Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Akabidhiwa Riboti ya Kamati ya Madawati Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikabidhiwa Ripoti ya Kamati ya Madawati Zanzibar na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar. Mhe. Haroun Ali Suleiman, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 30-9-2020. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Madawati Zanzibar wakati wa hafla ya kukabidhiwa Ripoti ya Madawati Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroub Ali Suleiman akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi Ripoti ya Madawati Zanzibar na kushoto Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe.
Wajumbe wa Kamati wa Madawati Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, (hayupo pichani) akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kukabidhiwa ripoti na Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati Zanzibar.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Kamati ya Madawati kwa Skuli za Serikali kwa kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa vikalio.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na baadae kukabidhiwa ripoti na Kamati ya Madawati ya Zanzibar ambayo inaongozwa na  Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman.

Katika pongezi zake hizo Rais Dk. Shein alieleza kuwa kazi kubwa imefanywa na Kamati hiyo na hatimae mafanikio makubwa yameweza kupatikana kwa asilimia 70 ya kupunguza uhaba wa vikalio kwa skuli za Unguja na Pemba.

Rais Dk. Shein ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba na ile ijayo itaendelea kuiitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa vikalio ili kuhakikisha wanafunzi wote wa Msingi na Sekondari kwa Unguja na Pemba hakuna anaekaa chini.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa Kamati hiyo aliyoiunda mnamo tarehe 27 Julai mwaka 2016 imeweza kufanya kazi nzuri ya kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya Nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa vikalio kwa skuli za Zanzibar.

Aliongeza kuwa Kamati hiyo yenye Wajumbe 13 wakiongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman na Makamu Mwenyekiti wake Riziki Pembe Juma imefanya kazi kubwa na kuna kila sababu ya kupongezwa.

Alisema kuwa kila Mjumbe katika Kamati hiyo ana sifa zake hali ambayo imepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa  hatua ambayo imetokana na nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

‘”Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuhakikisha inawapatia wanafunzi wa Skuli za Serikali madawati kwani hapo mwanzo wengi wao walikuwa hawana pa kukaa tumeanza na tumetimiza wajibu wetu”,alisema Rais Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisem kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuendeleza azma ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abaid Amani Karume kutangaza elimu bure hivyo ni vyema na wanafunzi wote wakakaa kwenye vikalio vya uhakika ili juhudi hizo ziende sambamba katika kuimarisha sekta ya elimu.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa elimu bure pamoja na huduma za afya ili kufikia azma ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 huku akitumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe wa Kamati hiyo kwa kuonesha uzalendo wao mkubwa kwa wanafunzi pamoja na nchi yao.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema kuwa  kufuatia makusanyo ya fedha za Madawati TZS Bilioni 7.6 Kamati ilinunua vikalio kwa awamu mbili.

Alisema kuwa Awamu ya kwanza ilifanyika kwa vikalio vya wanafunzi wa Sekondari vilivyojumuisha seti 44,620 ya viti na meza na awamu ya pili ni kwa vikalio vya wanafunzi wa Skuli za Msingi vilivyojumuisha meza 11,560 za wanafunzi watatu watatu na  viti 34,680.

Aliongeza kuwa jumla ya TZS bilioni 5.7 zilitumika katika ununuzi wa vikalio hivyo vya Msingi na Sekondari ambapo kwa awamu ya tatu  kwa wanafunzi wa Sekondari zitatumika bilioni 1.8 na tayari vikalio vimeshaagizwa na vinatarajia kufika nchini mnamo mwezi wa Disemba mwaka huu ambapo vikalio vyote hivyo vitaendelea kusambazwa katika Skuli za Unguja na Pemba.

Kamati hiyo pia, ilipongeza mashirikiano amzuri yaliyofanyika kati yake na Wizara ya Fedha na Mipango na hatimae kupata mafanikio hayo makubwa ndani ya miaka minne ya Kamati hiyo.

Nao Wajumbe hao walimpongeza Dk. Shein kwa kuthubutu na kuibua wazo hilo katika uongozi wake jambo ambalo limeweza kuleta faraja kubwa kwa wanafunzi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar huku Kamati hiyo ikisifu uimara wa vikalio hivyo vilivyonunuliwa nchini China.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki pembe Juma kwa niaba ya Wizara yake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa jitihada zake hizo za kuhakikisha wanafunzi wanapata vikalio changamoto ambayo waliikabili kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa uwepo wa vikalio hivyo umepelekea kuimarika kwa sekta ya elimu kutokana na mazingira mazuri waliyowekewa wanafunzi kwa kuwez akupata vikalio vya uhakika na kuwasaidia katika kujisomea.

Alieleza kuwa hivi sasa hakuna mwanafunzi hata mmoja anaefanya mitihani katika skuli za Serikali anaekaa chini na badala yake wanafunzi wote wanakaa kwenye viti na madawati ya uhakika ambapo aliongeza kuwa mbali ya vikalio pia Serikali imejenga majengo mapya na  ya ghorofa, imeajiri walimu wengi pamoja na kuongeza huduma nyengine katika sekta hiyo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.