RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Vietnam
kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana nchini humo chini ya Chama cha Kikomunisti
cha (CPV).
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo
Ikulu Mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mjumbe na Katibu wa Kamati Kuu ya Uongozi wa
Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV) Bwana Pham Minh Chinh akiwa amefuatana
na ujumbe wa viongozi kutoka Chama hicho.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alisema kwamba nchi hiyo imepata mafanikio makubwa katika nyanja
zote zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa na kueleza kuwa Zanzibar
itaendelea kujifunza kutoka nchi hiyo.
Rais Dk. Shein
aliipongeza Vietnam kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo
ambao umeweza kuleta mafanikio makubwa sambamba na mahusiano kati ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV).
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa ziara ya kiongozi huyo hapa nchini inaimarisha na kukuza uhusiano
na ushirikiano uliopo kati ya Vietnam na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikiwemo Zanzibar pamoja na vyama vikuu vinavyotawala katika nchi mbili hizo.
Alieleza kuwa uhusiano
huo ulianza tokea mwaka 1965 kati ya Vietnam na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
umeweza kuleta manufaa katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo kilimo,
uwekezaji, elimu, biashara pamoja na sekta nyenginezo.
Rais Dk. Shein
alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM, kitaendeleza
urafiki na udugu uliopo kati yake na Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV) ikiwa
ni pamoja na kuendelea kutembeleana kati ya viongozi wa vyama hivyo na wale viongozi
wa Serikali.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein hakuchelea kumueleza kiongozi huyo hatua nzuri na mafanikio
yaliopatikana katika ziara yake aliyoifanya nchini humo mnamo mwaka 2012
kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Troung Tan Sang.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa katika ziara hiyo alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Rais
wa nchi hiyo pamoja na viongozi wengine
wakuu na kujadili masuala mbali mbali yaliyojikita kukuza uhusiano na
ushirikiano wa pande mbili hizo ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya
kilimo, uvuvi, utafiti, biashara na sekta nyenginezo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alitoa pongezi kwa nchi hiyo kutokana na kuendelea kukua kwa uchumi wake pamoja
na kuendelea kuwepo kwa amani, utulivu na usalama ambao umeweza kuipaisha nchi
hiyo katika nyanja za Kimataifa hatua ambayo inafaa kuigwa na mataifa mengine.
Alimueleza kuwa
Tanzania ni nchi ya amani na inafarajika kuona nchi nyengine zinakuwa na amani
kwani panapokuwa na amani maendeleo hupatikana kama ilivyo Vietnam, ambapo aliahidi
kuendelea kushirikiana katika sekta za maendeleo ikiwemo biashara, kilimo na
uwekezaji.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo Kuipongeza Serikali ya Vietnam na chama chake cha
(CPV) kwa kuwahamasisha wawekezaji wa Kampuni ya Halotel kutoka nchini humo
kuja kuekeza Tanzania katika sekta ya mawasilianio.
Rais Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo kuwa wafanyabiashara wa Zanzibar bado wanaendelea
kufanya biashara nchini humo hasa biashara ya mchele hasa ikizingatiwa kwamba
nchi hiyo ni ya pili duniani katika uzalishaji wa bidhaa hiyo.
Nae Mjumbe na Katibu wa Kamati Kuu ya Uongozi wa
Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV) Bwana Pham Minh Chinh alimpongeza Rais
Dk. Shein kwa mafanikio makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar chini ya uongozi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kiongozi huyo wa chama
cha (CPV) alimueleza Rais Dk. Shein kuwa nchi yake inaona fahari mkubwa kuwepo
kwa mashirikiano na uhusiano mwema kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikiwemo Zanzibar.
Alieleza kuwa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imekuwa ni rafiki mkubwa wa Vietnam kwani imeweza
kuiunga mkono nchi hiyo katika mambo mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwa
ni pamoja na suala zima la usalama kupitia Umoja wa Mataifa (UN) sambamba na kuunga
mkono mapambano katika uvamizi wa nchi yao.
Aidha, kiongozi huyo
wa chama cha (CPV), alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ziara yake hiyo yeye na
viongozi wengine wa chama hicho hapa nchini ina lengo la kukuza uhusiano,
ushirikiano na udugu uliopo kati ya (CPV) na (CCM), pamoja na mahusiano kati ya
Serikali za nchi hizo.
Pamoja na hayo,
kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein jinsi nchi hiyo ilivyopata mafaniko na
kupiga hatua katika kuimarisha uchumi wake sambamba na uendelezaji wa amani na
utulivu huku kiongozi huyo akisisitiza haja ya kuendeleza utamaduni wa
kutembeleana kati ya viongozi wa vyama hivyo na Serikali kwa lengo la kukuza
uhusiano na ushirikiano uliopo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment