweka kwamba suala la dawa za kulevya ni janga kubwa duniani kote, wazee, vijana na watoto wa jinsia na rika zote wameathirika na janga hili. Madhara yake kwa jamii yetu tunayaelewa sote. Kutokana na hali hiyo Serikali inaendelea kuchukuwa hatua mbali mbali za  kupambana, kukemea, kuchukia shughuli yoyote inayoshajihisha matumizi yake na   inachukua hatua kali sana kuhakikisha inatokomeza na kudhibiti uingizwaji, usambazaji na utumiaji dawa za kulevya  nchini.  Hivyo, tunawaomba wananchi wote waendelee kutoa ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na kuwafichua wale wote wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
Suala la kudumisha amani na utulivu kwa nchi yetu wananchi  wake, rasilimali zake ni jukumu la kila mwananchi aliyemo nchini kwetu. Hivyo, naviomba vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuhakikisha amani na utulivu inalindwa kwa gharama yoyote ile hasa tukiwa tunaelekea katika Sherehe za Mapinduzi yetu Matukufu yanayotegemewa kilele chake hapo tarehe 12 Januari, 2020.  Si vyema tukawaachia baadhi ya wanasiasa uchwara au watu wanaoahidi kutaka kuvunja amani yetu kwa kauli au kwa vitendo nchini kwetu, naomba sana hatua kali zianze kuchukuliwa na wakibainika sheria ifate mkondo wake.
 Mheshimiwa Spika,
Muda si mrefu ujao, uandikishaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura utafanyika hapa Zanzibar, kwa upande wa NEC na ZEC hivyo, nawataka Wawakilishi wachukue nafasi hii kuwahamasisha wananchi wetu kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba na kisheria ili waweze kujiandikisha na hatimae kupiga kura kwa kiongozi wanaemtaka kwa maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Uwazi, uwajibikaji, maadili na ukweli ni chachu ya mafanikio kwa Utumishi wa Umma na nchi yetu.  Hivyo niwatake watendaji wote wa umma wawe waadilifu na kuwa na uchungu na rasilimali za nchi, sio vyema tukawa tunapanga mbinu za kuhujumu, rasilimali za Taasisi zetu kwa kujibinafsisha, kuongeza thamani, kutumia muda wa kazi au kutotoa huduma stahiki kwa wananchi na kujali maslahi binafsi.  Naomba sana mtindo huu ukomeshwe mara moja na Tume ya Maadili ya Umma na Wizara ya Kazi, Utumishi wa Umma na Utawala bora wajitahidi kufuatilia maaadili ya watendaji na kuchukua hatua stahili.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kumalizia hotuba yangu napenda kuwashukuru wale wote waliotuwezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Kumi na Mbili wa Baraza la Tisa la Wawakilishi kwa ufanisi.  Pongezi hizo zaidi ziwafikie watendaji wote wa Baraza hili la Wawakilishi wakiongozwa na Katibu wa Baraza Ndugu Raya Issa Mselem pamoja na Watendaji wake wote.  Pia nawapongeza wakalimani wetu wa lugha ya alama ambao wamewawezesha wanchi wetu  wenye  ulemavu  wa  kusikia kuweza kufuatilia yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Baraza hili Tukufu.  Vile vile, nawashukuru wanahabari kwa kufanya kazi nzuri ya kuwapatia habari wananchi wetu kwa shughuli zote ambazo zilikuwa zikiendelea kufanyika Barazani hapa.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na taadhima kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liakhirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 5 Febuari, 2020 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
 Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.