Habari za Punde

Balozi Seif Aendelea na Ziara Yake Mkoani Shinyanga.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akiwapungia Mkono Vijana wa CCM alipofika Shinyanga Mjini kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Nyumba ya Katibu wa UVCCM Wilaya hiyo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Vijana mara baada ya kujweka Jiwe la Msingi la Nyumba ya Makaazi ya Katibu wa UVCCM Wilaya hiyo hapo Mtaa wa Negezi.
VIJANA wa UVCCM CCM wakihamasika katika hafla ya uwekwaji wa Jiwe la Msingi la Nyumba ya Katibu wao wa Wilaya katika Mtaa wa Negezi Shinyanga Mjini.
Muonekano wa Jengo la Makaazi ya Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ambalo Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi aliliwekea Jiwe la Msingi.

Na.Othman Khamis.OMPR.
Umoja wa Vijana wa CCM {UVCCM} Tanzania umetahadharishwa kutokubali kubeba wagombe kwa maslahi binafsi kwa vile kundi hilo mara kadhaa hukabiliwa na ushawishi unaoishia kuwaingiza katika vitendo vya Rushwa sambamba na kumuunga mkono Mtu asiyestahiki kupewa dhama ya kuongoza Umma.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi  Balozi Seif  wakati akizungumza na Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika hafla fupio ya kuweja jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Nyumba ya Katibu wa Umoja wa Vijana wa Wilaya hiyo.
Balozi Seif alisema wajibu wa Vijana wa CCM  wakati wowote ni kuhakikisha wanasimamia pamoja na kushiriki katika kumpata mgombea anayekubalika ndani ya CCM mwenye sifa na Mzalendo wa kufuata Kanuni na Miongozo yote inayowekwa na Chama.
Alisema zoezi la kupata Kiongozi mahiri na mzalendo linahitaji umakini mkubwa wakati wote wa mchakato wa Kura za Maoni jambo ambalo litawahakikishia Viongozi, Wanachama na Wananchi  kwamba Yule waliyempendekeza kushika Uongozi atakuwa tayari kutumikia Umma muda wowote ule.
Alitahadharisha kuepukwa kwa makundi na ubaguzi unaoashiria cheche za kutaka kuwagawa Wananchi hasa Watanzania waliokwishaungana kidamu muungano uliorasimishwa mnamo Aprili 26 Mwaka 1964.
Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Kichama ameupongeza Uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini kwa uamuzi wake wa kulitekeleza Agizo la Baraza Kuu la Umoja huo lililoagiza Wilaya ya Mikoa yote iwe na Majengo ya Ofisi na Nyumba za kuishi watumishi wa Umoja huo.
Balozi Seif alisema uamuzi huo wa Kizalendo kwa kiasi kikubwa utasaidia kuondosha adha za wenye Nyumba Mitaani ambao wamekuwa na tabia ya kuwabughudhi Wapangaji wao na Watumishi hao wa UVCCM wakiwa miongoni mwa waathirika hao.
Akitoa Taarifa fupi ya Mradi wa Ujenzi wa Nyumba hiyo ya Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Katibu wa Jumuiya hiyo Nd. Raphael Patrick Nyani alisema lengo la Mradi huo ni kuwaondoa Watumishi wote wa Jumuiya katika mfumo wa nyumba za kupanga.
Nd. Raphael alisema ujenzi huo ulioanza Mnamo Tarehe 27 Mei Mwaka huu wa 2020 tayari umeshafikia hatua ya Linta uliolenga kuwa na Vyumba Vitatu,Jiko, Sebule na umeshagharimu jumla ya shilingi Milioni 5,000,000/- wakati hadi kukamilika kwake utafikia gharama ya shilingi Milioni 20,000,000/-.
Alisema Mkoa wa Shinyanga tayari umeshaanza mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Watumishi wa UVCCM ambapo kwa sasa Wilaya ya Kishapu na Kahama zimefikia hatua kubwa inayokwenda sambamba na Wilaya ya Shinyanga Mjini.
Katika hafla hiyo ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Nyumba ya Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Balozi Seif  Ali Iddi alichangia Shilingi Miloni Moja Taslim zilizoleta hamasa na kumshawishi Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi naye kuchangia shilingi Laki 500,000/-.
Mama Asha katika kulipa msukumo suala hilo muhimu kwa uhai wa Jumuiya akalazimika kuanzisha mchango wa papo kwa papo uliowahusika Viongozi na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi na hatimae kupatikana  mchango wa Shilingi Milioni 6,713,000/-.
