Habari za Punde

Balozi Seif akabidhi Viti na Meza vilivyotolewa na Serikali kupunguza uhaba maskulini

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Kushoto akimkabidhi Meza na Viti Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Kitope ikiwa ni Mgao wa Vikalio vilivyotolewa na Serikali kupunguza uhaba wa Vikalio katika Skuli za Unguja na Pemba.
 Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Vuga Mkadini Bibi Khadija Hamad Khamis akipokea Viti na Meza kutoka kwa Balozi Seif ikiwa ni Mgao wa Vikalio vilivyotolewa na Serikali kupunguza uhaba wa Vikalio katika Skuli za Zanzibar.
 Baadhi ya Wananchi wa Shehia zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda wakimsikiliza Balozi Seif  hayupo pichani wakati wa hafla ya kugawa Meza na Viti kwa Skuli zilizomo ndani ya Jimbo hilo vilivyotolewa na Serikali Kuu.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikalia moja ya Kiti vilivyotolewa na Serikai kwa Skuli za Zanzibar kukijaribu umadhubuti wake wakati wa hafla ya kukabidhi.
Baadhi ya Meza na Viti vilivyonunuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kupunguza uhaba wa vikalio kwa Wanafunzi wa Skuli za Unguja na Pemba.
Picha na –  OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis , OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  ameonya kwamba uvamizi wa ujenzi holela wa Majengo ya Kudumu katika Eka za Serikali walizopewa Wananchi  Mwaka 1964 kuendeleza Kilimo ukiachiliwa kuendelea unaweza kuleta athari katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema Masheha pamoja na Watendaji wa Halmashauri za Wilaya lazima waelewe kwamba watabeba dhima dhidi ya kasi hiyo ya ujenzi inayofanyika ndani ya Macho yao  ambayo inakwenda kinyume na ile Falsafa ya Muasisi wa kwanza wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Balozi Seif Ali Iddi ametoa onyo hilo wakati akizungumza na Wananchi, Kamati za Skuli pamoja na Walimu waliomo ndani ya Jimbo la Mahonda alipofanya ziara maalum ya kukabidhi Meza na Viti kwa Skuli Nne za Jimbo hilo ikiwa ni mgao wa Serikali kufuatia Kampeni Maalum ya kuondosha tatizo la Vikalio kwa Skuli za Zanzibar.
Skuli hizo ni pamoja na Mahonda iliyopata Meza 45, Viti 135, Kitope iliyopata Meza 45 na Viti 137, Vuga Mkadini iliyopata Meza 30 na Viti 90 pamoja na Skuli ya Fujoni iliyopata Meza 30 na Viti 90.
Alisema tamaa ya baadhi ya Viongozi wa Halmashauri pamoja na Shehia kwa kuhusika katika masuala ya uuzaji wa ardhi hasa maeneo ya Eka Tatu Tatu yataumiza Kizazi cha sasa na Zaidi kile kijacho kwa kukosa maeneo ya kuendeleza Miradi ya Maendeleo ndani ya Sekta ya Kilimo.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba wapo baadhi ya Watu walioamua  kuendeleza Kampeni ya kutumia fedha nyingi kwa kununua Eka za Serikali zilizotolewa kwa Kilimo wakiwa na Mkakati Maalum wa kujirejeshea Maeneo hayo kwa mlango wa Nyuma wakati Serikali Kuu tayari imeshayataifisha Mnamo Mwaka 1964.
Alibainisha wazi kwamba Serikali haitasita kumchukulia hatua za Kisheria Mtu  au Kiongozi ye yote yule atakayebainika kujihushisha na masuala ya uuzaji wa Eka za Serikali hatua itakayokwenda sambamba na kunyang’anywa maeneo hayo Mtu aliyeuziwa na kuyarejesha Serikalini.
Akizungumzia suala la Vikalio vya Wanafunzi Maskulini  Unguja na Pemba, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi hao wa Shehia mbali mbali zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwapunguzia bughdha Wanafunzi wake kutokana na changamoto kubwa inayowakabili ya uhaba wa Vikalio.
