Habari za Punde

MKAPA: MSHUMAA ULIOZIMIKA GHAFLA: TUTAKUKUMBUKA DAIMA MZEE WA UKWELI NA UWAZI


Na.Jonas Kamaleki                                                                                           
Ni majuzi Mzee wetu Mpendwa, Benjamin William Mkapa ukiwa Dodoma uliongoza Kikao cha Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa umahiri mkubwa, kumbe ndo ulikuwa ukituaga! Wengine tulijua kuwa utapiga kura Oktoba na kushiriki katika sherehe za kumwapisha Rais atakayekuwa amechaguliwa, kumbe sivyo, Mkapa umetutangulia ghafla kwenda kwa Muumba wetu. Burian Mzee wetu wa Uwazi na Ukweli.
Tutakukumbuka kwa uongozi wako uliotukuka na unyenyekevu uliokuwa nao kwa kuwaheshimu wakubwa kwa wadogo tangu ukiwa Pugu Sekondari, Chuo Kikuu Makerere hata ulivyorudi nchini na kuendelea na majukumu yako kwa uzalendo mkubwa. Kwenye Tasnia ya Habari msiba huu ni pigo kwani Mzee Mkapa alikuwa  Mhariri mahiri wa The Nationalist hadi Daily News. Waliofanya nawe kazi akiwemo mwandishi nguli, Jenerali Ulimwengu anasema kuwa kwenye chumba cha habari Mzee Mkapa alikuwa mwalimu na mlezi.
Mkapa atakumbukwa kwa kupinga na kupambana na rushwa. Katika kudhihirisha hilo, Mzee Mkapa aliunda Tume ya Warioba kuchunguza vitendo vya rushwa na kutoa mapendekezo. Hakuishia hapo kwani aliunda Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) ambayo baadae ikaja kujulikana kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Wakati Mzee Mkapa anaingia madarakani alikuta uchumi wa nchi unayumba, hivyo alibuni mbinu kadhaa za kufufua uchumi. Moja ya mbinu aliyoibuni kiongozi huyo ni kuunda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kubuni vyanzo vya mapato na kukusanya kodi.
Hakuishia hapo bali alitilia mkazo ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na kuboresha usafiri wa majini. Katika hili alianzisha Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Wakala ambao ulijenga barabara kwa kiwango cha lami za kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara. Kwenye hotuba zake za kila mwezi hakuchoka kujinadi na kazi yake ya kuboresha miundombinu. Mzee Mkapa alisikika akisema, “Tumeboresha miundombinu, tumejenga shule za msingi na sekondari”.
Mkapa alifanikisha kuunda Taasisi za udhibiti, Taasisi na mifuko ya kuinua Wananchi kama  Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) na Mpango wa Kurasimisha Biashara na Mali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
Jambo jingine ambalo watanzania wanapaswa kulijua au kulikumbuka ni lile la kumuibua Jemedari Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi chini Waziri Anna Abdallah mwaka 1995.
Ukweli na Uwazi ndio ilikuwa Kaulimbiu maarufu ya Mpendwa wetu Benjamin William Mkapa. Aliamini kuendesha Serikali yake kwa ukweli na uwazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.