Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Awasilisha Mapato na Matumizi ya Bajeti Kwa Mwaka 2020/2021.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenye Mkutano wa Kumi na Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi ulioanza rasmi kujadili Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Mwaka wa Fedha wa 2020/2021.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba mwelekeo wa hali ya uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2020 unategemea kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo, MKUZA III na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

Alisema Pato la Taifa lilitarajiwa kukuwa kwa kasi ya asilimia 7-8 kwa mwaka 2020 kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa shughuli mbali mbali za Kiuchumi na maendeleo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa Mwaka wa Fedha wa 2020/2021 kwenye Mkutano wa Kumi na Tisa wa Baraza la Tisa la Wawakilishi ulioanza rasmi kujadili Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hata hivyo Balozi Seif alifafanua kwamba kutokana na janga la Virusi vya Corona{COVID – 2019},uchumi wa Taifa unatarajiwa kukuwa kwa kasi ya chini ya asilimia 3 hii itatokana na kuyumba kwa sekta za uchumi ikiwemo utalii, biashara, uwekezaji na kupungua kwa mapato ya Serikali.

Alisema kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na huduma nchini imeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 2.7% mwaka 2019 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.9% mwaka 2018.

Balozi Seif alisema kwamba kushuka huko kumesababishwa na kushuka kwa bei za bidhaa zote za vyakula na zisizo za vyakula ambazo zilitoka asilimia  1.4% mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 2.8% mwaka 2019 wakati bidhaa zisizo za chakula zimeshuka kutoka asilimia 5.7% mwaka 2018 na kufikia asilimia 2.6% mwaka 2019.

Alifahamisha kuwa hali hii inatokana na kuwepo kwa hali nzuri ya hewa, kuendelea kuwawezesha wakulima kwa kutoa pembejeo na mafunzo juu ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia ya gharama nafuu, kuendeleza tafiti katika sekta ya kilimo ili kupunguza na hatimae kutokomeza maradhi yanayokabili mazao ya matunda na mboga za majani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kuendelea kutoa nafuu maalum ya ushuru kwa baadhi ya bidhaa muhimu za chakula, dawa na pembejeo za kilimo kumechangiwa na Benki Kuu ya Tanzania {BOT}kuimarisha sera za kifedha kwa lengo la kuongeza kiwango cha fedha katika uchumi kwa kutoa mikopo kwa benki za biashara.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na utekelezaji wa jukumu  la  kuratibu na kusimamia maliasili zisizorejesheka ikiwemo uchimbaji na usafirishaji wa mchanga katika maeneo mbalimbali yanayohitaji huduma hiyo Muhimu hapa Nchini.

Balozi Seif alibainisha kwamba suala la uratibu wa upatikanaji wa mchanga hapa Nchini umejumuisha maeneo makuu mawili ambayo ni Utoaji wa vibali vya mchanga kwa miradi mikubwa ya maendeleo.

Aliitaja baadhi ya Miradi hiyo kuwa ni pamoja na ile ya Serikali, wawekezaji pamoja na watu binafsi na Utoaji wa vibali vya mchanga kupitia wanajamii ambao utahusisha wananchi wa kawaida, wafanyabiashara wa matofali na kampuni za ujenzi za wazawa.

Katika kuendeleza usimamizi mzuri wa matumizi ya maliasili ya mchanga, Balozi Seif alisema Serikali itaanzisha utaratibu mpya wa maombi ya mchanga kupitia wanajamii wenyewe wanaohitaji mchanga badala kazi hiyo kuendelea kusimamiwa na madereva.

Alisema usajili wa gari Mia 200 Unguja na Mia 150 Pemba zinazopakia mchanga utafanywa kila baada ya miezi mitatu pamoja na kuendelea na utafiti wa kiwango cha maliasili zisizorejesheka (mchanga, mawe, kifusi) kilichopo Nchini kwa mujibu wa mahitaji kwa Zanzibar.

Akizungumzia suala la upatikanaji wa huduma muhimu za Kijamii Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imeanzisha muundo mpya wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kulingana na mahitaji ya Mfumo ulioanzishwa wa Madaraka Mikoani Maarufu Ugatuzi.

Alisema Muundo huu umezingatia majukumu mapya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuundwa Idara sita na vitengo vitano ambapo mafanikio yameanza kuonekana tokea kuanzishwa kwa mfumo huo ikiwemo kuimarika huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile huduma za miundombinu ya barabara za ndani.

Aidha ongezeko la ujenzi na matengenezo ya skuli pamoja na vituo vya afya, idadi ya uandikishaji wa wanafunzi wa maandalizi kwa mwaka 2020 imepanda mara dufu sambamba na ongezeko la mama wanaojifungulia katika vituo vya afya na hospitali.

Balozi Seif amewasisitiza wananchi waendelee kuzitumia huduma zilizopo katika ngazi za Mikoa na Wilaya katika maeneo mbalimbali wanayoishi jambo ambalo litasaidia sana kupunguza msongamano wa kusubiri huduma katika maeneo mengine ya upatikanaji wa huduma hizo Nchini.

Akigusia Mitandao ya Kijamii iliyoshika kasi katika matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na utandawazi Duniani Balozi Seif alisema Maendeleo hayo hayawezi kuepukika wakati huu wa maendeleo ya Ki- Teknohama kupitia mitandao ya kijamii.

Alisema Watu wengi hivi sasa wanatumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Whatsapp na instagram kwa ajili ya kuwasiliana na kupata habari mbalimbali ambapo mitandao yote hiyo inanguvu kubwa katika usambazaji wa habari. 

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionyesha masikitiko yake makubwa kutokana na baadhi ya watu hasa Vijana kutumia visivyo sahihi mitandao hiyo kwa kusambaza habari ambazo hazina ukweli na kuwatia taharuki wanajamii.

Alieleza kwamba mara nyingi taarifa kama hizo hutokea kipindi ambacho Taifa huwemo katika uchaguzi au kipindi kama hiki cha mtafaruki wa kuendelea kuenea kwa maradhi Virusi vya Corona.

Balozi Seif Ali Iddi ameendelea kuwa omba wananchi waache kutumia vibaya mitandao hiyo kwa kutoa taarifa zisizo sahihi na badala yake waziachie mamlaka husika zichukuwe jukumu la kutokaTaarifa husika kwa jambo lolote linalojiri katika Taifa.

Aidha, aliendelea kuwasihi wananchi kuwa na tabia ya kufuatilia habari kutoka vyombo vya habari vya kuaminika ili kuepuka kupokea na wao kusambaza taarifa ambazo si sahihi .

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wananchi wote Nchini kwa mchango wao mkubwa wa kushiriki katika utekelezaji wa miradi na program mbalimbali kwenye maeneo yao.

Balozi Seif aliwanasihi waendelee kushirikiana na Serikali na kuitunza miradi hiyo ili iwe ya kudumu kwani mafanikio katika utekelezaji wa miradi hiyo yanatokana na ushirikiano mzuri baina ya wananchi na Serikali kupitia viongozi wao katika ngazi mbalimbali za usimamizi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliliomba Baraza la Wawakilishi Zanzibar liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Sabini na Tano, Kumi na Tano Milioni, Laki Tano na Thalathini na TatuE lfu { 75,015,533,000 } kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake kwa ajili ya kutekeleza Programu 11ndani ya Kipindi cha Fedha cha Mwaka 2020/2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.