Habari za Punde

Ulipaji wa Ada Hatua Muhimu Kumfanya Mwanachama Kuwa Hai Ndani ya Chama Cha Mapinduzi - Mhe Samia.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi, hafla katika ukumbi wa Utengamano ‘Peace Building Center’ uliopo Welezo wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.

Na.Mwandishi Wetu.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa CCM mkoa wa Magharibi kuwahimiza wanachama kulipa ada za Chama.

Amesema ulipaji wa ada ni hatua muhimu ya kumfanya mwanachama kuwa hai ndani ya chama cha mapinduzi hivyo kila mwanachama anatakiwa kutekeleza wajibu huo.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi katika ziara yake ambayo anayoifanya katika mikoa ya CCM kwa upande wa Unguja hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Utengamano ‘Peace Building Center’ uliopo Welezo Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.

Makamu wa Rais huyo aliongeza kuwa katika mkoa huo kiwango cha malipo ya ada ya wanachama yapo chini na kwamba hairidhisha.

Alisema kuna baadhi ya viongozi na wanachama wamekuwa na tabia ya kulipa ada kila ikikaribia kipindi cha uchaguzi jambo linalohatarisha uhai wa uanachama wao.

Mbali na hilo, Makamu wa Rais huyo alisema kuna tabia ya baadhi ya viongozi wanajitafutia kura zao binafsi na si za chama na kwamba hawafanyi kazi za chama badala yake wanajiandaa kutafuta nafasi za uongozi kwenye kuelekea uchaguzi.

Aliwataka viongozi hao kukisemea chama na kukiombea kura na si kujiombea kura binafsi  na jambo hilo linachangia kudhorotesha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

" Viongozi,watendaji na wanachama wote muendelee kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha mnaanda vyema mazingira rafiki ya Chama kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.", Mhe.Samia alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja, Mgeni Mussa Haji alisema uongozi wa mkoa huo umejipanga vizuri katika kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Alisema CCM imejipanga kushinda katika uchaguzi huo kwenye shehia zote za mkoa wa Magharibi ikiwemo wadi 26 na majimbo 13.

Katibu huyo alisema uongozi wa mkoa huo umejipanga kimkakati katika kuhakikisha majimbo yote yanakwenda CCM katokana na kuwa upo vizuri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.