Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al Hajj Dk. Ali Mohamed Shein Akitowa Salamu za Eid El Fitry leo.


Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein, Katiba Baraza la IDD EL FITR, Tarehe 24 Mei ,2020, Sawa na Mwezi Mosi Shawwal , Mwaka 1441 HIJRIYAH.

IDDI MUBARAK

BISMILLAHI RAHMANI RAHIM

Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhanahu Wa Taala, Muumba wa Mbingu na Ardhi kwakuturuzuku neema ya uhai na afya, tukaweza kuikamilisha ibada ya saumu kwa salama na amani na leo hii tunasherehekea sikukuu hii ya Idd El Fitri tukiwa na furaha.

Kwa hakika,  tuliojaaliwa kuikamilisha ibada hii tunapaswa tumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani wenzetu kadhaa ambao tulianza kufunga nao, hivi sasa wameshatangulia mbele ya haki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na awalaze mahala pema  Peponi. Kwa wale wenzetu ambaowalipata mtihani wa maradhi na wakashindwakuitekeleza ibada ya saumu, Mwenyezi Mungu Inshaallah awaondoshee maradhi yanayowasibu na awape afya njema.

 

Ndugu Wananchi,

Kwa baraka za siku hii ya Iddi, tunamuomba Mola wetu Mtukufu azikubali ibada zetu zote tulizozifanya katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na miezi mengine. Kadhalika, tunamuomba atujaaliye uwezo, ilituyatekeleze maamrisho yake na tujiepushe na makatazo yake,tupate kufanikiwa hapa duniani na kesho mbele ya haki. Kwa hakika, tunatamka kwa ulimi na kuitakidi kwa moyo kwamba, hapana Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah. Yeye ndiye anayemiliki uhai wetu na kwake ndiyo marejeo yetu. Tunamuomba Allah, Azza Wa Jalla, atusamehe makosa yetu, na turejee kwake akiwa ameturidhia.

Sala na salamu zimshukie Mtukufu wa daraja na mbora wa viumbe; Mtume wetu Muhammad (SAW), Aali na Sahaba zake, pamoja na wafuasi wake walioshikamana na mwenendo mwema wa mafundisho yake na wakaongoka. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaaliye na sisi sote tuwe miongoni mwao.

Baada ya kumtukuza Mola wetu Mtukufu; Subhanahu Wa Taala na kumtakia rehema na amani Mtume wetu Muhammad (SAW), natoa  salamu zangu kwawananchi wote wa Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  pamoja na Waislamu duniani kote. Allah atujaalie sikukuu njema yenye furaha na amani na aizidishie baraka nchi yetu.

Ndugu Wananchi,

Leo ni sikukuu ya Idd el Fitri, ambapo Waislamu wa Zanzibar na wananchi wote tunaungana na wenzetu katika mataifa mbali mbali katika kusherehekea sikukuu hii muhimu ya furaha, ikiwa ni miongoni mwa sikukuu adhimu alizotuwekea Mwenyezi Mungu kwa kila mwaka. Imepokelewa kutoka kwa Imam Ahmad, Hakim, Abu Daud na An-nisai kwamba Bwana Mtume Muhammad (SAW) alipohamia Madina na kuwakuta wakaazi wake wakisherehekea sikukuu kinyume na twaa ya Mwenyezi Mungu aliwaambia; maneno yenye tafsiri ifuatayo:-

“Hakika Mwenyezi Mungu amekubadilishieni sikukuu mbili, bora kuliko zenu mlizokuwa mkizisherehekea. Sikukuu ya Idd el Fitri na Idd el Hajj.”

Kwa hivyo, tuna wajibu wa kumshukuru Mola wetu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii ya Idd el Fitri, tukiwa hai na wazima wa afya. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kusali sala ya Idd katika misikiti mbali mbali kwa salama. Ni vyema tuendelee kuisherehekea siku hii kwa kufanya mambo yote ya halali, pamoja na kuombeana dua za kheri, zikiwemo zile za kuwaombea wagonjwa wetu waliomo katika nyumba zetu na hospitalini.

Ndugu Wananchi,

Tumeukamilisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mwezi ambao una utukufu mkubwa kwa Waislamu. Huu ndio mwezi ulioteremshwa kitabu kitukufu cha Qurani, ili uwe muongozo na uongofu kwetu sote. Mwenyezi Mungu ametubainishia katika  aya ya 185 ya Suratul Baqarah  yenye tafsiri isemayo:

“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa ndani yake Qurani kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi na uwongofu na upambanuzi,….”

Katika hadithi nyengine mashuhuri inayothibitisha ubora wa Mwezi wa Ramadhani, Mtume Muhammad (S.A.W) amesema, katika tafsiri ifuatayo:

“Enyi watu! Hakika umewaelekeeni nyinyi Mwezi wa Ramadhani kwa baraka, rehma na msamaha, mwezi ambao ni  bora mbele ya  Mwenyezi Mungu  kuliko miezi yote, siku zake ni bora kuliko siku zote, na saa yake ni bora na muhimu kuliko saa zote”.

Kwa mnasaba wa hadithi hio, ni dhahiri kwamba ibada zote tulizozifanya katika Mwezi wa Ramadhani zilikuwa na fadhila kubwa zaidi kuliko zile tunazozifanya katika miezi mengine. Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe miongoni mwa walionufaika na fadhila kubwa za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tulioukamilisha na aendelee kutudumisha katika ibada.

Utukufu mwengine wa Mwezi wa Ramadhani ni kwamba, amali za waja katika kufanya ibada huwa na fadhila kubwa zaidi kuliko miezi mengine, ikiwa ni pamoja na kusamehewa makosa yote, iwapo tulifunga kwa imani na kumtegemea Yeye, Mwenyezi Mungu. Imepokelewa kutoka kwa Imamu Al- Bukhariy na Muslim, kwamba Mtume Muhammad (S.A.W) amesema, katika tafsiri ifuatayo:

“Atakayefunga Ramadhani kwa imani na kutaraji malipo, ataghufiriwa madhambi yake yaliyotangulia”

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu azikubali saumu zetu, na ziwe sababu ya Yeye kutusamehe makosa yetu.

 

Ndugu Wananchi,

Kama mnavyofahamu kwamba ni kawaida yetu baada ya kuikamilisha ibada ya saumu, tunaamkia na sala ya Iddi ambayo waumini wengi hujumuika pamoja, kwa ajili ya sala hio, kwenye uwanja uliokubaliwa rasmi na katika misikiti mingine mbali mbali ya Unguja na Pemba.  Kwa bahati mbaya, katika kipindi hiki, nchi yetu imekumbwa na mtihani wa maradhi ya COVID-19. Maradhi haya yameathiri mwenendo wa baadhi ya taratibu zetu za maisha na kutufanya tuitekeleze ibada ya funga mwaka huu, katika hali maalum, tafauti na miaka iliyopita.Tumelazimika tuziache baadhi ya taratibu na utamaduni tuliouzowea kuufanya katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani wa mwaka huu, kama sote tulivyoshuhudia na tunavyokumbuka. Kwa mfano, sala za jamaa na tarawehe hazikusaliwa kama ilivyo kawaida;baadhi ya misikiti ilifungwa na hata vikao vya  itikaaf havikufanyika katika utaratibu  uliozoeleka. Vile vile, mashindano ya Quran katika ngazi mbali mbali hayakuweza kufanyika, na tuliiacha ile desturi yetu ya kualikana na kufutari kwa pamoja.

 

Katika sikukuu ya Idd El Fitr ya mwaka huu,hatukuweza kukutana kwenye Baraza la Iddi, ambalo ni sehemu muhimu katika historia na utamaduni  wa  watu Zanzibar. Katika hali hio, nimeona ni muhimu nitoe salamu zangu za Iddi kwa kuzungumza nanyi kwa njia hii ya telivisheni na redio. Kwa hivyo, pokeeni salamu zangu za Idd el Fitri Waislamu nawananchi wote wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla. Nakutakieni nyote na familia zenu sikukuu njema, yenye kheri na baraka nyingi. Kwa baraka za siku hii, tumuombe Mola wetu Mlezi atuondoshee balaa na majanga katika nchi yetu; na aizidishie nchi yetu amani na mshikamano, ili iwe sababu ya kupiga hatua zaidi za maendeleo na ustawi wa jamii yetu.

 

Ndugu Wananchi,

Mafunzo makubwa tuliyojifunza katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni uchamungu. Maulamaa wengi wamekubaliana kuwa uchamungu ni kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kujitenga na madhambi  na kila alichokikharamisha Yeye. Hapana shaka, katika kipindi chote cha utekelezaji wa ibada ya saumu, jamii yetu ilijipamba vazi la uchamungu kutokana na namna tulivyodhamiria kushikana na mwendo mwema. Kwa hakika uchamungu

 

si kufunga na kusali tu, bali uchamungu umekusanya mambo mengi mema,yakiwemo subira, kuhurumiana, kupendana, uaminifu na uadilifu. Mambo yote haya yanatuwezesha kuishi vizuri katika jamii kwa kutendeana mema, kuzitii sheria, pamoja na kufuata maadili na maelekezo mbali mbaliyanayotolewa na Serikali, yanayolenga kutuepusha na matatizo yanayoweza kuepukika.

  

Katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tulijifunza subira kwa kukaa kutwa bila ya kula, kunywa na kujinyima mambo mengine ya halali. Vile vile, tulijifunza kusubiri kwa kujizuia na vitendo viovu na badala yake tukajitahidi kufanya mambo mema, kama vile kujitafutia riziki za halali, kuacha kusema uongo, kusengenya, kuvaa mavazi ya heshima yenye kufuata mafundisho ya dini na mambo mengineyo tuliyoyaelekeza katika kumtii Mwenyezi Mungu. Kwa ujumla, subira ilihuisha imani na utii wetu mbele ya Mola wetu. Funga zetu zilikuwa baina  yetu na Mola wetu tukiwa na imani kwamba anatuona na anayajua yote tunayoyafanya, na Yeye ndiye atakayetulipa.

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuahidi malipo ya subira katika tafsiri ya sehemu ya aya ya 10 ya Surat Azzumar kwa kumuagiza Mtume wetu Muhammad (S.A.W) atwambie, katika tafsiri isemayo:

“Sema:………Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hesabu”

 

Kwa hivyo,tumuombe Mola wetu atulipe malipo bora kama alivyotuahidi katika aya niliyoitaja.Kadhalika, kwa mnasaba wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,  hadithi ya Mtume Muhammad (S.A.W) inasema, katika tafsiri ifuatayo:

“Huu mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kusubiri na hakika subira malipo yake ni pepo”

 

Kwa mantiki hii, hatuna budi tuendelee na mwendo huu wa kuwa na subira kwa manufaa yetu hapa duniani na kesho akhera. Tumuombe Mwenyezi Mungu, atuwezeshe kuwa na subira, ili tupate malipo hayo ya Pepo.

 

Ndugu Wananchi,

Kadhalika, tulijifunza kupendana na kuhurumiana, ambapo baadhi ya wenye uwezo waliwasaidia wananchi wenzao wasio na uwezo katika kuwapa sadaka na zaka za aina na viwango tafauti. Vile vile, nilipata taarifa kwamba baadhi ya wafanyabiashara waliuza bidhaa zao kwa bei nafuu, ili kuwawezesha wananchi wenzao wanunue mahitaji yao ya Ramadhani. Hili ni jambo jema sana na ni miongoni mwa faida za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mwenyezi Mungu katika sehemu ya mwisho ya aya ya 2 ya Suratul Maidah anatwambia katika tafsiri ifuatayo:

“ …..Na saidianeni katika wema na taqwa, wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni

Mwenyezi Mungu , hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu”.

 

Kwa hivyo, mbali yakuongeza jitihada zetu katika kufanya ibada mbali mbali,  zikiwemo kusali sala za faradhi na sunna, kusoma Qurani, na kujizuia kufanya maovu mbali mbali,kwa kutarajia fadhila na radhi za Mola wetu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu atatujaalia kupata faida nyengine muhimu na kutuepusha na adhabu Zake kali,iwapo  tutaendelea na mwenendo huu wa kupendana na kusaidiana katika mambo mema. Tujiepushe na husda, kuchukiana na uhasama kwa visingizio mbali mbali.Mara nyingi mambo haya husababishwa na kibri, dharau na kejeli miongoni mwa wanaadamu. Ni khulka mbovu ambazo zinaletwa na ushawishi wa shetani. Katika aya ya 21 ya Surat Nur, Allah Subhanahuu Wa Taala anatuonya tusifuate ushawishi wa shetani katika tafsiri isemayo:

“Enyi mlioamini! Msifuate nyayo za Shetani; na atakayefuata nyayo za Shetani (atapotea) kwani yeye huamrisha mambo ya aibu na maovu;…..”

 

Kwa mnasaba wa aya hii, Mola wetu Mlezi anatuzindua kuwa iwapo tutamfuata shetani tutapotea. Kwa hivyo, tuone kwamba tabia za kuchukiana, kudharauliana na kukejeliana hazitatuletea faida yoyote, ila zinakuwa kichocheo kikubwa cha kuharibu amani na utulivu tulio nao. Ili tuweze kudumisha amani na ustawi wa jamii yetu, ni lazima tuyaache  mambo hayo maovu. Katika hadithi ya Bwana Mtume Muhammad(S.A.W), iliyopokelewa na Imamu Bukhariy, Kiongozi wetu huyo anatuusia kwa kusema maneno yenye tafsiri ifuatayo:-

“Msihusudiane, msichukiane, wala kuoneana. Na kuweni na umoja na mshikamano, mambo yatanyooka”.

 

Kwa hivyo, tujitahidi katika kufungamana na wasia huo wa Mtume wetu (S.A.W), ili tunyookewe na mambo yetu katika maisha yetu ya kila siku.

 

Tunamuomba Mola wetu azidi kututia imani,mapenzi na huruma,ili tuendelee kuzishukuru neema zake, na atudumishe katika kuyafuata maamrisho yakena tuzitii sheria za nchi yetu.

 

Ndugu Wananchi,

Mafunzo mengine tuliyoyapata katika ibada ya saumu, ni uaminifu na uadilifu. Wengi wetu tulijitahidi natulijidhatiti katika kufanya haki na kuepuka kufanya vitendo viovu kwa ajili ya kupata radhi za Allah. Vile vile, tukumbuke kwamba tunaposhirikiana na Serikali katika kuimarisha uchumi, kudhibiti mapato na kuzilinda rasilmali zetu mbali mbali, ni njia moja ya uaminifu na kufanya uadilifu. Sote tuendeleze tabia hii ya uaminifu na uadilifu katika kutekeleza majukumu yetu kwenye familia zetu, jamii au katika dhamana tulizokabidhiwa na Serikali yetu. Tuepuke kufanya vitendo viovu kama vile vya uonevu na hujuma ambavyo vinaweza kutupeleka katika mustakabali mbaya.

 

Ni wajibu wetu tuyaendeleze mafunzo haya tuliyoyapata katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani popote na wakati wote katika maisha yetu ya kila siku.Katika hadithi iliyopokelewa na masahaba wawili, nao ni, Jundub Ibn Junaida, kwa umaarufu akiitwa Abu Dharr na Mu’adh Ibn Jabal au Abu Abdul Rahman, Bwana Mtume Muhammad (SAW), ametuhimiza tuwe wachamungu kwa kumcha Mwenyezi Mungu wakati wote na popote tulipo. Haya yamo katika tafsiri ya hadithi isemayo:

“Mche Mwenyezi Mungu popote ulipo, na fuatanisha kitendo kibaya kwa kitendo kizuri, na ishi na watu kwa uzuri”

 

Kwa hivyo, ni vyema tukatanabahi kuwa mafunzo tuliyoyapata katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ambayo yote yamefungamana na ucha mungu, ni wajibu wetu tuyaendeleze na tuyadumishe wakati wote katika maisha yetu na yasiwe katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani peke yake. Tuziendeleze khulka zote njema huku tukizingatia kuwa sote ni waja wa Mwenyezi Mungu, Azza wa Jalla, Yeye ndiye tunayemtegemea na Kwake ndio marejeo yetu.

