RADIO Jamii iliyopo Micheweni Pemba imepongezwa kwa mchango
wake mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii juu ya tahadhari ya ugonjwa unaosababishwa
na virusi vya Corona kisiwani humo.
Pongezi hizo
zimetolewa wakati viongozi wa Mikoa miwili ya Pemba walipokutana na na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein huko Ikulu ndogo,
Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Akisoma taarifa ya
Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkuu wa Mkoa huo Omar Khamis Othman alisema kuwa Redio
Jamii iliyopo Micheweni imeweza kutoa vipindi mbali mbali ikiwa ni pamoja na
uvaaji wa barakoa, umuhimu wa kunawa maji tiririka na sabuni kama njia ya
kujihadhari na ugonjwa huo.
Kiongozi huyo alieleza
kuwa jumla ya wananchi 7,689 wananoishi maeneo ya kisiwa cha Fundo, Kokoa,
Njau, Kojani, Makangale,Kifundi, Msuka, Micheweni, Shanake na Kiuyu kwa Manda,
Tondooni, Tumbe, Shumba Mjini, Maziwa Ngombe, Michenzani, Kiuyu Mbuyuni
wamepata elimu ya kuelewa ugonjwa wa Corona na hatua za kujikinga na ugonjwa
huo.
Alieleza kuwa redio
hiyo imeweza kusaidia jitihada hizo za kutoa elimu katika maeneo hayo yakiwemo
yale ya visiwa na maeneo mengineyo ikiwa ni pamoja na kueleza katika vipindi
vyake juu ya umuhimu wa kutoa taarifa pale wanapogundua kuna mtu ama watu
wameingia kutoka nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa huo
alieleza kuwa elimu iliyolenga kuutambua ugonjwa wa Corona na mbinu zote muhimu
za kujikinga na ugonjwa huo imetolewa kupitia mikutano ya jamii kwa Shehia 61
za Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Aidha, aliongeza kuwa
elimu kwa wachuuzi na wanunuzi wa samaki 2,651 ilitolewa katika Shehia nne
ambazo zina bandari za kuuzia samaki ikiwemo Msuka, Kiuyu, Shumba Mjini, Wete,
Mtambwe, Gando na Tumbe.
Vile vile, Mkuu wa
Mkoa huyo alieleza kuwa Mkoa huo umetoa elimu kwa makundi tofauti wakiwemo
Maimamu, Mashehe, Watu maarufu, Madalali na Kamati za afya za Shehia kwa Shehia
zote 61 za Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo elimu imetolewa juu ya kuelewa
ugonjwa wa Corona.
Ambapo pia kiongozi
huyo alieleza kuwa hatua muhimu za kujikinga na ugonjwa huo zikiwemo uvaaji wa
barakoa, kutekeleza maelekezo ya Serikali pamoja na umhimu wa kutoa taarifa
pale wanapogundua kuna mtu ama watu wana dalili za maradhi ya Corona.
Kwa maelezo ya Mkuu wa
Mkoa huyo juhudi zimechukuliwa za kufanya ukaguzi na uchunguzi wa wasafiri
wanaotoka nje ya Kisiwa cha Pemba sambamba na kufanya usimamizi wa kambi ambazo
zilifunguliwa kwa ajili ya kuwaweka wasafiri waloingia nchini kutoka Kenya.
Pamoja na hayo, kiongozi
huyo alieleza hatua zilizochukuliwa
katika kufanya ukaguzi wa bandari bubu ambapo Mkoa huo una jumla ya bandari
bubu 172 ambazo zinatumiwa na wananchi
kwa shughuli mbali mbali.
Aliongeza kuwa Shehia
17 zenye bandari bubu zilikaguliwa na kufuatiliwa ambapo jumla ya wananchi 725
walipitia bandari zisizo rasmi walipatikana ambapo pia, juhudi zilifanywa za
ziara katika maeneo hatarishi yenye mikusanyiko ya watu.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini
Pemba Hemed Suleiman Abdallah alieleza kuwa Mkoa huo kwa kushirikiana na Wizara
ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kupitia Idara ya Habari Maelezo umeweza
kutoa taaluma ya kutosha katika maeneo mbali mbali mjini na vijijini kwa
kutumia gari la matangazo.
Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na wataalamu wa afya vipindi
mbali mbali vimeweza kutengeneza katika
redio za Jamii ikiwemo redio hiyo ya Micheweni pamoja na Redio Istiqama na
Redio pamoja na Televisheni ya ZBC.
Aidha, alieleza kuwa
mashirikiano makubwa baina ya uongozi wa Kusini Pemba na Mkoa wa Tanga katika
kufuatilia wananchi wanaotoka Mombasa ili kujikinga na ugonjwa wa Corona
yamefanyika kwa mafanikio
Mkuu huyo wa Mkoa
aliongeza kuwa hali ya upatikanaji wa chakula kwa kipindi hichi cha Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani ni nzuri ambapo mahitaji ya vyakula vya msingi ukiwemo mchele,
sukari, unga wa sembe na ngano yanaendelea kupatikana madukani na vipo vya
kutosha.
Aliongeza kuwa kutokana
na uhamasishaji na uimarishaji wa huduma za kilimo wananchi wameweza kuzalisha
mazao ya ndizi na muhogo kwa wingi na kwa sasa Mkoa huo tatizo la upatikanaji
wa chakula halipo.
Kuhusu bei ya vyakula,
Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa bado haijabadilika na Serikali ya Mkoa
inaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kwamba bei hazipandi kiholela
lwa kisingizio cha mwezi wa Ramadhani ama maradhi ya Corona.
Pamoja na hayo, Mkuu
huyo wa Mkoa alieleza kuwa katika utekelezaji wa mikakati ya kupambana na janga
la Corona Mkoa huo umeweza kuchukua hatua mbali mbali katika maeneo yote ya
mikusanyiko kama vile masoko,maeneo ya biashara, maeneo ya michezo, sehemu za
ibada, vituo vya daladala na katika Taasisi za Serikali na binafsi ili
kuthibiti ugonjwa huo.
Kwa maelezo ya
kiongozi huyo alieleza kuwa Afisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini Pemba kwa
kushirikiana na vikosi vyengine vya Ulinzi na Usalama vya Mkoa wa Kusini kwa
kushirikiana na Masheha na Madiwani imefanya doria maalum ya kuzikagua na
kuzitambua bandari bubu zote 253 kwa Mkoa wa Kusini.
Sambamba na hayo,
viongozi hao walieleza hali ya amani na utulivu iliyopo katika Mikoa yote
miwili na kueleza kuwa wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kijamii na
kiuchumi kama kawaida pamoja na kushirikiana na Serikali katika kufanikisha
shughuli mbali mbali za kijamiii na kimaendeleo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment