Habari za Punde

SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO YA BENKI RUFIJI

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma katika mkutano wa 18 wa Bunge la 11 ulioanza leo.
Na Josephine Majula na Saidina Msangi
Serikali imeahidi kuongeza jitihada za kuanzisha matawi ya benki ya uhakika katika Wilaya ya Rufiji mkoani  Pwani ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za kifedha kwa urahisi.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa aliyetaka kujua ni lini Serikali itapeleka huduma za benki katika Wilaya hiyo.
Mhe. Mchengerwa alisema kuwa wananchi wa Jimbo kongwe nchini wamekuwa wakipata tabu ya kupata huduma za kifedha hali inayowalazimu kusafiri umbali wa Kilometa 100 kufuata huduma hizo.
Akijibu swali hilo, Dkt. Kijaji alisema kuwa wananchi wa Rufiji waendelee kutumia huduma za fedha zilizopo wakati Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu muhimu pamoja na kufanya majadiliano na kuzishawishi benki kuanzisha matawi yao katika Wilaya hiyo.
“Kufuatia mabadiliko ya Sekta ya Fedha nchini ya mwaka 1991, Serikali ilitoa uhuru kwa benki kufanya tafiti za kuamua kuhusu maeneo ya kupeleka huduma za kibenki kulingana na taarifa za utafiti uliofanywa pamoja na vigezo vya benki husika. Kwa kuwa benki zinajiendesha kibiashara maamuzi ya kufungua tawi sehemu yoyote hapa nchini huzingatia vigezo hivyo”,alisisitiza Dkt. Kijaji.
Alisema Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za kifedha hasa zile zinazotolewa maeneo ya karibu na wananchi, itaongea na benki kuona namna ya kupunguza baadhi ya vikwazo vinavyoweza kusababisha gharama za uendeshaji wa shughuli za benki wilayani hapo kuwa juu ili wananchi waweze kupata huduma hizo kwa urahisi.
Alisema kwa sasa wananchi wa Wilaya hiyo wanapata huduma za kifedha kupitia Kituo cha Makusanyo ya Fedha cha NMB (Cash Collection Point - CCP) kilichopo katika Kata ya Utete pamoja na Mawakala wa Benki, hususan Benki ya NMB na CRDB waliopo katika Wilaya ya Rufiji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.