Habari za Punde

China yaipatia Zanzibar msaada wa dawa na vifaa vya tiba vya thamani ya zaidi ya Mil 500

 Mkurugenzi Bohari Kuu ya dawa Zanzibar Zahrani Ali Hamadi akiwakaribisha viongozi waliofika katika makabidhiano ya dawa yaliyofanyika Ofisini kwake Maruhubi Mjini Zanzibar.
 Balozi mdogo wa China Zanzibar Xie Xiaowu akimkabidhi Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed msaada wa dawa na vifaa tiba uliotolewa na Serikali ya China, hafla iliyofanyika Bohari Kuu ya dawa Maruhubi Mjini Zanzibar.
 Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed na Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu wakisaini hati ya makabidhiano ya dawa na vifaa tiba kutoka Serekali ya China.
 Baadhi ya waalikwa na wafanyakazi wa Bohari Kuu ya dawa Zanzibar wakishuhudia makabidhiano ya dawa na vifaa tiba zilizotolewa na Serekali ya China.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Bohari Kuu ya dawa (hawapo pichani) baada ya makabidhiano ya dawa yaliyofanyika Ofisini Maruhubi.
Picha na Makame Mshenga. 

Na Ramadhani Ali   -  Maelezo                     04.08.2020
Zanzibar imepokea msaada wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni miatano kutoka Serikali ya Watu wa China wenye lengo la kuimarisha huduma za afya nchini.
Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xaiowu alikabidhi msaada huo kwa Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed katika hafla iliyofanyika Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi.

Balozi Xie alisema msaada huo wenye dawa za maradhi tofauti na vifaa tiba vikiwemo vya kujilinda na maradhi ya Korona ni kielelezo cha uhusiano mzuri kati ya Wananchi wa China na Zanzibar.
Alieleza kuwa China itaendelea kuisaidia Zanzibar katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya afya ili iweze kupiga hatua ya maendeleo kwa urahisi.

Balozi wa China amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kufuata maagizo ya viongozi na wataalamu wa afya wakati wa kipindi cha Korona na kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi na hatimae kuyadhibiti.

Akipokea msaada huo Waziri Hamad Rashid Mohamed aliishukuru Serikali ya China kwa misaada yake inayotoa kwa Zanzibar hasa katika kuimarisha huduma za afya.

Alisema wakati Zanzibar ilipopata maradhi ya Korona China ilikuwa nchi ya kwanza kutoa vifaa na wataalamu waliosaidia katika kupambana na maradhi hayo.

Waziri Hamad alisema baadhi ya dawa alizopokea zinahitajika sana wakati huu hasa katika wodi za wazazi na wodi ya wagonjwa wa matatizo ya figo.

Alisema dawa na vifaa tiba hivyo vitasambazwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja, hospitali za Wilaya na vituo vyote vya afya Unguja na Pemba ili kuongeza ufanisi wa kuwahudumia wananchi.
Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa Zahran Ali Hamad alisema msaada wa dawa na vifaa tiba vilivyotolewa zitaongeza ufanisi katika sehemu ya upasuaji na zitasaidia kupoteza damu nyingi wananchi watakaopatwa na ajali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.