Habari za Punde

Waandishi wa Habari Zanzibar Wapata Mafunzo ya Corona

 
Mkufunzi kutoka kitengo cha Kuratibu,kufuatilia na kudhibiti Maradhi Wizara ya Afya Asha Ussi Khamis akitoa mada ya kinga na kudhibi Maradhi katika Mafunzo kwa Waandhishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali kuhusiana na maradhi ya Korona Chanzo chake na Dalili zake ili kuweza kutoa habari sahihi kwa Wananchi hafla iliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini Zanzibar.
Mkuu wa kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar Halima Ali Khamis akitoa mada ya Uvumi  katika Mafunzo kwa Waandhishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali kuhusiana na maradhi ya Korona Chanzo chake na Dalili zake ili kuweza kutoa habari sahihi kwa Wananchi hafla iliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa habari kutoka Vyombo mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika mafunzo hayo. 
Picha na Yussuf Simai -Maelezo Zanzibar.

Na Khadija Khamis  -  Maelezo  Zanzibar 10/03/2020.
Meneja wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Udhibiti wa Maradhi ya Mripuko Asha Ussi Khamis amesema virusi vipya vya Corona (Novel Coronavirus) huambukiza kwa muda mfupi na kuenea kwa haraka katika mataifa mbali mbali duniani.
Amesema serikali inachukuwa juhudi kubwa kudhibiti ugonjwa huo ili usiingie nchini kwa kuwahakiki wageni wanaokuja kupitia katika viwanja vya ndege na bandari .
Meneja huyo  aliyasema hayo katika Ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu  wa Serikali Mazizini wakati akitoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali kuhusu Mripuko wa Maradhi ya Virusi vya Corona.
Alisema ugonjwa huo wa mripuko ambao umeenea katika mataifa mengi duniani ni vyema jamii kuchukua tahadhari.
Alieleza kuwa maradhi hayo kwa Zanzibar hayapo hivyo aliitaka jamii kuchukua tahadhari ya kuudhibiti kutokana na ugonjwa huo huenea kwa uingiaji wa wageni ambao hutokea katika  nchi zilizopata maambukizo.
“Lazima wananchi tuendelee kuweka mazingira katika hali ya usafi kuwa na utamaduni wa kunawa mikono kwa sabuni mara kwa mara kwani wadudu hao huimarika sehamu za baridi na huathiri zaidi binaadamu na wanyama na dalili zake kuzidi kwa joto kali mwilini, huziba mirija ya pumzi pamoja na kushambulia mapafu’’, alisema Meneja huyo .
Nae Meneja wa elimu ya Afya Halima Ali Khamis alisisitiza kuwa maradhi hayo ni hatari ambao yamekuwa yakisambaa kila siku katika nchi mbali mbali hivyo jamiii iache uvumi katika mitandao ya jamii ili kuondoa hofu kwa wananchi.
“Kumekuwa na tuhuma mbalimbali ambazo huenezwa kupitia mitandao ya kijamii kufanya hivyo kutapelekea kuwatia hofu wananchi kwa taarifa ambazo sio sahihi“, alisema Meneja Halima .
Alifahamisha kuwa taarifa ya maendeleo ya ugonjwa huo hutolewa na Mamlaka husika kutoka Serikalini hivyo si vyema wananchi kutoa taarifa za upotoshaji kwa umma.
Aidha alieleza kuwa Serikali tayari imeshatenga maeneo mbali mbali ya dharura kwa lengo la kudhibiti maambukizi pindiko atagundulika mgonjwa ana dalili ya maradhi ya virisi vya corona.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.