Habari za Punde

ZEC itamuandikisha kila mwenye sifa atakaefika kituoni




Na Jaala Makame Haji- ZEC

Makarani wa Uandikishaji katika Vituo vya Uandikishaji wamesisitizwa kuwa makini  na kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo ya Uchaguzi ili kutoa huduma bora wakati zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura likiendelea katika vituo vya uandikishaji kwa Mikoa ya Unguja.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar THABIT IDAROUS FAINA akifungua mafunzo ya siku moja kwa Makarani wa uandikishaji huko Elimu mbadala alisema matarajio ya Tume ni kuandikisha idadi kubwa ya wananchi waliokosa fursa hiyo hapo awali hivyo ni vyema makarani hao kuwa makini pale wanapotekeleza majukumu yao katika vituo vya uandikishaji.

Alisema kwa kuwa Tume inadhamira ya Kumuandikisha kila mwenye sifa atakayefika kituoni kuomba kuandikishwa ama kuhakiki taarifa zake ni vyema makarani hao kufanyakazi kwa bidi ili kufikisha dhamira hiyo iliyowekwa na Tume ili Wazanzibari waliowengi wapate kushiriki katika hatua zote za mchakato wa Uchaguzi.

Mkurugenzi FAINA alisema, Tume imekamilisha kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kwa Mikoa yote ya Pemba kazi ambayo ilianza tarehe 30/5/2020 na 31/5/2020 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba na kumalizika Mkoa wa Kusini Pemba tarehe 01/6/2020 na 2/06/2020 bila kutokezea changamoto yoyote ambayo ingeathiri mfumo mzima wa uandikishaji.

Ndugu, FAINA alifafanua kuwa, kwa upande wa Unguja Kazi hiyo ya Uandikishaji itaanza katika Mkoa wa Kaskazini Unguja tarehe 5 na 6/6/2020 na kuendelea Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 7 na 8/6/2020, tarehe 9 na 10/6/2020 Wilaya ya Magharib A na Wilaya ya Magharibi “B” na itamalizika katika Wilaya ya Mjini tarehe 11 na 12/6/2020

Alisema kukamilika kwa kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura ni hatua muhimu ambayo itaiwezesha Tume kuweka wazi Daftari, kugawa vitambulisho vya kupigia kura na kukamilisha kazi ya uchaguzi mkuu. 2020

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo juu ya utaratibu na miongozo ya kazi ya uandikishaji Mkuu wa Kurugenzi ya Mifumo ya Uchaguzi Tume ya uchaguzi ya Zanzibar MWANAKOMBO MACHANO ABUU alisema kazi ya uandikishaji itafanyika kwa muda wa siku mbili kwa kila kituo cha uandikishaji na kuwataka kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika zoezi la awali.

Baadhi ya Makarani wa uandikishaji waliahidi kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi sambamba na kuwataka wananchi wenye sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutodharau fursa hiyo ambayo itawapa haki ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.