Habari za Punde

Taarifa Kwa Umma Mahakama Kuu Zanzibar Kusitishwa Usikilizaji wa Kesi Zote Kwa Muda wa Siku 30.

Na Mwajuma Juma, Zanzibar.
MAHAKAMA Kuu Zanzibar imetangaza kusitisha usikilizwaji wa kesi zote kwa muda wa siku 30 kuanzia Machi 26 mwaka huu hadi April 24 mwaka huu.
Hatua hiyo ambayo inahusu mahakama zote za Zanzibar  inafanyika ikiwa ni moja ya kukinga na kupunguza maambukizi ya virusi vya CORONA COVID 19 kwa mahakama, hatua ambayo inaenda sambasamba na maelekezo ya Serikali za Zanzibar ya Machi 17 mwaka huu, juu ya kujikinga na kupunguza kuenea kwa virusi hivyo hapa Zanzibar.
Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman  Makungu, Mrajisi wa Mahakama hiyo Mohamed Ali Mohamed alisema kuwa kwa kesi ambazo ziko katika hatua ya kusikilizwa ‘Submission’ mahakama husika itawashauri mawakili au wenye kesi kuwasikilisha kwa maandishi.
Mohamed alisema  mahakama kwa sasa zitakuwa zinashughulikia kesi za dharura na washitakiwa wenye kesi nzito na maombi ya dhamana, ambapo muombaji na wakili wake au kwa ombi la dhamna wadhamini ndio watakaoruhusiwa kuingia mahakamani.
Aidha alifhamisha kwamba kwa makosa yenye dhamana majaji na mahakimu wanatakiwa kutoa dhamana yenye masharti nafuu, ili kupunguza mrundikano katika vyuo vya mafunzo.
Kwa makosa madogo madogo kama ya wizi wa kuku, ndizi, hizi Polisi wajitahidi kuzimalizia vituoni”, alisema.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na zuio hilo lakini katika kipindi hichi watendaji wote wa mahakama wataendelea kuwepo kazini na kumbi za mahakama hazitatumika.
“Kwa majaji na mahakimu wenye hukumu na maamuzi watatumia kipindi hichi katika kuzikamilisha.
Sambamba na hilo alisema kuwa zaidi ya muongozo ambao umetolewa hapo juu na hatua nyengine za kinga zitawekwa na kusema kuwa muongozo huo unaweza kurekebishwa wakati wowote kufuatana na maelekezo yatakayotolewa na Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.