 

Ndugu Wananchi,

Tumetekeleza ibada ya Saumu mwaka huu, ikiwa tumo katika msimu wa mvua za masika. Mvua za masika za mwaka zimenyesha zaidi ya  viwango vya kawaida katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

  

Inasemekana kuwa mvua hizi zimefuatana  na mvua za vuli zilizonyesha kwa wingi na kwa kipindi kirefu, hali ambayo imesababisha mafuriko hapa  Zanzibar yaliyopelekea wananchi wa maeneo mbali mbali hasa ya nje ya Mji waathirike kwa namna mbali mbali.

 

Natoa pole kwa wananchi wote waliokumbwa na mafuriko na hasa wale  wote  ambao nyumba na mali zao zimeathiriwa kutokana na mvua zilizonyesha. Namuomba Mwenyezi Mungu awape subira, nguvu na uwezo waathirika wote wa mafuriko hayo, ili waweze kurejesha mali walizopoteza na waendelee kuishi katika hali ya kawaida na furaha.

 

Hivi sasa,  Serikali inaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ya Unguja na Pemba  yaliyoathirika, ili iweze kurejesha miundombinu iliyoharibika na ichukue hatua nyengine za haraka, ili ione namna inavyoweza kuwahudumia walioathirika.   Nawaagiza viongozi  wa  Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri waongezekasi katika kuimarisha usafi wa Miji, ili tujikinge  na maradhi ya miripuko, ikiwa ni pamoja  na kuhakikisha kwamba tunayadhibiti maradhi ya kipindupindu.

 

Kwa upande mwengine, sote tunafahamu kwamba mvua ni neema, kwa hivyo, nawahimiza wakulima waitumie neema hio, kwa kuzidisha  nguvu katika kilimo cha mazao mbali mbali pamoja na miti ya kudumu, ilituimarishe mazingira pamoja na kuongeza upatikanaji wa chakula  nchini.

 

Ndugu Wananchi,

Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tulijifunza kufanyakazi kwa bidii, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya familia zetu kwa jasho letu wenyewe. Ni  wajibu wetu tuuendeleze moyo huu wa kujituma kwa njia za halali wakati wote wa maisha yetu, kwa kadri afya zetu zinavyoturuhusu. Mara nyingi nimekuwa nikisisitiza kwamba, ili  kazi  tunazozifanya ziwe na tija, ni lazima  tuzifanye kwa bidii, maarifa na kwa kuzingatia  misingi ya  uaminifu, na tujiepushe na tamaa  na ghilba. Nawahimiza viongozi wawewabunifu , wenye kujiamini katika kazi kwa kutumia vizuri ujuzi, elimu na maarifa waliyonayo. Uislamu unatufundisha kwamba uaminifu, elimu, na ujuzi ni vigezo muhimu ambavyo mwajiri anapaswa avizingatie  wakati anapotaka kumwajiri mfanyakazi.

 

Tunajifunza hayo katika maisha ya Nabii Mussa (A. S),  kwamba aliwahi kupendekezwa na mtoto wa Nabii Shuaib aajiriwe na baba yao, kwa sababu ya nguvu (uwezo) na uaminifu aliokuwa nao. Haya yanathibitika katika Suratul Qasas, kwenye aya ya 26, pale Mola Wetu Mtukufu anapotufahamisha katika tafsiri isemayo:

Alisema mmoja wa  Wale wawili :

“Ewe baba  yangu! Mkodi huyu. (awe anachunga wanyama wako badala yetu). Bila ya Shaka mbora uwezaye kumwajiri ni ambaye mwenye nguvu, mwaminifu (Na huyu ana sifa zote hizo.)”

