Habari za Punde

DKT. KALOKOLA NA NDOTO ZA URAIS 2025

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
Dkt. Mzamini Kalokola Mwanasiasa mkongwe na Kada wa Chama Cha Mapinduzi jana amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Ubunge jimbo la Tanga mjini na kusisitiza kufanya utekelezaji wa mambo ambayo hayajatekelezwa katika jimbo hilo.

Dkt. Kalokola ambaye aliwahi kuwania kiti cha Urais mwaka 2015 ameeleza kwamba kilichomsukuma kuchukua fomu ya kuwania kiti hicho ni uchungu alionao kwa jimbo hilo ambalo anadai yapo baadhi ya mambo hayajafanyiwa utekelezaji hivyo atakapopata ridhaa kutoka kwa wananchi atafanya mageuzi na kulifanya jimbo hilo kuwa la mfano ambapo pia atakuwa amepata nafasi nzuri itakayompelekea kuwania Urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Nimepania kugombea nafasi hii na endapo wananchi watanichagua nitahakikisha nafanya utekelezaji katika sehemu zote ambazo hazijatekelezwa awamu iliyopita, Nina uchungu sana na jimbo la Tanga mjini pamoja na wananchi wake, na hii ni tiketi ya kunipeleka kwenye kinyang'anyiro cha Urais mwaka 2025 nimepania kuchukua fomu na kugombea kiti hicho uchaguzi mkuu wa 2025 utakapowadia" alisema Kalokola.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Tanga Salimu Kidima hadi kufikia hapo jana julai 15 tayari watia nia ya kugombea kiti cha ubunge katika Jumbo la Tanga mjini walifikia 11 ambapo kati yao alikuwepo mwanamke mmoja na wanaume kumi na kwamba leo mchakato unaendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.