Habari za Punde

Wakati Umefika Wanawake Kujitokeza Kuwania Nafasi za Uongozi -Balozi Seif.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi kadi ya Uanachama wa CCM aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chake chake kupitia CUF Mh. Kaiza YussuF Makame baada ya kuamua kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa Kusini Pemba wakiendelea na Kikao chao ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba ambao ulipata Baraka ya kuhutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu  ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chake chake kupitia CUF Mh. Kaiza YussuF Makame akila kiapo cha utii baada ya kujiunga na CCM na kupewa Kadi rasmi ya Uanachama.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wanawake Nchini kujitokeza kuwania nafasi mbali mbali za Uongozi ndani ya Majimbo yao ili kujiwekea nguvu zaidi za kuelekea kwenye asilimia 50% katika maeneo ya maamuzi.
Alisema tabia ya Wanawake waliowengi Nchini kukimbilia kwenye nafasi za Viti Maalum endapo hawataachana nayo inaweza kuwalete usumbufu kwa kusingizia mfumo Dume sambamba na kuviza ile kiu yao ya kufikia malengo ya Hamsini kwa Hamsini na Wanaume.
Akizungumza na Wajumbe wa Halmashauriu Kuu ya CCM ya Mkoa wa Kusini Pemba kwenye Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake chake Pemba Balozi Seif alisema wapo baadhi ya Wanawake wamejihalalishia zile nafasi za Viti Maalum kitendo ambacho kinawanyima fursa Wanawake wenzao hasa wale Vijana.
Balozi Seif alisema Taifa kupitia Sekta ya Elimu tayari imeshazalisha wanawake wengi wenye uwezo wa Kitaaluma na nguvu za kuwatumikia Wananchi lakini wengi kati yao wanashindwa kujitokeza kwa kuhofia nguvu kubwa waliyonayo Wanaume pamoja na udhaifu wa Kijinsia Majimboni.
“  wanawake lazima wathubutu kuingia katika mchakato wa Majimbo badala ya kulemaa katika Viti Maalum na hii huchangia kuondoa wale wenye tabia ya kununa pale wanaposhindwa katika uchaguzi”. Alisema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Balozi Seif aliwapongeza wale wanasiasa wa Vyama vyengine vya upinzani walioamua wenyewe kujiunga  na wengine kurejea Chama cha Mapinduzi kilichoonyesha msimamo wake wa kusimamia Ilani ya Uchaguzi ambayo hivi sasa kila Mwananchi amekuwa shahidi wa Maendeleo hayo.
Aliwahakikishia wale wote waliojiunga na Chama cha Mapinduzi kutokana na Sera zake inazotekelezeka watapewa ushirikiano mkubwa utakaosaidia kuongeza nguvu za CCM katika kuwatumikia Wananchi waliowengi bila ya kujali tofauti za Kidini na Kisiasa.
Akizungumzia suala la ajira Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kwa uwezo wake kujenga mazingira bora yatakayowezesha kupatikana kwa fursa za ajira miongoni mwa Vijana ambao kwa sasa wengi kati yao wanazurura Mitaani.
Aliwakumbusha Viongozi wenye dhamana ya kuhusika na masuala ya ajira hasa Maafisa Wadhamini Kisiwani Pemba wazingatie kwa kina namna watakavyoweza kuwasaidia Vijana walioamua kutumia muda wao mkubwa katika shughuli za kujitolea.
Alisema ni vyema Jamii ikaelewa kwamba Ofisi yake ambayo kwa sasa imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya Vijana wanaohitaji Ajira haina fursa hiyo kwa vile utaratibu wa ajira unasimamiwa na Taasisi inayohusika na masuala ya Utumishi wa Umma Serikalini.
Katika Kikao nhicho Mjumbe huyo wa Kamati Kuu Balozi Seif alimpokea aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chake Chake kupitia Chama cha Wananchi {CUF} Mh. Kaiza Yussuf  ambae aliamua rasmi kujiunga na Chama cha Mapinduzi .
Akitoa salamu mara baada ya kukabidhiwa Kadi ya CCM pamoja na kula kiapo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chake Chake kupitia Chama cha Wananchi {CUF} Kaiza Yussuf Makame alisema amefikia uamuzi wa kujiunga na Chama cha Mapinduzi kutokana na Ilani yake kutekelezeka na kuwagusa Wananchi wa aina zote Nchini.
Mh. Kaiza alisema haamini kama kuna upinzani wa Kisiasa Nchini Tanzania katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita na uamuzi wake wa kuacha upinzani umempa faraja kubwa itakayojenga Historia Mpya kwake kwa kukabidhiwa Kadi ya CCM ndani ya Kikao Kizito cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa.
Alitahadharisha kwamba Wananchi wa Kisiwa cha Pemba wanapaswa kufikiri wenyewe katika maamuzi yao ya kuwachaguwa Viongozi na kukataa kuburuzwa kwa kuchukuwa fikrta za Watu wengine wenye maslahi binafsi kwani yeye tayari ametoka baada kuelewa upinzani wa ndani wa Kisiasa.
Mh. Kaiza alifahamisha kwamba mambo yaliyo ndani ya upinzani hayapendezi kutokana na kukosa uwajibikaji katika masuala ya Maendeleo na nguvu kubwa ikielekezwa zaidi kwenye ushindani wa Kisiasa.
Akitoa Taarifa ya Mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa Kusini Pemba Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa huo Nd. Mohamed Khalfani alisema Uongozi wa CCM wa Mkoa huo umejipanga katika kuhakikisha unafanywa vyema kwenye matokeo ya Uchaguzi Mkuu  ujao wa Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Nd. Mohamed alisema mipango hiyo inakwenda sambamba na kumjengea Heshima Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr.Ali Mohamed Shein kutokana na usimami wake wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi uliotia fura kipindi cha Miaka Mitano.
Akigusia Miradi ya Maendeleo na Kiuchumi Mkoani humo Nd. Mohamed Khalfan alieleza kwamba Mkoa wa Kusini Pemba umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya Bara bara za ndani pamoja na uhaba wa huduma za Maji safi na salama.
Alisema mgao wa Maji kwa Wananchi unaofanywa na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} unafanywa kutokana na Mamlaka hiyo kukosa Matangi ya kuhifadhia Maji na matokeo yake mashine zinazotumika kusukumia Maji hayo zinashindwa kutoka huduma kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.