Habari za Punde

UNODC Yaipongeza Tanzania Kudhibiti Dawa za Kulevya

Na. Erick Msuya -MAELEZO DAR ES SALAAM 12.3.2020
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kupitia kamisheni ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya limeipongeza Tanzania kwa jitihada madhubuti za kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa taarifa inasema, juhudi hizo  zimeleta matokeo chanya katika mapambano ya dawa za kulevya duniani katika kipindi cha miaka  mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Vyombo vya Habari kuelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini katika kupambana na kudhibiti dawa za kulevya.

“Katika mkutano wa 63 wa Kamisheni ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (CND 63) uliofanyika Nchini Austria, ni Mkuu wa shirika la UNODC alitupongeza Tanzania kuwa ni moja kati ya nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kupunguza upatikanaji na uhitaji wa dawa za kulevya, na kuweza kutekeleza mikakati minne ya kupambana na tatizo la dawa za kulevya kwa uwiano ulio sawa“ alisema Kamishna Haji.

Alisema mafaniko hayo yamekuja kutokana na juhudi za serikali ya Tanzania katika kufanya marekebisho makubwa ya kisheria, ikiwemo kutungwa kwa Sheria Na. 5 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 na mabadiliko yake ya mwaka 2017 kwa Tanzania bara, na kwa upande wa Zanzibar  ambako mabadiliko ya sheria yalifanyika mwaka 2019.

Aidha Kamishna  Haji aliwataka waandishi wa habari kutoa taarifa za uhakika juu ya takwimu za kupambana na kudhibiti dawa za kulevya  nchini, kwani pasipo kufanya hivyo kwa kutoa takwimu za uongo kutasabisha hofu na taharuki katika jamii na kuchafua taswira ya  Tanzania.

“Pamoja na mafanikio hayo makubwa, bado tuna masikitiko makubwa kwa baadhi ya magazeti wanaichafua nchi yetu kwa kuandika habari zisizo sahihi kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya niwaombe kuwa makini katika uandishi wa habari na ni vyema kutumia vyanzo vya uhakika na kuzingatia maadili ya Uandishi” alisema Kamishna Haji

Baadhi ya Mgazeti hayo ni pamoja na gazeti la The East African la Nchini Kenya katika toleo lake Na. 1323 la tarehe 07-13 Nachi 2020 na gazeti la Kimtandao la The Citizen la Tarehe 8 Machi 2020 yaliandika  Tanzania ni Kitovu cha Dawa za Kulevya Afrika Mashariki.

Aidha Kamishna Haji amewataka Watanzania kuendelea kujivunia kwa mafanikio hayo yaliyopatikana na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano wa kuigwa katika mataifa ya Uganda, Msumbiji, Ghana, Nigeria na Norway ambazo zilliomba kujifunza  mfumo wa utendaji kazi na sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa kulevya ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.