Vile vile,  umuhimu wa ujuzi  katika kuleta ufanisi katika kazi tunazozifanya  umeelezwa  wazi  wazi katika Qurani,  katika Surat Yusuf, aya ya 55 katika tafsiri isemayo:

“Nifanye mtazamaji wa hazina za nchi (yote) hakika mimi ni mlinzi na mjuzi hodari.”

 

Tuzingatie elimu na hekima iliyomo katika aya hizo,ili  tuzidi kuhamasika  kufanya kazi kwa kutumia vizuri elimu, ujuzi, uzoefu na maarifa yetu zaidi. Nazidi kuwahimiza na kuwakumbusha wafanyakazi wenzangu tulioko kwenye ajira ya Serikali na katika sekta binafsi,  tuithamini   na tuishukuru neema ya kupata ajira  kwa kutekeleza dhamana na majukumu tuliyokabidhiwa  kwa uadilifu na kwa kuzingatia  sheria na kanuni mbali mbali zinatuongoza. Tuziheshimu mali za umma na za waajiri wetu natuhakikishe kwamba familia zetu zinanufaika na tunavyovichuma vya halali hivi sasa na baadaye tutakapokuwa tumeshatangulia mbele ya haki. Ni lazima tupambane na  vishawishivyote vinavyoweza kututumbukiza katika vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

 

Serikali kwa upande wake  itahakikisha kwamba inaendelea kuwapatia wafanyakazi fursa za kujiendeleza kwa elimu na ujuzi zaidi, ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi. Sambamba na utekelezaji wa azma hio, Serikali itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa, kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale  wote watakaothibitika kushiriki au kuchochea vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.

 

Ndugu Wananchi,

Wakati tuna furaha ya kusherehekea Sikukuu hii ya Eid el Fitri, ni muhimu  tukakumbushana na kuzingatia kwamba bado nchi yetu imekabiliwa na janga la maradhi ya COVID 19, yanayosababishwa na Virusi vya  Korona. Maradhi haya bado yapo, licha ya mafanikio ya kuridhisha tunayoendelea kuyapata kutokana najitihada mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali.Tunafarijika kuona namna wananchi walivyokuwa imara katika kupambana na COVID-19 kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa wakati wote, mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa  kupunguza kiwango cha maambukizo katika sehemu zote za Unguja na Pemba.  Hadi  tarehe 20 Mei, 2020, jumla ya wagonjwa 34 walioambukizwa maradhi hayo wanaendelea kupata  matibabu katika vituo  vitano tulivyovianzisha, kutoka miongoni mwa idadi yawagonjwa 134 iliyowahi kufikiwa tarehe  1 Mei, 2020.Wagonjwa wote hao wanaendelea vizuri na hapana mwenye hali mbaya.

 

Licha ya sababu mbali mbali za kitaalamu, ambazo zinaaminika kuhusiana na kuibuka ghafla kwa maradhi haya ya COVID-19; hata hivyo, Mwenyezi Mungu katika Quran ametuelezea kwamba misukosuko itatukuta katika maisha. Katika Aya ya 155 ya Surat Al Baqarah, Mola Mtukufu anatueleza juu ya mitihani ya aina hio katika tafsiri isemayo:

“Na tutakutieni  katika  msukosuko wa ( baadhi ya mambo haya), hofu na  njaa na upungufu wa mali  na wa watu na matunda.  Na wapashe habari njema wanaosubiri.”

 

Kwa hivyo, pamoja na vifaa na ujuzi wa wataalamu wetu, inatupasa tuongeze nguvu katika kutumia umoja wetu na mshikamano tulionao, maelewano, bidii,subira na tuendelee kushirikiana katika kupambana na ugonjwa huu na katika ibada zetu tuendelee kumuomba  Mola wetu  Mtukufu kama tunavyomuomba wakati wote, ili atupe ushindi katika vita hivi na atukinge na kila janga na balaa.

