Habari za Punde

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed Atowa Taarifa kwa Umma Kuhusiana na Maradhi ya Corona

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed akizungumza na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali viliokoJijini Zanzibar akitowa Taarifa kwa Umma kuhusiana na maradhi ya Corona, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar. 

Na Mwashungi Tahir -Maelezo Zanzibar. 19-3-2020.
WAZIRI wa Afya Zazibar Mhe.Hamad Rashid Mohamed amesema Serikali inachukua hatua ya kufunga skuli zote ikiwemo maandalizi , msingi , sekondari pamoja na vyuo vyote ikiwemo na madrasa kwa lengo la kupunguza uwezekano wa maambukizi ya maradhi ya corona .
A kitoa taarifa kwa umma huko kwenye Ukumbi wa Idrissa Abdul Wakil ulioko  Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu taarifa za uingiaji maradhi ya virusi vya corona kuingia nchini.
Amesema Skuli hizo pamoja na madrasa zitafungwa hadi Serikali itapotoa tangazo jengine na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu na kufuata miongozo inayotolewa na wataalamu wa afya juu ya njia bora za kujikinga na ugonjwa huo ambao tayari umeshaingia nchini.
Aidha amesema Serikali inazuwia mikusanyiko yote inayokutanisha watu wengi kwa wakati mmoja ikiwemo mikutano, makongamano, semina, warsha , michezo ya ligi kuu , harusi na burudani za ngoma mpaka hali ya maradhi itakapotengemaa.
Hivyo amesema  utaratibu wa maziko  utatolewa na viongozi wa taasisi za dini na kutowa wito shughuli za maziko zisihisishe watu wengi.
“Natoa wito kuhusu shughuli za maziko zihusishe watu wachache ili kujilinda na janga hili la Taifa katika mkushanyiko utakafanyika”alisema Waziri Hamad.
Pia amesema Serikali inawataka watu wote wanaoingia nchini kutoka nchi zilizoathirika na maradhi hayo kufuata utaratibu wa kujitenga kwa hiyari kwa muda wa siku 14 kwa gharama zao wenyewe pamoja na kufuata masharti ya afya.
Hata hivyo Waziri Hamadi aliwataka wananchi kuondoa hofu na kuwataka kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji ya kutiririka na sabuni za kunawia mikono.
Pia amewataka kuziba pua na mdomo kwa kitambaa  tishuu au kujiziba kwa mkono  pindi mtu akenda chafya  au kukohoa  na kupenga mafua  na kuiomba jamii kutoa taarifa kwa mtu yeyote atakaebainika na dalili za maambukizi ya maradhi hayo kwa wataalamu wa afya.
Amesema hapa Zanzibar wamegundulika washukiwa watatu wa ugonjwa huo wawili wakiwa ni raia wa kigeni ambao mmoja ni Mghana na Majerumani na mmoja ni Mtanzania .
Amefahamisha mtu huyo kutoka Ghana ni mwanamke mwenye umri wa miaka 24 ambaye aliingia nchini akitokea Ujerumani na sasa amelazwa katika kituo maalum kilichotengwa kwa ajili ya maradhi hayo huko Kidimni Wilaya ya Kati Unguja kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Ali Salim Ali ameitaka jamii kuacha kurundikana katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na badala yake kuvitumia vituo vyengine vya Afya.
Amewataka wagonjwa kwenda katika vituo vidogo vidogo vya afya kwani wataalamu wapo wa kutosha na huduma zinapatikana za uhakika kwani  kuepuka mrundikano kutaweza kuepuka  maambukizi ya maradhi ya virusi vya korona ambavyo hivi sasa vimeshamiri nchi mbali mbali duniani. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.