Habari za Punde

SMT Imetiliana Saini na BADEA Ujenzi wa Skuli za Ghorofa Zanzibar.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetiliana saini na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA)Mkataba wa Mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni 13.5 kwa ajili ya Ujenzi wa skuli za Sekondari za Ghorofa (Roshani)za Zanzibar.

Sherehe hizo za utiaji saini mkataba huo wa makubaliano zilifanyika jumamosi 21 Dec 2019 katika Makao Makuu ya Benki hiyo ya BADEA Khartoum nchini Sudan, ambapo kwa Upande wa Tanzania mkataba huo umesainiwa na Mheshimiwa Mohammed Ramia Abdiwawa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwa upande wa BADEA umesainiwa na Dkt.Sidi Ould Tah.

Katika Mradi wa Ujenzi wa Skuli hizo za sekondari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itatoa Dola Milioni 1.5 katika kufanikisha.

Skuli hizo tatu za kisasa zitajengwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi,Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mkoa wa Kaskazini Unguja na kufanya jumla ya Skuli za Sekondari zilizojengwa kwa mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) kufikia tano,ambapo tayari skuli mbili zimeshajengwa na moja inatoa huduma Skuli ya Mohammed Juma Pindua ya Mkoa wa Kusini Pemba na ile ya Sekondari Kibuteni ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi Mwaka 2020.

Sherehe hizo za utiaji saini zimehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Sudan Balozi Silima Haji, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Abdulla Mzee Abdulla, Kamishna wa Fedha za Nje katika Wizara ya Fedha na Mipango Bihindi Nassor Khatib na Loveness Msechu na Ndugu Issaya kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.