Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akitoa Salamu za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Pia aliwatakia waislamu wote mfungo mwema wa Mwezi huu wa Ramadhani kwa kufanya ibada mbali mbali ikiwemo sadaka na zaka na mengineyo pia kuondokana na mikusanyiko isiyofaa kuyaepuka maradhi yaliyoingia Duniani kote na kufuatana maelekezo yanayotolewa na Viongozi wao pamoja na kujihifadhi na kuyashinda mambo mbali mbali yanayobatilisha funga kwa ujumla.
WAFANYABIASHARA wote wametakiwa kuendesha biashara zao kwa uadilifu na huruma na kamwe wasitumie sababu ya kuwepo kwa janga la maradhi ya COVID 19 kwa kuwawekea mazingira magumu wananchi katika kuwauzia bidhaa kwa bei kubwa hasa katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhanii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj
Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika risala ya Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni utaratibu wake
aliuoweka kila ukikaribia mwezi huo Mtukufu kila mwaka.
Katika risala yake hiyo Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kuwapongeza wafanyabiashara kwa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha
kwamba bidhaa zote muhimu hasa za chakula zinapatikana kama kawaida tangu
yalipoingia maradhi hayo na kueleza matumaini yake kwamba hali hiyo itaendelea
katika mwezi wa Ramadhani na miezi mengine inayokuja.
Alhaj Dk. Shein aliwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu
kumkumbuka sana Mwenyezi Mungu na kumgtukuza pamoja na kusoma dua mbali mbali
katika funga na sala zao za faradhi na
sunna katika mwezi wa Ramadhani na miezi mingene ili kuzidi kupata rehema na
ulinzi wake.
Aliwaeleza wananchi kuwa mwaka huu wa 2020 mwezi Mtukufu wa
Ramadhani unakaribishwa huku kukiwa na mtihani wa maradhi yanayosababishwa na
virusi vya Korona vinavyojulikana kwa jina la COVID 19.
Alhaj Dk. Shein alisisitiza kuwa miongoni mwa mambo muhimu
katika mapambano dhidi ya COVID 19 ni kujiepusha na mkusanyiko wa watu ingawa
suala hilo limekuwa changamoto kubwa lakini ni lazima litekelezwe kwa sababu
mikusanyiko ndio njia mojawapo inayosababisha maambukizo.
Aliwanasihi wananchi kuepuka mikusanyiko na kuukubali
ushauri na nasaha wanazopewa kwa ajili ya kuudhibiti ugonjwa huo katika familia
na jamii kwa jumla.
Hivyo, Rais Dk. Shein amewagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya
pamoja na Masheha wahakikishe kwamba katika maeneo yao ya utawala wanavidhibiti
vitendo vyote vinavyoweza kuathiri juhudi na mipango ya Serikali katika
kupambana na maradhi hayo ikiwemo mikusanyiko ya watu.
Kwa kutilia mkazo suala hilo Rais Dk. Shein amewataka
viongozi hao wasichelee kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayejaribu
kwenda kinyume na miongozo iliyotolewa na Serikali katika kupambana na maradhi
hayo.
Aidha, Alhaj Dk.Shein aliwanasihi wananchi wote
wasisikilize taarifa zisizo rasmi wanazozitoa watu wasiohusika ambao hawana
mamlaka ya Kiserikali ya kutangaza taarifa za Serikali.
Aliongeza kuwa Serikali inafuatilia kwa karibu sana na kwa
umakini mwenendo wa maradhi hayo nchini na tukio lolote linalohusu ugonjwa huo
hapa nchini na matukio mengine yatatolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa wakati.
Alieleza kuwa hadi tarehe 22 Aprili, 2020 jumla ya wagonjwa
83 wameripotiwa kati yao watatu wamefariki na wane wamepona na wameruhusiwa
kurudi nyumbani huku akisisitiza kuwa kazi ya kutoa taarifa itaendelezwa na
Wizara ya Afya kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza mambo matatu muhimu
ambayo yanapaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na kuyafuata na kuyatekeleza
maelekezo ya madaktari na wataalamu wa afya kutokana na yote yanayoelekezwa
kuhusu ugonjwa unaosababishwa na COVID-19.
Pia, alisisitiza haja ya kuyasikiliza na kuyatii kwa
ukamilifu maelekezo yanayotolewa na viongozi mbali mbali wa Serikali, viongozi
wa dini na wengineo kwenye jamii.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwataka wananchi
kuendeleza utamaduni uliojengeka miaka mingi kwa wananchi kuchangia huduma za
jamii ili lengo la kupambana na maradhi hayo liweze kufanikiwa.
Hivyo ilivyokuwa janga hilo ni tatizo la watu wote anaamini
kwamba wananchi watakuwa tayari kuchangia juhudi za Serikali katika Mfuko
Maalum wa kukabiliana na COVID 19, ulioanzishwa tarehe 4 Aprili, 2020.
Aliongeza kuwa Mfuko huo utasimamiwa na Wizara ya Fedha na
Mipango na Akauti mbili tayari zimeshafunguliwa kwenye Benki ya Watu wa
Zanzibar (PBZ), ambapo namba yake ya Akauti alizitaja kuwa ni 0748946001 na ile
ya benki ya CRDB ambayo ni 0150485100.
Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa waliothibitika
kuambukizwa na maradhi hayo Serikali imelazimika iongeze nguvu na uwezo katika
kuyafuatiliya, kuyashughulikia na kuyadhibiti maradhi hayo.
Hivyo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea
kutimiza wajibu wake na kuongoza mapambano dhidi ya maradhi hayo ambayo
yanahitaji mchango wa kila mmoja. “Tukishirikiana sote kwa umoja wetu na kila
mmoja akitimiza wajibu wake bila ya shaka tutafanikiwa kuyashinda maradhi
haya”, alisema Alhaj Dk. Shein.
Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote
kutowanyanyapaa wale ambao waliugua maradhi ya COVID 19.
“Wakishathibitishwa na madaktari na wataalamu wetu wa afya
kwamba wamepona na kuruhusiwa warudi kwenye makaazi yao ya kawaida ni wajibu
wetu tushirikiane nao na tuwape moyo na maneno ya faraja ili waweze kuyakabili
maisha yao ya ykila siku na shughuli zao bila ya kuwanyanyapaa”,alisema Alhaj
Dk. Shein.
“Nasema haya kwa sababu hawa ni wananchi wenzetu na ni ndugu zetu lazima tuwathamini. Inshaallah,
tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu awape nafuu na maisha bora”,aliongeza Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwatakia wananchi wote kheri na
Baraka za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na
uwezo wa kuendeleza ibada za saumu na ibada nyengine zote katika Mwezi wa
Ramadhani na miezi ijayo.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi
kuendelea kufanya kazi kwa kasi zaidi na kwa bidii ili kupunguza athari za
janga la COVID 19 ikiwa ni pamoja na kuzitumia mvua za
masika zilizokwishaanza katika kuimarisha
kilimo cha mazao mbali mbali ili kuweza kukidhi mahitaji ya chakula.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment