Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Aweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Hospitali Kivunge.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan akikata utepe katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi  Jengo la Huduma za Mama na Mtoto Kivunge Wilaya ya Kaskazini A Unguja. Ikiwa ni shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Na Miza kona Maelezo / Zanzibar 
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutoa umuhimu wa kuziimarisha huduma za mama na mtoto ili kuhakikisha kwamba vifo vinavyotokana na uzazi vinapungua na kumalizika nchini.
Makamu wa Rais ameyasema hayo katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Jengo la Huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazinin Unguja ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyoongozwa na Jemedari Mkuu Marehemu Mzee Abeid Amani Karume serikali ilitangaza matibabu bure kwa wananchi wote bila ya ubaguzi kwa lengo la kujenga msingi wa uwapatikanaji wa huduma za afya nchini.
Mhe. Samia alieleza kuwa sera hiyo ilitia mkazo zaidi katika kutoa kinga hivyo serikali imeweza kusambaza huduma ya afya karibu na wananchi ili kuondosha upungufu wa kwenda masafa marefu kufuata huduma hiyo ambapo kwa sasa takriban vituo 180 vimejengwa ikilinganishwa na mwaka 1964 ambapo vilikuwepo 32.
 Makamu huyo wa Rais alifahamisha kuwa kujengwa kwa jengo hilo la huduma ya mama na mtoto katika Mkoa huo litasaidia kupunguza vifo vya akinama na watoto wakati wa uzazi pamoja na kupunguza msongamano wa wazazi na wagonjwa kupelekwa Hospitali ya Mnazi mmoja.
Mhe. Samia alieleza Wizara ya Afya inatarajia kuongeza nguvu kwa kuleta madaktari bingwa katika hospitali hiyo ili kupunguza matatizo yanayotokana na uzazi pamoja na shida nyengine za kinamama na watoto walio chini ya umri miaka mitano 5.
“Hatufurahii kila mama anaepifika hapa kisu halafu ndio atoke tunafurahi sana mama aweze kujifungue mwenyewe, lakini kuna mambo hayawezi kuepukika lazima huduma hiyo iwepo na kwa bahati mbaya watu wanaohitaji huduma hiyo wanazidi kuongezeka, sababu zinazosababisha kupata upasuaji ni ndoa za umri mdogo hivyo wazee tuache kuwaozesha watoto wakiwa hawajafikia umri”, alisisitiza Mama Samia.
Aidha Makamu huyo aliwataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kutoa mashirikiano na upendo katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa ili kuweza kutoa huduma nzuri na maendeleo katika sekta hiyo
“Natoa wito kwenu watoa huduma za Afya, Madaktari, wauguzi na wataalam wa fani mbalimbali za afya mnaotoa huduma katika Hospitali hii, mfanye kazi zenu huku mkijua kwamba Mungu aliwateuwa nyinyi kuhudumia wanadamu wenzenu, hivyo basi timizeni majukumu yenu kila mmoja kwa fani yake mkiwa na hofu kwa Mungu”, alieleza Mama Samia.
Hata hivyo Mama Samia aliwataka wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini kuilinda na kuienzi Hospitali hiyo pamoja na kufuata taratibu zinazowekwa na uongozi wa hospitali kuwa wavumilivu ili kuweza kupatiwa huduma vizuri na kuepuka migogoro.
Aidha Mama Samia aliisihi jamii kushirikiana na Serikali kupiga vita vitendo vya udhalilishaji, dawa za kulevya na rushwa kwa kutoa ushahidi na kuwafichuwa wale wote wanaofanya vitendo hivyo ili kutokomeza janga hilo na jamii iweze kuishi kwa amani nchi.
Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla alisema kukamilika kwa jengo la Huduma ya Mama na Mtoto kutasaidia kupunguza rufaa za wazazi na wagonjwa kwenda Hospitali ya Mnazi Mmoja na kupunguza msongamano pamoja na kuimarisha ubora na kutanua wingo katika Hospitali hiyo kuongeza majengo kwa kuweka vifaa na wafanyakazi wenye sifa zinazohitajika.
Aidha alisema ujenzi huo pia ni utekelezaji wa agizo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 kuzipandisha hadhi Hospitali za vijiji kuwa za wilaya na za wilaya kuwa za Mkoa pamoja na kutekeleza sera ya afya kuendeleza ustawi wa watu wa Zanzibar kwa kutilia mkazo zaidi uimarishaji wa afya yawanawake, watoto pamoja na makundi yenye mahitaji maalum.  
Jengo hilo lenye ghorofa mbili 2litatoa huduma mbalimbali za mama na mtoto limefahdiliwa na serikali ya Mapindzi na Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Masuala ya Watu Duniani (UNFPA) ambalo litagharimu zaidi bilioni 3 hadi kukamilika kwake. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.