Habari za Punde

JKT kusajili wachezaji wane kuongea nguvu kikosi

Na Mwandishi wetu


KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya JKT Tanzania Abdalla Bares amesema kuwa anakusudia kusajili wachezaji wane ili kuongezea nguvu kikosi chake hicho ambacho kinashiriki ligi kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Bares alisema kuwa kati ya wachezaji hao mmoja atatokea visiwani na waliobakia ni kutoka katika klabu za Tanzania Bara.

“Zanzibar nimewaona wachezaji wanne washambuliaji lakini kati ya hao mmoja tu ndie tutakae msajili kwa ajili ya kikosi chetu”, alisema Bares.

Alieleza kuwa tayari mazungumzo kwa ajili ya wachezaji hao yanaendelea wote wameonesha kukubali kujiunga na timu hiyo.

Alisema kuwa nafasi ambazo watasajili katika timu yao msimu huu ni mlinda mlango, walinzi wa kushoto na kulia na mshambuliaji mmoja.

Hata hivyo alisema kuwa kupatikana kwa wachezaji hao kutaongeza chachu ya ushindani katika timu yao hiyo ambayo msimu uliomalizika ilishika nafasi ya sita katika timu 20 zilizokuwa zikishiriki ligi hiyo.

Akizungumzia ligi hiyo iliyomalizika alisema kuwa ilikuwa ngumu na ilikuwa na mvuto kutokana na kila mmoja kufanya kazi kwa upande wake ili kupata matokeo mazuri.

Hata hivyo alisema kuwa wamejipanga vizuri kwa ajili ya msimu ujao na ndio maana wakataka kusajili idadi ya wachezaji ambao anauhakika wataongeza nguvu vizuri kikosini hapo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.