Mapema asubuhi Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga alikabidhi msaada wa Kompyuta Nne na Shilingi Laki 500,000/- akikamilisha ahadi aliyoitoa kwa Skuli ya Sekondari ya Uloa katika Wilaya ya Ushetu.
Akikabidhi msaada huo kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama Nd.Thomas Muyonga, Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi alisema ameamuwa kutoa mchango huo kutokana na Kazi kubwa wanayoifanya Walimu na Wanafunzi wa Skuli ya Uloa katika kuimarisha Sekta ya Elimu.
Balozi Seif alisema mchango wake pamoja na, Fikra, mawazo na jitihada za washirika wengine wa maendeleo katika kuunga mkono Sekta ya Elimu utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza vipaji vya Taaluma kwa Wanafunzi hao walioonyesha mfano katika matokeo ya ufaulu wao ndani ya Mkoa.
Akipokea msaada huo wa Kompyuta Nne Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kahama  Ndugu. Thomas Muyonga kwa niaba ya Uongozi wa Skuli ya Sekondari ya Uloa amemshukuru na kumpongeza Mlezi huyo bora na muungwana  kwa kutekeleza ahadi anazotoa.
Wakati wa Mchana Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Alikutana na Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM ya Wilaya ya Shinyanga Mjini na Shinyanga Vijijini katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya CCM Mkoa Shinyanga.
Akibadilishana mawazo nao Balozi Seif alisema kila Mtu au Mwanachama  wa wa chama cha siasa ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa katika nafasi yoyote kwa mujibu wa Katiba na Sheria zilizopo Nchini hasa ndani ya Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa.
Hata hivyo alisema zipo sababu zinazoelezea wazi  ndani ya Katiba na Sheria hizo zinazotoa fursa kwa anayefaa kama ni muumini thabiti anayeweza kuwa tayari kusimamia Umoja na Mshikamano na kuwa tayari Kulinda Katiba, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania.
Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi hasa wale wenye nia ya kutaka kuwa Viongozi wazingatie kukwepa udhaifu wa kutanguliza dhana dhidi ya wengine hasa muda huu unaokaribia Uchaguzi kwani unaweza kumuathiri Mtu bila ya sababu akiwa hana hatia yoyote.
Amewahakikishia Wajumbe hao kwamba Viongozi wa Zanzibar watasimamia kumpata Rais bora atakayekuwa na uwezo kamili wa kuvaa kiatu atakachokiacha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi anayemaliza muda wake Dr. Ali Mohamed Shein.
Ameziagiza Sekreterieti za Wilaya pamoja na Mkoa wa Shinyanga kuandaa taratibu safi zitakazolinda Demokrasia ya kila mgombea anayeomba ridhaa ya Chama kugombea nafasi ya Uongozi.
Wakielezea Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 hadi 2020 Wabunge wa Majimbo yaliyomo ndani ya Wilaya ya Shinyanga Mjini , Shinyanga Vijiji na wale wa Viti Maalum Mkoa walisema kasi ya utekelezaji wa Ilani ndani ya Majimbo yao ilikwenda kwa kasi na kuleta matumaini kwa Wananchi.
Walisema wao bado ni Watumishi wa Wananchi hadi Tarehe 14 Mwezi huu wakati wa kuchukuwa Fomu na wanaendelea kukamilisha Miradi na Ahadi zilizobakia katika kipindi hichi kifupi.
Hata hivyo walibainisha kwamba wakati wanaposhirki masuala ya Kijamii katika maeneo yao wasionekane kwamba wanapiga Kampeni wakati bado wana dhima ya kuwatumikia Wananchi kwa wakati huu uliobakia.
Akimkaribisha Mlezi huyo Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga akiwa pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Nd. Gasper Kileo alisema Uchaguzi bila ya fedha unawezekana kabisa hasa katika Majimbo na Wadi.
Nd. Gasper alisema upo ushahidi wa maendeleo makubwa yaliyopatikana vipindi vilivyopita yaliyosimamiwa na Waheshimiwa Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar na Madiwani yanayoonekana na wala Viongozi hao hawana haja ya kubabaika.
Hata hivyo Nd. Gasper aliwatahadharisha baadhi ya wale waliotia nia ya kugombea wametengeneza makundi ambayo kwa kutumia mfumo wa Mitandao ya Kijamii yanaweza kubomoa mchakato mzima wa Uchaguzi kitendo kisichovumiliwa na Chama na hata Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.