Balozi Seif alisema kitendo cha Wanafunzi kuendelea kusoma madarasani kwa kutumia mapaja badala viti na Meza huviza Maendeleo ya Elimu hasa ikizingatiwa kwamba Mwanafunzi wa Karne ya 21 lazima aende na wakati wa sasa wa mfumo wa Sayansi na Teknolojia.
“Karne ya 21 ya Sayansi na Teknolojia kamwe haifanani ya mazingira ya Mtoto kupata Elimu katika mazingira  ya Karne ya 18 walioyokuwa wakisoma kwenye Miti na sehemu za wazi”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuagiza Vifaa hivyo kutengenezwa nje ya Nchi umefanywa kwa makusudi ili viwahi mahitaji sambamba na kupunguza gharama kwa vile upatianaji wa mali ghafi nyingi za mbao hapa Nchini ungeleta changamoto.
Balozi Seif Ali Iddi alizikumbusha Kamati za Uongozi za Skuli zilizopata na zile zitakazopata mgao huo kuhakikisha kwamba Viti na Meza hizo zinasimamiwa vyema ili ziendelee kutoa huduma kwa Wanafunzi katika kipindi kirefu kijacho.
Akigusia agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein la kuruhusu Skuli zote Nchini zirejee kuendelea na masomo yao kama kawaida kuanzia Tarehe 29 Mwezi huu, Balozi Seif  aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu pamoja na skuli husika kuhakikisha kwamba Wanafunzi wote wanazingatia muongozo wa Wataalamu wa Afya wakati wote wa Masomo.
Balozi Seif alisema Virusi vya Corona bado vipo Nchini. Hivyo Jamii hasa Wanafunzi wanapaswa kuufuata muongozo huo wa Afya kwa kunawa Mikono kwa Maji ya kutiririka kabla ya kuingia Madarasani pamoja na kuvaa Maski wakati wakiendelea na masomo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda anayemaliza muda wake wa utumishi  aliwashukuru Wananchi wote wa Jimbo la Mahonda kwa ushirikiano mkubwa waliompa wakati wa Utumishi wake  wa Miaka Mitano.
Alisema Wananchi na hasa Wanachama pamoja na Viongozi wa Jimbo hilo lazima watafakari kwa kina kumpata Mtumishi atakayeweza kuendeleza Mikakati   anayoiacha kwa kuwaletea Maendeleo ya Kudumu Wananchi wa Jimbo la Mahonda.
Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unaguja Nd. Iddi Ali Ame alisema wakati umefika kwa Walimu wa Skuli zilizomo ndani ya Mkoa huo kuurejeshea Heshima yake Mkoa huo kwa matokeo mazuri ya ufaulu wa Wanafunzi.
Nd. Iddi alisema Kipindi cha Miaka Mitatu iliyopita Mkoa huo pamoja na Wilaya zake zimekuwa zikishuhudiwa kuwa na Matokeo hafifu ya Wanafunzi wake jambo ambalo kwa sasa Viongozi wake hawapendi kulishuhudia kutokana na nguvu kubwa ya Serikali iliyofanywa ya kuwapunguzia changamoto zao ikiwemno Vikalio vya Skuli.
Wakitoa Shukrani zao Walimu Wakuu na Wenyeviti wa Kamati za Skuli hizo wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutekeleza ahadi yake iliyotoa ya kuondosha Changamoto la Vikalio lililokuwa likiwakabili Wanafunzi hawa wale wa Skuli za Msingi.
Walisema mgao huo wa Meza na Viti kwa kisi kikubwa utachangia kupunguza uhaba wa Vikalio kwenye Majengo yao ya Skuli jambo ambalo kwa upande mwengine litatoa utulivu kwa Walimu pamoja na Wanafunzi wakati wa masomo yao.
Katika ziara hiyo ya ugawaji wa Meza na Viti ndani ya Skuli za Jimbo la Mahonda Balozi Seif pia alipata wasaa wa kulikagua Daraja lililojengwa kwenye bara bara ya Kazole kuelekea Matetema lililovunjika kutokana na Mvua kubwa za masika zilizopita hivi karibuni.
Balozi Seif aliwaeleza Wananchi wa maeneo hayo kwamba ile ahadi ya Serikali iliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein ya kuijenga Bara bara hiyo bado iko pale pale na itatekelezwa kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.