 

Tunapaswa tuzingatie kwamba jitihada zetu hizo zinahitaji zaidi usikivu wetu katika kufuata maelekezo na kuiheshimu miongozo inayoendelea kutolewa na Viongozi wa Serikali,Madaktari na Wataalamu wetu  wa afya. Hatuna budi, ni lazima tuyatekeleze mambo tunayoelekezwa  naWakuu wa Mikoa, Wilaya, Mabaraza ya Miji na Manispaa, Halmashauri na viongozi katika ngazi mbali mbali.  Tuendelee kujenga ujasiri na kuondoa hofu katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa wa COVID 19. Tuendelee kufanya shughuli zetu, ili tuweze kuchangia katika kuimarisha uchumi wetu ambao umepata changamoto  tanguyalipoingia maradhi haya.

 

Ndugu Wananchi,

Kwa mara nyengine, natoa pongezi zangu za dhati kwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kupambana na Maafa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, ambaye ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar  pamoja  na wajumbe wote, na  Mwenyekiti wa  Kamati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Kupambana na Maradhi haya ya COVID 19, Mheshimiwa Kassim Majaaliwa Majaaliwa, ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; pamoja na wajumbe wote, kwa kufanya kazi nzuri kwa kushirikiana  na uzalendo wa hali ya juu.Mambo yote waliyoyafanyia kaziyametoa  matokeo mazuri, katika kuwahudumia wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Vile vile, shukurani zangu nazitoa kwa viongozi wengine mbali mbali wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama; viongozi wa dini,  wafanyabiashara, madereva wa vyombo vya usafiri wa nchi kavu na baharini na  wananchi wote kwa jumla kwa kuziunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na maradhi haya. Kila Taasisi ilitekeleza wajibu wake kwa kulingana na majukumu na uwezo wa Taasisi hio.Kadhalika, shukurani zangu za dhati nazitoa kwa madaktari na wataalamu wa afya, ambao tangu yalipoanza maradhi haya, wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kutoa elimu kwa wananchi, pamoja na kuwapa huduma mbali mbali wale wote walioathirika au walioonesha dalili za maradhi hayo.

 

Kadhalika, navipongeza vyombo vya habari mbali mbali kwa kufanya kazi kubwa ya kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu  maradhi haya. Nawahimiza waandishi wa habari waendelee na ari na uzalendo wa   kuyalinda maslahi ya nchi yetu, kwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili yao.

 

Natoa pole kwa wananchi wote waliopata msiba kwa kuondokewa na ndugu na jamaa zao kutokana na maradhi ya COVID-19, Mwenyezi Mungu awape subira na wale wote waliokwishatangulia mbele ya haki kutokana na maradhi haya, Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema peponi.Amin.

 

Ndugu Wananchi,

Kutokana natamko rasmi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lililotolewa tarehe 19 Machi, 2020, kuhusu hali ya ugonjwa wa COVID 19 hapa Zanzibar, na mambo kumi muhimu yaliyopaswa yatekelezwe, katika kuwahudumia waathirika wa maradhi hayo na kuyadhibiti Maambukizo yake.  Vile vile,kwakuzingatia hali ya maradhi na mwenendo wake ulivyo, Serikali ya Mapinduziya Zanzibar inakusudia kuregeza masharti yaliyowekwa hapo awali katika mambo hayo kumi, hatua kwa hatua.  Hata hivyo, uamuzi wa kuregeza masharti hayo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utatolewa wakati wowote kuanzia sasa.

 

Ndugu Wananchi,

Kuanzia tarehe 6 Mei, 2020, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilianza vikao vya kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba ya kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021.  Hadi leo, tunaposherehekea Sikukuu ya Idd El Fitri tayarijumla ya Wizara nane (8) zimeshawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara zao. Bajeti kuu ya Serikali itawasilishwa tarehe 15 Juni, 2020. Nakuhimizeni wananchi muendelee kufuatilia vikao hivyo, ilimuweze kuifahamu kwa undani mipango mbali mbali ya maendeleo ya nchi yetu iliyopangwa na Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.

