Habari za Punde

Ofisi ya Mufti Yatoa Mafunzo Juu ya Amani na Utulivi kwa Maimamu Zanzibar.

Mkuu wa Fatwa Sheikh Othman Jongo akizungumza na Maimamu mbalimbali wa Mkoa wa Kusini Unguja (hawamo pichani) katika mafunzo  kuhusu Amani na Utulivu huko  Ofisi ya Mufti Mazizini Zanzibar. 
Katibu wa Mufti Zanzibar Khalid Mfaume akizungumza na Maimamu mbalimbali wa Mkoa wa Kusini Unguja (hawamo pichani) katika mafunzo  kuhusu Amani na Utulivu katika Ukumbi wa Ofisi ya Mufti Mazizini .
Sheikh Shaaban Batwash , akizungumza na Maimamu mbalimbali wa Mkoa wa Kusini Unguja (hawamo pichani) katika mafunzo  kuhusu Amani na Utulivu huko  Ofisi ya Mufti Mazizini Zanzibar.

Baadhi ya Maimamu wa Mkoa wa Kusini Unguja wakisikiliza kwa makini wakati wa uwasilishwaji wa mada katika mafunzo kuhusiana na Amani na Utulivu yaliyofanyika Ofisi ya Mufti Mazizini Zanzibar. 
Picha na Fauzia Mussa - Maelezo 

Na. Issa Mzee  Maelezo  Zanzibar  01/10/2020

Maimamu na mashekhe nchini wametakiwa kuzitumia nyumba za ibada kwa kuwafundisha waumini maadili mema, ili kuhamasisha amani nchini hasa katika kipindi cha siasa  kwa lengo la kuepuka machafuko.

Akizungumza na Maimamu na Mashekhe mbalimbali wa mkoa wa Kusini Unguja huko Mazizini ,Katibu Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume alisema Maimamu wa misikiti wanauwezo mkubwa wa kutumia taaluma zao katika nyumba za ibada ili kuwahamasisha waumini waendelee kuitunza amani iliyopo nchini.

Alieleza kuwa amani  ndio msingi wa  mambo yote katika maisha kwani bila ya amani harakati za kidini na za maisha kwa ujumla hazitoweza kufanyika katika jamii.

“Imamu na shekhe wa msikiti anauwezo mkubwa wa kuijenga jamii hasa anapokutana na waumini katika hotuba mbalimbali za siku za ijumaa,hivyo ni lazima wazitumie vyema nafasi hizo ili kuijenga jamii kimaadili na kuhamasisha mambo mema”alisema katibu huyo.

Alifafanuwa kuwa pale ambapo jamii itakosa amani baadhi ya watu wasio na maadili huitumia fursa hiyo kwa kufanya vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ubakaji, hivyo ipo haja ya viongozi wa dini kuhamasisha amani katika jamii.

Akitoa ufafanuzi kuhusu wajibu wa Maimamu na Mashekhe katika nyumba za ibada Mkuu wa Fatwa Sheikh Othman Jongo amesema haipaswi kwa nyumba za ibada ikiwemo Misikiti kutumika kuhamasisha fujo ama kufanyika vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake ziwe  nyumba za kujenga jamii katika maadili mema.

“Ni lazima zitolewe hotuba ambazo zitajenga ili kuiweka jamii katika usalama haipaswi kwa imamu kutoa hotuba za kuchochea mambo ya fujo kila jamii inahitaji amani duniani” alisema Sheikh Jongo

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Mpinga Gyumi aliwataka maimamu na mashekhe wa misikiti wa Mkoa wa Kusini Unguja kutoa hotuba ambazo hazifungamani na upande wowote wa kisiasa ili kuendeleza amani kwa wanajamii nchini.

Aidha alisema Jeshi la Polisi litahakikisha wananchi wote wanakuwa salama na halitaruhusu mtu yeyote ama kikundi chochote kuwanyima wanajamii waliowengi  haki zao za  kisiasa kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.