Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Afanya Uhakiki Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akifanyiwa uhakiki kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura alipofika kwenye Kituo chake cha kupiga Kura kilichopo Skuli ya Sekondari ya Kitope.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea Risiti yake  yenye kuthibitisha kwamba tayari ameshafanyia uhakiki kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hapo Skuli ya Kitope Sekondari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpatia Vitambulisho vyake Mkuu wa Kituo cha Kujiandiskisha kwenye Daftari la Wapiga Kura Bibi Jena Ramadhan Mussa katika Kituo chake cha Kujiandikisha cha Skuli ya Sekondari ya Kitope kwa ajili ya kujihakiki.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Nd.Nd. Thabit Idarous Faina akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Skuli ya Sekondari ya Kitope kwa kufanya Uhakiki wa Daftari la Wapiga Kura.
Balozi Seif akizungumza na Vyombo mbali mbali vya Habari nje ya Kituo cha Kujiandikisha Wapiga Kura Wapya na wale wa zamani wanaohakiki majina yao mara baada ya kujihakiki.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi tayari ameshajihakiki katika Daftari la kudumu la Wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC} kujiandaa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae Mwaka huu.
Uhakiki huo ameutekeleza kwenye Kituo chake cha kawaida cha Kupiga Kura kilichopo Skuli ya Sekondari ya Kitope Shehia ya Kitope ndani ya Jimbo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda kupitia Chama cha Mapinduzi {CCM} anayemaliza muda wake wa kuwatumikia Wananchi wa Jimbo hilo  katika Kipindi cha Miaka Mitano tayari ameshatangaza kutogombea tena nafasi hiyo na kuamua kujipumzisha na shughuli za Kisiasa.
Akitoa maoni yake mbele ya vyombo vya Habari mara baada ya kujihakiki kwenye Daftari hilo la  Wapiga Kura Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bado ipo changamoto kwa baadhi ya Wananchi kwa kutokupata Vitambulisho vyao vipya  vya Mzanzibari Mkaazi vinavyowapa fursa ya kufanya uhakiki kwenye Daftari la Wapiga Kura.
Alisema changamoto hiyo imejionyesha kwa baadhi ya Wananchi kutokuwemo majina yao na wengine kuelezwa Majina yao kuwepo Shehia nyengine mambo yanayoleata usumbufu kwao baada ya kuacha shughuli zao za kila siku za kujitafutia maisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya taratibu za kuhakikisha  kwamba kila Mwananchi wa Taifa hili anapata haki yake ya Kidemokrasia ikiwemo ya Kupiga Kura kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi zilizopo.
Balozi Seif  aliiagiza Taasisi inayosimamia Vitambulisho wa Mzanzibari kuitafutia ufumbuzi  changamoto hiyo ili kila Mwananchi mwenye haki ya kupiga Kura anatumia nafasi yake.
Akielezea kuridhika kwake na zoezi la Uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Kituo chake liloanza Alhamisi na Kumalizia Jumatatu ya Tarehe 24 Mwezi huu Balozi Seif Ali Iddi aliwaomba Wananchi wote waliotimiza Sifa za Kujiandikisha Nchini kuitumia nafasi yao ya Kidemokrasia ili kupata fursa sahihi ya kuwachagua Viongozi wao katika Kipindi cha Miaka Mitano inayofuata.
Alisema si vyema wala si busara kupoteza nafasi yao kizembe inayotumia muda mfupi  kwa sababu ya uvivu na visingizio vya kuzongwa na shughuli nyingi za kujitafutia riziki ambazo upo muda, saa na wakati mwingi zaidi wa kuziendeleza.
Zoezi la Uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ndani ya Jimbo la Mahonda limeanza Alhamis ya Tarehe 20 Febuari na kuendelea kwa muda wa Siku Tano hadi Jumatatu ya Tarehe 24 Mwezi huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.