Habari za Punde

Kazi Kubwa ya SMZ Ambayo Imechaguliwa na Wananchi ni Kuwahudumia Kwani Wao Ndio Walioiweka Madarakani -Dk.Shein.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiwahutubia Wananchi wa Pemba katika hafla ya ufunguzi wa Hoteli ya Mkoani ya ZSSF, baada ya kukamilika ujenzi wake mkubwa, mkutano huo umefanyika katika uwanja wa zimamoto Mkoanui Pemba leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kazi kubwa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imechaguliwa na wananchi ni kuwahudumia kwani wao ndio waliyoiweka madarakani.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika uwanja wa Zimamoto Bandarini, Mkoani Pemba wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka jiwe la Msingi afisi za ZSSF Tibirinzi, Afisi za ZRB Gombani pamoja na kuzindua Hoteli ya Mkoani ambayo imefanyiwa ukarabati mkubwa.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kazi  ya Serikali ni kuwaletea maendeleo wananchi na kwa hivi sasa Serikali ya Awamu ya Saba imekuwa ikifanya hivyo kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuwasogezea huduma muhimu za kimaisha.

Rais Dk. Shein alisema kuwa tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kutekeleza ahadi zilizoahidiwa na Chama Cha ASP.

Alisema kuwa hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza ahadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilizoziahidi katika Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wananchi.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kuzinduliwa kwa hoteli ya Mkoani  ambayo ni miongoni mwa hoteli za Serikali zilizojengwa mwanzoni mwa miaka 1970 sambamba na ya Chake Chake na ya Wete ambazo zilikuwa chini ya Shirika la Utalii Zanzibar ambalo kwa sasa halipo ilikuwa ni kuwahudumikia wananchi wa ndani na nje ya nchi.

Alisema kuwa hoteli ni kwa ajili ya watu mbali mbali wakiwemo watalii na wananchi ambao wanapata huduma za kitalii ambayo hatua hiyo inaimarisha utalii wa andani.

Aidha, Rais Dk. Shein aliwanasihi wananchi nao kwa upande wao kujenga hoteli kwani tayari ZSSF imeonesha njia na Serikali imewaamini huku akisisitiza kuwa Makampuni, Mashirika pamoja na Wajasiriamali nao wana nafasi ya kufanya hivyo.

Alieleza kuwa Serikali zilizopita za Kikoloni hazikuimarisha sekta ya Kitalii na badala yake Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeimarisha kwa kiasi kikubwa sekta hiyo tokea Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kupelekea kuongezeka kwa hoteli na wageni.

Kwa upande wa hatua za Serikali za kujenga jengo la Afisi za ZRB Pemba, Rais Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukusanya kodi kwa ajili ya mapato ya Zanzibar.

“Tukisema wengine wanaguna na wagune mpaka wagunuke sisi tunasonga mbele kubwa ninalowaambia wananchi wa Mkoani wajiandae kupokea wageni....Serikali imeridhika na mimi mwenyewe nimeridhika”,alisema Dk. Shein.

Aliongeza kuwa ZRB imefanya kazikubwa na ndio maana uchumi wa Zanzibar umeimarika na hivi sasa kufikia uchumi wa kati kama ilivyo kwa upande wa Tanzania Bara ambapo hivi sasa uchumi wa Zanzibar umekwua kwa asilimia 7.

Alisema kuwa hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya mamabo yake wenyewe wka kutegemea fedha zake inazozikusanya.

Pamoja na hayo, Kwa upande wa afisi za ZSSF zinazojenwga huko Tibirinzi, Rais Dk. Shein alisema kuwa kjengwa kwa afisi kutasaidia kwa kiasi kikuwba kuwawekea mazingira mazuri wafanyakazi.

Rais Dk. Shein alisema kuwa ZSSF imeweza kuanzisha miradi mbali mbali mikubwa Unguja na Pemba hatua ambayo imepelekea kukua na kuimarika kwa miji yote ya Zanzibar.

Mapema Rais Dk. Shein alipokuwa akiweka mawe ya msingi katika Afisi za ZSSF huko Tibirinzi na ZRB huko Gombani alisema kuwa miradi kadhaa inatarajiwa kuendelezwa na mengine kuanzwa ukiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba.

Katika mkutano huo huko Mkoani, Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa alieleza mafanikio yaliopatikana kutoka Mfuko wa ZSSF na kutoa historia ya ujenzi wa hoteli kisiwani humo.

Balozi Ramia aliwaondoa wasiwasiw ananchi na kuwaeleza kwamba fedha zao zilizoko katika Mfuko wa Jamii wa ZSSF ziko salama.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa alisema kuwa maendeleo yameendelea kupatikana hapa nchini katika miaka 10 ikiwemo katika uwekezaji wa Ofisi za Serikali na Taasisi zake.

Alisema kuwa kwa upande wa hoteli ya Mkoani, hoteli hiyo ilifnguliwa Januari 9, 1974 na kutoa huduma kwa miaka 1970 hadi 1990 ambapo kutokana na kukosa matunzo yanayopaswa hoteli ilichakaa na kusita huduma zake.

Alieleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein Baraza la Mapinduzi liliamua kuikabidhi hoteli hiyo kwa ZSSF kwa lengo la kuifufua na kuiendeleza kiuchumi kama lengo la awali kuijenga kwake ambapo makabidhiano rasmi yalifanyika Oktoba 19 mwaka 2018.

Alisema kuwa Kampuni ya ARQES AFRICA ya Dar es Salaam ilibarikiwa kazi za kuandaa mchoro mpya kwa kuzingatia hali ya jengo lenyewe pamoja na mahitaji ya ZSSF ambapo Kampuni ya ukandarasi ya BENCHMARK ENGENEERING ilibarikiwa Kandarasi ya kukarabati jengo na kulikabidhi Julai 4, 2019.

Alisema kuwa ujenzi huo umezingatia watu wenye ulemavu na mahitaji maalum ikiwemo “lift” ambapo matengenezo ya jengo hilo yamegharimu jumla ya TZS Bilioni 4 ambayo yalichukua miezi minane.

Aliongeza kuwa Afisi za ZSSF zinazojengwa Tibirinzi mbele ya Kiwanja cha Kufurahishia watoto cha Umoja Kampuni ya ARQES AFRICAN ya Dar es Salaam ndio iliyobarikiwa  zabuni ya kuandaa michoro ya jengo hilo la ghorofa tatu ambapo ujenzi umefanywa na kampuni ya Quality Building Contractors ya Zanzibar.

Alisema kuwa ujenzi huo umegharimu TZS bilioni saba na mia tisa na thelathini milioni hadi Juni 30,2020 na jumla ya TZS bilioni mbili na milioni mia mbili na arobaini na tisa zimeshalipwa sawa na asilimia 28.56 ya malipo yote kwa mradi mzima.

Sambamba na hayo, jengo la ghorofa nne la ZRB Gombani ambalo mkataba wake ni wa mwaka mmoja na ulitiwa saini mwezi Disemba 2019 na jengo linatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2020 na gharama za ujenzi ni TZS Bilioni 10.6.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.