Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Afungua Barabara ya Kiwango cha Lami kutoka Bububu hadi Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikata uteke kuashiria kuifungua barabara ya Bububu hadi Mkokotoni iliyojengwa kwa kiwango cha lami na kampuni ya Ujenzi kutoka Chini ya  (CCECC) (kulia kwa Rais) Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar.Mhe.Dkt, Sira Ubwa na Mwakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya Kanda ya Afrika Mashariki Bw.Zhang Junle na (kushoto kwa Rais) Katibu Mkuu Ndg. Mustafa Aboud Jumbe na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Meneja Mkaazi Bw.Alex,M.Mubiru.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wale wote wanaosingizia demokrasia na kuhakiribu kwa makusudi barabara wakiwemo vijana kuacha mara moja tabia hiyo.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye hafla ya ufunguzi wa Barabara ya Bububu-Mahonda-Mkokotoni yenye urefu wa kilomita 31, hafla iliyofanyika Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wale wote wakiwemo vijana wanaoharibu barabara kwa kusingizia demokrasia kwani hawaijui wala haiitambua demokrasia hiyo hukua akiwataka madereva kujua athari za oil na mafuta barabarani.

Aliwataka vijana kutogombana na barabara na kuwaeleza kuwa wasigombane na kitu kisichosema na kama kuna mtu kawaudhi basi wapambane na huyo aliowaudhi na si barabara na badala yake barabara hiyo waitunze.

Rais Dk. Shein alisema kuwa barabara hiyo ni muhimu sana katika maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini ambapo Wakoloni hawakuona umuhimu wake wakati wakiitawala Zanzibar.

Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kwa makusudi kujenga barabara hiyo ambapo mbali ya barabara wakoloni walidharau kuwapa Wazazibari huduma za afya, elimu ardhi na nyenginezo.

Alieleza kuwa kutokana na hatua hiyo ndipo wazee walipoamua kujitawala wenyewe ili mambo yote yaweze kufanyika kwa maendeleo ya Wazanzibari wote.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi yamefanyika kwa ajili ya kuondosha ubinafsi, umbwannyenye, madhila na dhulma kwa wafanyakazi na wakulima.

Mapinduzi yameikomboa Zanzibar na leo iko huru chini ya chama cha ASP, ambapo kama si Mapinduzi maendeleo hayo yasingelipatikana na kuongeza kuwa maendeleo yameletwa na ASP na leo CCM.

Alisema kuwa mbali ya fedha zilizokopwa na Serikali ya Mapinduziya Zanzibar kutoka Benki ya AfDB zipatazo Bilioni 33.824 pia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa TZS Bilioni 4 katika ujenzi wa barabara hiyo.

Alisema kuwa miaka minane imepita barabara ya Ole- Kengeja haijesha lakini juhudi za makusudi zimechukuliwa katika kuhakikisha barabara hiyo inamalizika ambapo hivi sasa kilomita 20 imeshatiwa lami na kuahidi kuwa barabara hiyo itakwisha na sherehe za ufunguzi zitafanyika.

“Barabara hii iko kama mgongo wa ngisi”,alisisitiza Dk. Shein. Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa barabara hiyo kwa ukumbwa wake na uzuri wake ni namba moja kwani imenawiri sana kwani ina madaraja mengi na yako imara.

Rais Dk. Shein aliipongeza Kampuni iliyojenga barabara hiyo pamoja na kuipongeza Wizara pamoja na uongozi wake wote na wafanyakazi wa Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kutunzwa kwa barabara hiyo.

Alisema kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja ni maarufu kwa ajali za barabarani na kuwataka madereva kutahadhari sana na kuwataka wazee na wazazi kutokaribia barabarani na kutaka watoto waelimishe juu ya athari za barabara pamoja na wale wanaolala barabarani kuacha mchezo huo.

Alilitaka jenshi la Polisi wa barabarani kufanya kazi za ulizni barabarani na kutodharau kazi zao na kutaka waifanye kazi zao kwa heshima kubwa na busara ili kuepuka ajali za barabarani.

