Habari za Punde

Vijana watahadharishwa kutumiwa na wanasiasa

 Naibu Waziri wa Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Lulu Msham Abdalla akifungua Kikao cha Baraza la Watendaji  huko Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe Zanzibar. 
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana,Utamaduni.Sanaa na Michezo Amour Hamil Bakari akizungumza katika Kikao cha ufunguzi cha Baraza la Watendaji  huko katika Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe Zanzibar.
 Katibu Mtendaji Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Faraji Abdalla akizungumza katika ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Watendaji  huko katika Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe Zanzibar.
(Picha na Kijakazi Abdalla  Maelezo)  
Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Lulu Msham Abdalla akiwa naWajumbe wa Kamati ya Baraza la Vijana Zanzibar katika kikao cha Ufunguzi wa Baraza la Watendaji huko Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe Zanzibar.

Na Kijakazi Abdalla            Maelezo   
      
Naibu Waziri wa Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Lulu Msham Abdallah amewaasa vijana kuacha kutumiwa  na wanasiasa kwa lengo la kujipatia maslahi yao binafsi.

Waziri Lulu ameyasema hayo katika Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe wakati akifungua kikao cha Barazaa la Watendaji la Vijana Zanzibar.

Amesema mara nyingi wanasiasa wamekuwa wakiwatumia vijana katika kuvunja amani hivyo ni vyema kujiepusha na viongozi hao wasiopenda maendeleo na amani ilopo nchini
Amefahamisha kuwa ni rahisi kuvunja amani iliyopo lakini ni vigumu sana kuirejesha hivyo amewasisitiza vijana kuepuka kujiingiza katika siasa za chuki zenye kupinga na maendeleo.

Naibu Waziri amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali  za uongozi  pamoja na kuchagua viongozi walio bora kwa lengo lakuleta maendeleo ya Taifa.

Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Amour Hamil Bakari amesema Serikali itaendelea kutafuta fursa mbalimbali kwa Baraza la Vijana ili Baraza hilo liweze kujiendesha na kujitegemea.

Aidha ameeleza kuwa wataendelea kutayarisha sera, sheria ,kanuni na miongozo mbalimbali inayowaruhusu vijana kufanya maamuzi pamoja na kuyafanyia marekebisho ili kukidhi haja.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Baraza la Vijana Khamis Faraji Abdalla ameihakikishia Serikali kuwa watahakikisha vijana wanaleta maendeleo ya Taifa na hawatumiwi vibaya na wanasiasa katika kuvunja amani ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.