Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akiwasili ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa
mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kikazi kukagua kukagua athari
zilizosababishwa na korongo kubwa kando ya Mto Shaban Robert mwishoni mwa wiki.
Na.robert hokororo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu mwishoni mwa wiki amefanya ziara ya kikazi wilayani
Mpwapwa mkoani Dodoma kukagua athari zilizosababishwa na korongo kubwa kando ya
Mto Shaban Robert.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo aliagiza Baraza la Taifa
la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya haraka kupata
ufumbuzi wa tatizo hilo ili kunusuru wananchi kuzingirwa na maji yanayojaa
katika mto huo.
Waziri Zungu alisema pamoja na hayo Serikali kupitia
Ofisi yake imeichukua changamoto hiyo na kuahidi kukaa na wataalamu wa
mazingira kuanza utekelezaji wake.
"Athari hii sio ndogo ni kubwa na inahitaji uangalifu
mkubwa katika kuitatua kwani kila siku maji yanaongezeka katika mto huu, pia
sisi kama Serikali tumetenga fedha za kukabiliana na maafa kama kupitia mifuko
ya kitaifa na ya kimataifa hivyo tutazama tuone nini tunafanya," alisema.
Aidha Waziri Zungu aliwataka wananchi kuendelea kushiriki
katika suala zima la uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti na kuitunza
ili kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa shughuli za binadamu zinachangia kwa kiasi
kikubwa kwa matatizo hayo ambayo yamewaletea madhara ikiwemo kukatika kwa
mawasiliano baina ya eneo moja hadi lingine baada ya madaraja kusombwa na maji
ya mto yaliyofurika isivyo kawaida.
Pia waziri huyo aliwaahidi wananchi kuwasiliana na Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma kufahamu wana mkakati gani
katika kurudisha mawasiliano ya daraja lililosombwa na maji.
"Ombi langu kwenu muendele kulinda mazingira kwani
tukiharibu mazingira watoto wetu watateseka na dini zote zimesisitiza kulinda
mazingira. Pia tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atunusuru na janga hili la
Corona ili Taifa letu liendelee na shughuli za kawaida na pia tuendelee
kujikinga kama wanavyoelekeza wataalamu wa afya," alisisitiza.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mhe. George
Lubeleje aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutenga fedha
kiasi cha sh. bilioni 17.4 kwa ajili ya wilaya tano ikiwemo Mpwapwa kutekeleza
miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbunge huyo aliwaomba wananchi kuacha kufyeka na kuchoma
miti kwa ajili ya mkaa hususan katika maeneo ya milima kwa kuwa hatua hiyo
inasababisha kuharibiwa kwa vyanzo ya maji.
Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA)
Wilaya ya Mpwapwa, Emmanuel Lukumay aliahidi kuwa watafanyia kazi changamoto
hiyo kunusuru eneo la korongo kwa kutenga sh. milioni 457 kwa ajili ya kujenga
daraja la kudumu.
Lukumay alibainisha kuwa daraja hilo lililojengwa zaidi
ya miaka 60 iliyopita na kusombwa na maji hivi karibuni lilikuwa ni kiungo
muhimu kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Aliongeza kuwa TARURA daraja liko chini ya mradi wa barabara
ya lami iliyoanza kujengwa katika wilaya hiyo na kusema kuwa tayari wameomba
fedha kwa ajili ya kulijenga.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akipewa maelekezo na Mkuu wa Wilaya ya
Mpwapwa mkoani Dodoma Jabir Shekimweri kuhusu namna korongo lililopo katika Mto
Shaban Robert linavyoathiri wakazi wa eneo hilo wakati aliponya ziara ya kikazi
wilayani humo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia) akiangalia athari za
kimazingira zilizosababisha kukatika kwa mawasiliano baada ya daraja la Mto
Shaban Robert wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kusombwa na maji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia) akizungumza na wananchi wa
Kata ya Mpwapwa Mjini alipofanya ziara ya kikazi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma
kujionea na kusikiliza changamoto za kimazingira zinazosababishwa na korongo
lililopo kwenye Mto Shaban Robert.
Sehemu ya korongo kwenye mto Shaban Robert wilayani
Mpwapwa mkoania Dodoma ambalo limeleta athari kwa wananchi wa eneo hilo pindi
mvua inaponyesha na kusababisha maji kuzingira makazi.
Sehemu ya nyumba za wakazi wa eneo la Kata ya Mpwapwa
Mjijni wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma ikiwa imezingirwa na maji hatua
liyosababisha baadhi ya nyumba kubomoka kufuatia korongo lilipo katika Mto
Shaban Robert.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
No comments:
Post a Comment