Habari za Punde

KAMATI YA USIMAMIZI MAAFA RUFIJI YATAKIWA KUREJESHA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIKA NA MAFURIKO

Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Mhe.  Juma Njwayo,  misaada,  ikiwa ni magodoro, mikeka, sabuni, vyandarua  na ndoo, kwa ajili ya waathirka wa  maafa ya mafuriko wilayani humo, tarehe 23 Machi, 2020.

Kufuatia miundombinu ya barabara, shule na Zahanati kuathirika kutokana na maafa ya mafuriko wilayani Rufiji. Kamati za Usimamizi wa maafa za wilaya hiyo zimeshauriwa kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na maafa hayo kwa kurejesha hali ya kawaida ya miundombinu iliyoathirika na maafa hayo katika kata zote 13 za wilaya hiyo.

 Kata ya Muhoro na Chumbi ni miongoni mwa kata zilizoathirika sana na maafa hayo, ambapo kwa sasa madaraja matatu yaliyopo barabara ya Nyamwage- Utete inayoelekea makao makuu ya wilaya hiyo tayari yameathirika, Daraja lililopo kwenye barabara ya kuelekea Mradi wa kufua Umeme wa Mwalimu Nyerere nalo limeathirika pamoja na Daraja la Mkapa nalo limeanza kupata athari ya mafuriko hayo.

Akiongea mara baada ya kukagua athari za maafa  na kukabidhi misaada kwa waathirika wa maafa hayo tarehe 23 Machi 2020, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, ameeleza kuwa  Kamati za Usimamizi wa kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya, kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015 zinawajibika kutekeleza operesheni za dharura.

Nimezishauri kamati za usimamizi wa  maafa katika wilaya hii kuwa na mipango ya muda mfupi ya kuhakikisha barabara zinapitika kipindi chote ili wananchi wasishindwe kutumia miundombinu hiyo, kwani zipo barabara zinaunganisha mikoa ya kusini na zipo barabara zinawasaidiia wananchi kuweza kuzifikia huduma za kijamii”amesisitiza Kanali Matamwe.

Awali akiongea mara baada ya kupokea misaada kutoka kwa Idara ya Uratibu wa maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkuu wa wa wilaya hiyo, Mhe.  Juma Njwayo amefafanua kuwa misaada hiyo itakuwa ni msaada mkubwa kwa kuwa hadi sasa wapo watu zaidi ya elfu ishirini wameathirika na maafa hayo kwa kuwa zidi ya nyumba mia moja zimezingirwa na maji.

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutuletea Magodoro, Mikeka, Vyandarua, Ndoo na Sabuni na naamini kamati za maafa zitawajibika kugawa vifaa hivi kwa mujibu wa taratibu za menejimenti ya maafa. Wilaya tunaendelea na kukabiliana  na maafa kwa kaya takribani elfu sita,  kama tulivyoshauriwa kuhusu miundombinu, kwa kushirikiana na TANROADS tunaendelea kwa kasi kuchukua hatua za kurejesha miundombinu yote iliyo athirika ” Amesisitiza  Mhe. Njwayo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameeleza kuwa tangu maafa ya mafuriko yatokee wilayani humo, wamekuwa wakipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Ofisi hiyo,  kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu mwenye dhamana ya masuala ya maafa Mhe. Jenista Mhagama, ambapo amekuwa akiwatuma wataalamu na kufika kwa wakati kwa ajili ya kuzisaidia kamati za usimamizi wa maafa.

“Wananchi wa Rufiji wanafarijika sana kwa jinsi serikali yao inavyowajali, tunatambua mafuriko yamewaathiri sana ikiwemo na kuharibika kwa vyakula vyao, tunaomba  mtuletee mbegu ama chakula cha bei nafuu na wananchi hawataki chakula cha bure, sisi tunataka tufanye kazi na tukipata mbegu tutafanya kazi ya kilimo mara mafuriko yakiisha” amesisitiza , Mhe. Mchengerwa.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Mamlaka ya Hali hewa iliyotolewa mwezi Februari mwaka huu imeeleza kuwa kutakuwa na mvua za juu ya wastani katika eneo kubwa la nchi kati ya mwezi Machi hadi mwezi Mei, mwak huu, ambapo mvu ahizo zilitarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi Machi na kutaraji akumaliziaka kati ya wiki ya kwanza au ya pili yamwezi Mei. Hivyo kutokana na mvua hizo wananchi hawanbudi kuchukua tahadhari za athari za mvua hizo.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa kukakagua maeneo yaliyoathirika na maafa ya mafuriko katika kata ya Muhoro kijiji cha Shela tarehe 23 Machi, 2020, takribani  Watu elfu ishirini wameathirika  na maafa hayo.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Muhoro, kijiji cha shela wilayani Rufiji wakishuka kwenye mtumbwi wanaoutumia kuvuka na kuyafikia makazi yao baada ya barabara kujaa maji kutokana na athari ya maafa ya mafuriko. Miundombinu ya barabara , shule na zahanati katika wilaya hiyo imeathirika na maafa hayo.
Baadhi ya misaada kwa ajili ya waathirika wa maafa ya  mafuriko wilayani Rufiji, ikiwa imepelekwa wilayani humo tarehe 23 Machi, 2020, ambapo misaada  hiyo ni  magodoro, mikeka, vyandarua, sabuni na ndoo. Takribani kaya elf sita zinakadiriwa kuathirika na maafa hayo.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akiandika taarifa alizokuwa akielezwa na  Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa huku akimulikiwa kwa kutumia tochi ya simu wakati giza lilipotanda wakati wakiendelea na shughuli ya  kukakagua maeneo yaliyoathirika na maafa ya mafuriko katika kata za Muhoro  na Chumbi tarehe 23 Machi, 2020. Kata hizo ni kata zilizoathirika sana kati ya kata zote 13 za  wilaya hiyo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.