Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete(JKCI) Prof. Mohammed Janabi akizungumza na Waandishi wa Habari
(pichani), kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo katika miaka minne ya Serikali ya
Awamu ya Tano, mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya
Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam
(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)
Na.Paschal
Dotto-MAELEZO.28-01-2020
Serikali kupitia Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) ikishirikiana na Serikali ya China wanatarajia
kujenga hospitali kubwa ya moyo katika eneo la Mloganzila ambapo hatua za awali
za mchakato wa ujenzi zimekamilika.
Akizungumza katika Mkutano na
Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI,
Prof.Mohammed Janabi alieleza kuwa katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya
Tano taasisi hiyo imepanua huduma zake na kuboresha huduma za matibabu ya moyo
kwa kiwango cha kimataifa.
“Katika kipindi cha miaka minne
wagonjwa waliopatiwa huduma ni 300,836 ambao walitibiwa na kurudi nyumbani na
wagonjwa 14,960 ambao walilazwa kwa ajili ya kupata matibabu zaidi, na mahitaji
yanazidi kuongezeka hata kutoka katika nchi jiraniani”, Alisema Prof.Janabi.
Alisema kuwa mahitaji ya ujenzi
wa hospitali kubwa ya Mloganzila yanatokana na kuwepo kwa wagonjwa wengi nje ya
nchi ambao wamekuwa wakija kupata matibabu kwa hiyo uwepo wa hospitali hiyo kutaimarisha
utoaji huduma za matibabu ya moyo hapa nchini.
Katika kipindi cha Miaka minne
ya Serikali ya Awamu ya Tano JKCI imeweza kufanya upasuaji mkubwa kwa
kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,537 kwa mafanikio makubwa huku vifo vikiwa ni
asilimia 6 tu sawa na wagonjwa 92 kitu ambacho kinawashawishi nchi jirani kama
Uganda, Rwanda, Malawi, Burundi na Congo DRC kuleta wagonjwa wao kwenye Taasisi
hiyo.
Prof.Janabi alisema kuwa uwepo
wa vifaa vya kisasa na wataalam waliobobea kumewezesha zoezi la upasuaji kuwa
salama, ambapo upasuaji wa moyo kwa njia
ya tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa cathlab
(catheterization), wagonjwa 4,207
walipata huduma hiyo huku vifo vikiwa ni asilimia 1.3 tu sawa na wagonjwa 42.
“Katika kipindi cha miaka minne
huduma za JKCI zimeweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 86 kwa kufanya
upasuaji kwa wagonjwa 5,744 ambao wangeenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na
uwepo wa vifaa vyenye uwezo mkubwa, hususani kwenye masuala ya upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo” Alisema
Prof.Janabi.
Aidha katika kipindi hiki cha
miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, JKCI imeongeza ujuzi wa wataalam ambapo
kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kutoa matibabu ya moyo
yaliyo salama na kwa wagonjwa wengi ikitanguliwa na Afrika ya Kusini
Aliongeza kuwa JKCI imefanikiwa
kufanya upasuaji wa moyo kwa mtoto mdogo mwenye umri wa siku 7 na mzee mwenye
umri wa miaka 101 ambao kwa sasa wagonjwa hao wote wawili wanaendelea vizuri na
maisha yao.
“katika kukabiliana na
changamoto ya idadi kubwa ya wagonjwa, Rais John Magufuli mwezi Januari 2019
alitoa nafasi kwenye jengo la watoto lililopo katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa ajili ya kliniki za watoto tu”, Alisema Prof. Janabi.
Prof.Janabi alisema kuwa JKCI
imenunua mashine mpya mbalimbali za matibabu ya moyo zikiwemo mashine za
kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi, ventilators, cardiac
monitors, test gears, mashine ya X-ray pamoja na vifaa vya chumba cha tatu cha
upasuaji.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) ni hospitali kuu maalum kwa ajili ya matibabu ya moyo inayomilikiwa na
Serikali ambayo ilianzishwa Septemba 2015,ambayo imeendelea kuitangaza vyema
nchi yetu hata katika nje ya mipaka yetu.
No comments:
Post a Comment