Waziri
wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari(Hawapo pichani), kuhusu mlipuko wa
ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19) kwa Nchi za SADC katika Mkutano wa
Dharura uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam Tanzania.
Waziri wa Afya kutoka Zimbabwe, Dkt. Obadiah Moyo
akifafanua jambo kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19) kwa
Nchi za SADC katika Mkutano wa Dharura uliofanyika katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Tanzania.
Katibu
Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi
za Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt.Stergomena Tax akisoma Taarifa ya Mkutano wa
dharura wa Mawaziri wa Afya wa SADC
kuhusu kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Virusi vya Corona ulifanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam
Tanzania.
Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC), imesema imejiandaa kikamilifu kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Virusi
vya Corona (Covid-19) ambao umezidi kusambaa duniani na kwamba mikakati madhubuti
imeweka tayari kwa kutoa elimu ya kutosha jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo kwa
wananchi wa ukanda huo wa Afrika.
Akizungumza katika Mkutano wa dharura uliofanyika
Jijini Dar es Salaam, ambao uliitishwa kujadili hali ya mlipuko wa ugonjwa huo
uliohudhuriwa na nchi 10 kati ya 16 za ukanda wa Kusini mwa Afrika, zikiwemo
Angola, Congo DRC, Lethoto, Mauritius, Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe, Zambia
Namibia na Tanzania, Waziri mwenye dhamana ya Afya kutoka Tanzania, Mhe. Ummy
Mwalimu alisema kuwa tayari nchi hizo zimefanya maandalizi na sasa zimeingia
kwenye hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Tupo hapa leo kujadili hali ya mlipuko wa ugonjwa wa
Corona (Covid -19), ambao sisi kama nchi wanachama tumekuja kubadilishana
taarifa kuhusiana na ugonjwa huu na kuona kama nchi za SADC tumejipanga
kukabiliana nao na sasa imeonesha kuwepo na hali ya utayari kwa kila nchi
mwanachama”, Alisema Ummy Mwalimu.
Alibainisha kuwa kati ya Nchi 16 za SADC ni nchi moja
tu ambayo mpaka sasa imebainika kuwa na washukiwa wa ugonjwa huo ambayo ni
Afrika ya Kusini na nchi zingine ziko salama, lakini walikubaliana kuwa nchi
hizo zianzisha utaratibu wa kujipima na kujitathmini badala ya kusubiri
tathmini za wadau wa afya.
Katika Mkutano huo, Waziri Ummy alisema nchi hizo
zilifikia makubaliano mbalimbali katika kukabili ugonjwa huo ikiwemo hilo la
kujitathmini wenyewe, kushirikisha sekta nyingine kama Utalii, Uchumi, fedha
pamoja na Uhamiaji, kutoa ushauri kwa Baraza la Mawaziri wa SADC kutofanya
mikutano ya ana kwa ana badala yake njia nyingine zitumike kama vile video conference.
Aidha aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China
kuweza kupambana na ugonjwa huo kwani mpaka Machi 9, 2020 kumekuwepo na
mabadiliko makubwa ambapo maambukiza mapya yamepungua na kufikia watu 28 tu.
“Ninawashukuru Serikali ya China kwa kudhibiti ugonjwa
huu kwani mpaka leo China ina wagonjwa wapya 28 hali hii inaonesha jinsi gani
wenzetu wameweza kupambana kwa kiasi kikubwa kwa hiyo sisi kama nchi za SADC
tumejipanga kukabiliana na Corona (Covid
-19)”, Alisema Waziri Ummy.
Kwa upande wa Tanzania mpaka sasa hakuna mgonjwa
yeyote wa Corona (Covid 19), lakini Serikali imejiandaa kwa kiasi kikubwa kwa
kutenga maeneo iwapo ya kuwatibu iwapo
wagonjwa hao watapatikana na kwa sasa inajenga eneo la kudumu katika Hospitali
ya Mloganzila Jijini Dar es Salaam.
Katika sehemu za kusafiria na kupokea wageni na mizigo
ikiwemo Viwanja vya ndege, bandari na
maeneo ya mipakani Serikali imeweka vipima joto vya kutambua ugonjwa huo.
Naye Waziri wa Afya kutoka Zimbabwe, Mhe.Dkt. Obadiah
Moyo, alisema kuwa Nchi za SADC hususani nchini kwake zimejiandaa kukabiliana
na ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wake jinsi ya kujikinga
na kuepukana nao.
“Tutatoa elimu ya uelewa kwa wananchi wetu kwani elimu
hiyo ni muhimu sana kujikinga na ugonjwa huu na tutahakikisha kwamba
tunashirikiana na kushirikishana kama nchi za ukanda huu ili kuzuia kusambaa
kwa ugonjwa huu katika nchi nyingine za ukanda huu”, Alisema Waziri Moyo.
Aidha katika kuwatambua wanafunzi wa Nchi za Kusini Mwa Afrika walioko China,
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka
Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro alisema
kuwa mpaka sasa wanafunzi hao kutoka nchi za SADC wako salama na hakuna
aliyeambikizwa.
“Wanafunzi wa SADC walioko China wako salama kabisa
hakuna mwanafunzi yeyote aliyeambukizwa ugonjwa huo, lakini tunataka nchi zetu
za SADC zibaki salama tunatakiwa kupata elimu na kuelewa tunachofundishwa
kuhusiana na ugonjwa huu”, Alibainisha Dkt.Ndumbaro.
aliendelea kusema kuwa Dkt.Ndumbaro kuwa Vyombo vya
habari ni wadau wakubwa katika kutoa taarifa sahihi kuhusiana na ugonjwa huo,
hivyo vinatakiwa kushirikiana na mamlaka husika za afya ili kupata taarifa
sahihi ambazo zitawatoa hofu wananchi katika ukanda huo wa Afrika.
No comments:
Post a Comment