Alitoa shukurani kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuikopesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa azma ya kujenga barabara za Unguja na Pemba na kuwataka wananchi kuzitunza barabara zinazojengwa pamoja na miradi mengine inayojengwa na Serikali kwani hizo ni mali za watu wote.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ina mpango wa kujenga mji mpya wa kisasa pamoja na kujengwa kwa soko la kisasa katika eneo la Mkokotoni ambayo itakuwa Mkokotoni mpya na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo.

Mapema Rais Dk. Shein alizindua  barabara hiyo huko katika eneo la Bububu kwa Nyanya sambamba na kukata utembe kuashiria uzinduzi rasmin wa Barabara hiyo ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni na kuwaeleza wananchi walaiohudhuria katika eneo hilo azma ya Serikali ya kumalizia ujenzi wa barabara hiyo kutoka eneo hllo hadi kituo cha Polisi Bububu.

Rais Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa si muda mrefu ujenzi huo utaanza na wajenzi watakaojenga barabara hiyo ni Kampuni iliyojenga barabara ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni Kampuni ya “ China Civil Engineering Construction Corporation” (CCECC).

Pia, Rais Dk. Shein aliwasisitiza wazee na wazazi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo kuhakikisha inawaenga enga vizuri watoto wao katika kutumia barabara hiyo ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alitoa zawadi kwa washindi walioshinda mashindano ya mbio za baskeli zilianzia Bububu kwa Nyanya hadi Mkokotoni ambao miongoni mwao ni Ahmed Simai Tajo Kutoka Dimani, Shukura Mwiga Faki kutoka Chaani na wa tatu ni Khamis Juma Kheir kutoka Dimani ambapo kwa upamnde wa watoto wadogo ni Omar Ibrahim Omar kutoka Kianga, Harith Mbarouk Abdalla kutoka Chaani na wa tatu ni Sheha Abdallah Abubakar kutoka Kianga.

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji  Dk. Sira Ubwa Mamboya  alisema kuwa matokeo mazuri ya ukuaji uchumi yanategemea mambo mengi na moja wapo ni miundombinu imara ya barabara ambayo hupelekea kukua kwa sekta nyingi za kiuchumi ikiwemo biashara, kilimo, utalii na nyengine ambazo ni muhimu kwa uchumi.

Aliongeza kuwa alisema akuwa ujenzi wa barabara hiyo ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha miundombinu ya barabara kwa ajili ya kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji mjini na vijijini.

Alisema kuwa barabara nyingi zilizotajwa katika Ilani ya Uchaguziya mwaka 2015-2020 tayari zimeshajengwa ikiwemo barabara hiyo ambapo alisema kuwa zipo barabara nyengine ambazo zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami Unguja na Pemba ambazo ndani ya mwaka huu wa 2020 zitakamilika.

Akizitaja barabara ambazo zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu kuwani barabara ya Ole hadi Kengeja Pemba, barabara ya Matemwe hadi Muyuni na Fuoni hadi Kombeni.

Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo itapelekea kuongeza kasi ya maendeleo kwa Mkoa wa KaskaziniUnguja na Mikoa mengine ya Zanzibar hali hiyo inatokana na kuwepo kwa huduma bora ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa   mbali mbali sambamba na kukuza sekta ya utalii na kupelekea kuongeza pato laTaifa.

Waziri Dk. Sira alisisitiza kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 ndio Dira ya mafanikio yote hayo hivyo, aliwaomba wananchi wote kwa pamoja kuyaenzi na kuyalinda kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.


Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa  ujenzi wa barabara ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya kujenga ustawi wa wananchi wake kwa kuimarisha na kuendeleza miundombinu ya barabara za mjini na vijijini.

Aidha, alisema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kama ilivyoandikwa kwenye ukurasa wa 139 kupitia Sura ya 88, Dira ya Maendeleo (Vision 2020), MKUZA III, Sera ya Taifa ya Usafiri pamoja na Mpango Mkuu wa Usafiri Zanzibar.

