Habari za Punde

Maandalizi ya Kongamano la Sita la Diaspora Litakalofanyika Zanzibar Yakamilika Maandalizi Yake - Waziri Mhe Gavu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi(Gavu)akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari  kuhusiana na Kongamano la sita la Kitaifa la Watanzania wanaoishi nje ya Nchi(DIASPORA) litakalofanyika katika Hoteli ya Verde Zanzibar Disemba mwaka huu.
Na Maelezo Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa Mgeni rasmin katika kongamano la siku mbili la Diaspora ambalo linatarajiwa kufanyika katika Hoteli ya Verde Zanzibar tarehe 14-15 Mwezi huu.
Hayo ameyasema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi (Gavu) huko katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Kongamano hilo.
Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa kongamano la sita la Kitaifa la Watanzania wanaoishi nje ya Nchi.
Hivyo amesema kongamano hilo ni muendelezo wa makongamano mengine matano ya awali yaliyofanyika Tanzania Bara na Zanzibar yakiwa na lengo la kuwakutanisha wanadiaspora .
Pia ameeleza kongamano hilo linapelekea kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na kuwashajihisha kuzitumia fursa zilizopo kwa kuekeza miradi yenye maslahi na  ustawi wa uchumi wa Nchi yao ya asili.
Aidha amesema kuwa  washiriki wapatao 300 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo miongoni mwa washiriki ni pamoja na wanadispora  na wawekezaji 150 kutoka nchi mbali mbali duniani na watendaji 150 kutoka Taasisi za umma,binafsi za Tanzania Bara na Zanzibar .
Vile vile amesema Serikali zote mbili zimekuwa zikitumia fursa la kongamano hilo kujadiliana na wanadiaspora na hatimae kuweka wigo mpana zaidi wa kushirikiana kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya nchi.
Dhamira ya kongamano hilo ni “kuimarisha ushirikiano na Diaspora kama ni moja ya washirika wa maendeleo"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.