 

Natoa pongezi kwa Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, na Waheshimiwa Wawakilishi wote, kwa kazi nzuri wanayoifanya  ya kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali. Nimekuwa nikifuatilia mijadala ya vikao vya Baraza na nimeridhishwa sana na michango ya Waheshimiwa Wajumbe inayoonesha wazi dhamira yao ya kuongeza kasi na kuimarisha jitihada za maendeleo ya nchi yetu.

 

Kadhalika,  natoa shukurani kwa viongozi wa Serikali katika Baraza la Wawakilishi, wakiongozwa na Mheshimiwa Makamo wa Pili wa Rais, kwa namna wanavyoiwakilisha Serikali na kujibu hoja za Waheshimiwa Wawakilishi. Nalitakia Baraza letu kila la kheri na mafanikio katika kumalizia kazi yao hio ya kikatiba kwa wizara wanazoendelea nazo.

 

Vile vile, naipongeza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), kwa jitihada zao za kuwasambazia maji wananchi katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa wale waliokuwa hawapati huduma hizo. Nawahimiza viongozi wa  Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) wahakikishe kwamba miradi mikubwa ya maji safi na salama  tuliyoitekeleza kwa ufanisi hivi karibuni, inatoa tija iliyokusudiwa kwa wananchi. Wananchi tuna wajibu wa kushirikiana na ZAWA katika kuilinda miundombinu ya miradi ya maji, ili tuhakikishe kuwa miradi hio inakidhi lengo la Serikali lililokusudiwa kwa maslahi ya wananchi wote.

 

Ndugu  Wananchi,

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufunga mwezi wa Ramadhani bila ya kuwepo tatizo la bidhaa muhimu za chakula, licha ya kuwepo kwa changamoto ya maradhi ya COVID  19.  Natoa pongezi kwa Wafanyabiashara, wakulima, wavuvi na wafugaji kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na chakula cha kutosha wakati wote.

 

Kadhalika,natoa shukurani zangu za dhati kwa  wananchi  waliotoa zaka na sadaka kwa ajili ya kuwakirimu wananchi wengine  na ndugu zao wenye kustahiki kupata  haki na  riziki hizo. Bila ya shaka, waliofanya hivyo wana ujira mkubwa kwa Mola wetu Mlezi, kama alivyotuambia katika Surat Al Baqarah kwenye aya ya 262, katika tafsiri isemayo:

“Wale  wanaotoa mali zao kwa njia ya Mwenyezi Mungu, kisha  hawafuatishii- waliyoyatoa- masumbulizi wala udhia, wao wana ujira wao kwa Mola wao, wala haitokuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika”.

 

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuzidishie imani na hamu ya kutoa kwa yale aliyoturuzuku,  ili tupate  radhi zake na ujira mkubwa hapa Duniani na Akhera tuendako.

 

Nawahimiza  wazazi na walezi tuendelee kusimamia malezi, usalama na afya za watoto wetu katika Sikukuu hii, ambapo viwanja vya kufurahishia watoto vimefungwa. Tusiwaachie watoto wakaranda ovyo mitaani na tujuwe mahali maalumu walipo na nini wanachofanya, ili tuweze kuzilinda afya zao na usalama wao.

Ndugu Wananchi,

Namalizia hotuba yangu kwa kukutakieni nyote sikukuu njema yenye furaha na amani.  Tumuombe Mola wetu Mtukufu atuzidishie amani, umoja na mshikamano.  Aizidishie neema nchi yetu na atupe uwezo mkubwa zaidi  wa kupanga na kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo. Atupe neema ya mvua zenye kheri na atukinge na maradhi pamoja na majanga mbali mbali. Namuomba Mwenyezi Mungu atuondoshee balaa hili la maradhi ya COVID-19, na tuweze kurudi katika hali zetu za kawaida, katika kuendesha maisha yetu.

 

IDD MUBARAK

WAKULLU AAMUN WAANTUM BIKHAYR

Ahsanteni kwa kunisikiliza.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.