Habari za Punde

MAJALIWA:TUMEUNDA KAMATI TATU KUKABILIANA NA CORONA


Na.Khadija Mussa. OWM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi ya corona (COVID-19).

 

Ameunda kamati hizo leo (Jumatatu, Machi 23, 2020) na kuzitangaza katika Kikao Kazi cha Mawaziri na Makatibu Wakuu kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.

 

Kamati hizo ni ya Kitaifa ambayo itaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

 

Wengine ni Waziri Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

Pia, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

Amesema pamoja na mambo mengine, kamati hiyo ya Kitaifa itakuwa na jukumu la kuufahamisha umma hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na homa ya kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19)

 

Kamati ya pili ni ya Makatibu Wakuu ambayo itaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na itahusisha Makatibu Wakuu kutoka sekta husika ambapo itakuwa na jukumu la kufanya tathmini ya hali ilivyo na kutoa ushauri kwa Serikali.

 

Amesema kamati ya tatu ni ya Kikosi Kazi cha Taifa ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huku wajumbe wake wakiwa ni wataalamu akiwemo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Jukumu la kamati hiyo ni kuishauri kamati ya Makatibu Wakuu.

 

Pia, Waziri Mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona. 

 

Imeelezwa kuwa kinga dhidi ya virusi vya corona liwe ni jambo la kimkakati zaidi kuliko kusubiri kutibu, hivyo kwa sasa Serikali imeweka mkazo kwenye kuwahamasisha wananchi kujikinga na virusi hivyo.
IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 - DODOMA

JUMATATU, MACHI 23, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.