Alisema kuwa mradi huo ulitiwa saini tarehe 8 Novemba 2017 baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji na Mjenzi ambaye ni Kampuni ya ‘China Civil Engineering Construction Corporation’ (CCECC), kwa thamani ya TZS Bilioni 58.617.

Aliongeza kuwa Msimamizi wa Mradi ni Kampuni ya H.P Gauff Ingenieure GmbH ya Ujerumani ambae alifungiana Mkataba na Wizara hiyo tarehe 15 Julai 2017 kwa thamani ya Euro Milioni 1.180.

Kwa maelezo ya Katibu Mkuu huyo Mkataba huo unajumuisha ujenzi wa Barabara hiyo pamoja na ujenzi wa barabara ya Pale-Kiongele yenye kilomita 4.6, Matemwe-Muyuni Kilomita 7.5 na barabara ya Fuoni-Kombeni yenye kilomita 8.56.

Alisema kuwa muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi 24 ikijumuisha muda wa kuleta vifaa ambapo mradi ulianza tarehe 1 Machi 2018 na unatarajiwa kukamilika 29 Februari 2020.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa barabara hiyo ilikuwa katika hali mbaya kutokana kumaliza muda wake na lami iliyokuwepo ilikuwa katika hali mbaya na yenye mashimo kiasi ambacho ilihitaji kujengwa upya na kwa upande wa barabara za Pale-Kiongele, Fuoni-Kombeni na Matemwe-Muyuni zilikuwa barabara za kifusi.

Sambamba na hayo, alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulianza rasmi mwezi wa Juni, 2018 na unatarajiwa kumaliza mwishoni mwa mwezi wa Februari 2020 ambapo ujenzi wake umekamilika kwa kiwango cha lami mwanzoni mwa mwezi Disemba 2019.

Alieleza kuwa gharama za mwanzo zilizotumika kwa ujenzi wa barabara ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni ni TZS Bilioni 28.513. Aidha, Serikali imefidia nyumba na vipando vya wananchi kwa gharama za TZS Bilioni 4.014 ambapo watu 2,255 wamefidiwa ambapo pia,  gharama za kuhamisha huduma za maji ni TZS Milioni 964 na uhamishaji wa miundombinu ya umeme ni Milioni 331 na kufikia Bilioni 33.824.

Alisisitiza haja kwa wananchi kufuata sheria za barabara kwani katika kipindi kifupi cha ujenzi wa barabara hiyo tayari ajali nane zimeshatokea ambazo miongoni mwao zipo zilizosababisha vifo.

Aliongeza kuwa kwa sehemu ya barabara kutoka Bububu Polisi hadi Kwanyanya (Chuini) yenye urefu wa Kilomita 2.8, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji inamalizia taratibu za kumuongezea kazi Mkandarasi huyo wa Kampuni ya (CCECC) ili aijenge sehemu hiyo na kuikamilisha kwa kiwango kilekile na unategeewa ujenzi huo kumaliza kabla ya mwezi Juni 2020.

Kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Katibu Mkuu huyo alitoa shukurani za dhati kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa utekelezaji wa mradi huo wa barabara ya Bububu-Mahonda hadi Mkokotoni.

Nae Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB),  Alex Mubiru alisema kuwa mnamo mwaka 2015 benki hiyo iliidhinisha jumla ya Dola za Kimarekani milioni 350 kwa ajili ya kuimarisha barabara zenye urefu wa kilomita 492 katika barabara za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania moja wapo ikiwa barabara hiyo.

Aidha, alisema kuwa wakati AfDB inaundwa 1994 ilikuwa na ndoto ya ndoto ya Afrika iliyokuwa na uchumi ambapo leo ndoto hiyo imetimiaa kwa upande wa Zanzibar.

Alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni uthibitisho wa azma ya viongozi wa AfDB ambapo kilomita za baraara iliyojengwa, jiwe lililowekwa na madaraja yaliyojengwa ni dhamira ya viongozi wa benki hiyo ambapo leo hii inaona fahari sana katika kupata maendeleo hayo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.