Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Yafana Welezo Jijini Zanzibar.

Waziri wa Kazi,Uwezeshaji,Wazee,Wanawake na Watoto Zanzibar Mhe. Moudline Cyrus Castico akihutubia katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ilioadhimishwa katika viwanja vya Makaazi ya Wazee Welezo Jijini Zanzibar leo 1/10/2020.z
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar Bi. Fatma Gharib Bilali akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliofanyika katika viwanja vya makaazi ya Wazee Welezo Jijini Zanzibar leo.

Baadhi ya Wazee wanaoishi Nyumba  za Wazee Sebleni na Wazee wa Welezo wakifurahia wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani zilizofanyika katika viwanja vya Welezo Jijini Zanzibar , wakati Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Zanzibaer Mhe Moudline Castico akiwahutubia katuika viwanja vya Makaazi ya Wazee Welezo leo.

(Picha na Kijakazi Abdalla Habari Maelezo) 




Na.Sabiha Khamis -Maelezo Zanzibar. 01/10/2020

Waziri wa  Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico amesema ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuhakikisha anatoa mchango katika kuwahudumia na kuwatunza wazee.

Hayo ameyasema huko kituo cha kuwatunza Wazee Welezo katika Maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani yanayofanyika kila ifikapo tarehe 01 Oktoba ya kila mwaka.

Amesema jukumu la kuwatunza wazee ni la kila mmoja wetu kwa vile Wazee walitowa mchango mkubwa wakati wa ujana wao katika ujenzi wa Familia na Taifa.

Amesema siku hiyo imetengwa Kimataifa kwa lengo la kuwaenzi na kuwakumbuka Wazee Duniani kote na  kukumbuka michango yao katika kuleta maendeleo katika nchi zao.

Aliendelea kwa kusema siku ya Wazee Duniani hutoa nafasi ya kutathmini hali halisi ya wazee na hatua zinazochukuliwa katika kushughulikia masuala yanayowahusu wazee na changamoto zinazowakabili.

Aidha amesema kuwa Zanzibar ina historia ndefu ya kuwaenzi wazee na kuhakikisha ustawi maalum wa kuwatunza wazee wasiokuwa na jamaa kwa kuwaweka kwenye makaazi pamoja na kuwatunza.

“Tangu Mapinduzi ya 1964, Zanzibar imekuwa  na mfumo maalum wa kuwatunza wazee wasio na jamaa kwa kuwaweka kwenye makaazi na kuwalipa posho” alisema Waziri.

Hata hivyo amesema katika kuhakikisha haki na maslahi ya Wazee yanapata nguvu ya kisheria Wizara imeandaa sheria ya kulinda haki na huduma za ustawi wa Wazee.

Alieleza kuwa kuwepo kwa sheria hiyo itaweza kutoa nafasi ya kulinda na kusimamia haki, ustawi na maendeleo ya wazee wote nchini.

Vile vile Waziri Castico amekemea vitendo vya udhalilishaji kwa wazee na watoto na amelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali kwa wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.

Nae, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Fatma Gharib ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwalipa Pensheni ya kila mwezi kwa wazee waliofika umri wa miaka 70.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu  ni “FAMILIA NA JAMII TUWAJIBIKEk KUWATUNZA WAZEE”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.